loader
KIKWETE ATAKA SAYANSI, TEKNOLOJIA VITUMIKE KUFUNDISHA

KIKWETE ATAKA SAYANSI, TEKNOLOJIA VITUMIKE KUFUNDISHA

RAIS mstaafu, Dk Jakaya Kikwete amesema matumizi ya sayansi na teknolojia ni muhimu katika ufundishaji ili kuendana na mahitaji ya sasa duniani.

Dk Kikwete alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa 12 wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMeT).

Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau wa elimu kutoka nchi za Tanzania, Malawi, Zimbabwe, Lesotho, Uganda na Kenya.

Alisema nchi zinazoendelea zipo nyuma katika matumizi ya teknolojia kwani hadi sasa bado zinatumia chaki kufundishia, wakati mataifa yaliyoendelea yanatumia vishkwambi.

Dk Kikwete alisema hivi sasa elimu si ajenda ya kitaifa tu, bali kimataifa kwa kuwa dunia ni kama kijiji.

“Mbali na matumizi ya chaki watoto wengi hawamalizi shule kutokana na changamoto mbalimbali, kwani watoto zaidi ya milioni 263 walitakiwa kuwa shuleni lakini hawapo wakiwemo milioni 100 barani Afrika,” alisema.

Dk Kikwete alisema utafiti uliofanywa na Tume ya Kimataifa ya Elimu ambayo yeye ni mjumbe unaonesha elimu inayotolewa Afrika imetolewa kwa nchi zilizoendelea miaka mingi iliyopita.

Akizungumzia changamoto ya ugonjwa wa covid 19, Dk Kikwete alisema shule nchini zilifungwa na watoto walikaa nyumbani bila kuendelea na masomo.

“Kwa nchi zilizoendelea zikiwamo Sweden, Amerika na nyinginezo, wanafunzi waliendelea kusoma online na kuhitimu online, kwa nchi zinazoendelea watoto walibaki nyumbani na kucheza rede. Hivyo matumizi ya teknolojia ni ya muhimu katika nyanja zote,” alisema Dk Kikwete.

Alishauri kuangaliwa njia za ubunifu ili kuboresha elimu na kila shule ijiunge na mtandao wa intaneti ili kurahisisha ufundishaji na ufundishwaji.

Alitaja changamoto katika sekta ya elimu kuwa ni pamoja na elimu jumuishi inayojumuisha wanafunzi kulingana na mahitaji.

Dk Kikwete alitaja jambo jingine ni namna ya kubadilisha elimu ya Tanzania iingie katika mfumo wa kidijitali kwa sababu dunia inabadilika.

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Elimu, Ochola Wayoga alisema mkutano huo wa kimataifa ni wa kutathmini elimu bora Tanzania na kupata uzoefu kutoka nchi nyingine hasa namna ya kutatua changamoto za sekta hiyo.

“Tuna changamoto nyingi kwenye sekta ya elimu lakini haziwezi kutatuliwa kwa mara moja labda baada ya miaka mitano kama nchi itajipanga vizuri,” alisema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/9d1afa23517f1bc79684926c891f9406.jpeg

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi