loader
Ziara ya Samia Kenya ilivyoleta matumaini

Ziara ya Samia Kenya ilivyoleta matumaini

RAIS Samia Suluhu Hassan, alifanya ziara rasmi ya kikazi nchini Kenya ambapo, pamoja na mambo mengine, imeleta matumaini kwa nchi zote mbili baada ya viongozi wakuu wa nchi hizi mbili kusaini mikataba ya kibiashara na uimarishaji wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa na huduma.

Ziara ya Samia imeonekana kuchangia sehemu kubwa katika kufungua milango ya kibiashara kati ya Tanzania na Kenya na kuondoa dhana na hofu zilizokuwepo kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili haukuwa mzuri.

Akiwa ziarani nchini Kenya, Rais Samia alipata fursa ya kuhutubia kongamano la biashara kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya lililofanyika jijini Nairobi kwa lengo la kujadiliana masuala yahusuyo fursa za kibiashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania na Kenya.

AIS Samia Suluhu Hassan, alifanya ziara rasmi ya kikazi nchini Kenya ambapo, pamoja na mambo mengine, imeleta matumaini kwa nchi zote mbili baada ya viongozi wakuu wa nchi hizi mbili kusaini mikataba ya kibiashara na uimarishaji wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa na huduma.

Ziara ya Samia imeonekana kuchangia sehemu kubwa katika kufungua milango ya kibiashara kati ya Tanzania na Kenya na kuondoa dhana na hofu zilizokuwepo kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili haukuwa mzuri.

Akiwa ziarani nchini Kenya, Rais Samia alipata fursa ya kuhutubia kongamano la biashara kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya lililofanyika jijini Nairobi kwa lengo la kujadiliana masuala yahusuyo fursa za kibiashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania na Kenya.

Halikadhalika, aliangalia namna ya kukabiliana na changamoto zinaowakabili wafanyabiashara wa nchi hizo mbili.

Rais Samia katika ziara hiyo alisisitiza umuhimu wa nchi hizo mbili kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kudumisha undugu uliopo baina ya mataifa hayo.

Akihutubia mabunge ya Kenya; Bunge la Taifa pamoja na Bunge la Senate mara baada ya kumalizika kwa kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya, Rais Samia alisema: “Kenya na Tanzania siyo wapinzani kama inavyosemekana. Wanaosema mambo haya ni watu wenye mioyo ya choyo na maono mafupi.”

Mbali na kukutana na wafanyabiashara pamoja na kuhutubia Bunge la Kenya, Samia pamoja na mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta walikubaliana mambo kadha kadha kwa ajili ya mustakabali mzuri wa baadaye wa nchi hizi.

Kuimarisha ushirikiano

Rais Samia aliahidi kwamba katika uongozi wake atahakikisha kuwa Kenya inaendelea kushirikiana na Tanzania na inabakia kuwa ndugu, jirani, mshirika wa mkakati ambao utaufanya uhusiano kati ya Tanzania na Kenya kuendelea kuimarika zaidi.

Alisisitiza kwamba uhusiano wa Tanzania na Kenya umefungwa katika mambo matatu ambayo ni undugu wa damu usioweza kutenganishwa na mipaka ya kuchorwa kwenye ramani, suala la kihistoria na kijiografia.

“Ushirikiano wetu si wa hiari bali ni wa lazima kutokana na kanuni ya uasili wa undugu ambao Mwenyezi Mungu ameuumba, ushirika na ujirani yote yanatufanya tuwe pamoja na hatuna uwezo wa kulibadilisha, kilichobaki ni tupendane au tuchukiane. Hatuwezi kukwepa kutokana na mambo haya matatu yaliyowekwa pamoja, tunategemeana kwa kila hali, iwe heri au shari,” alisema Rais Samia.

Rais Samia aliongeza kuwa Tanzania inalenga kuhakikisha kwamba wawekezaji wa kigeni wanajenga imani na kuwekeza na tayari serikali imeanzisha miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ya miundombinu kama barabara, reli na bandari ili kupunguza gharama za usafirishaji na za kufanya biashara.

Miradi ya pamoja

Rais Samia na Rais Kenyatta pia walikubaliana, pamoja na mipango mingine, kushirikiana maendeleo ya mradi wa usafirishaji wa gesi asilia kutoka Tanzania hadi Kenya, kuondoa vikwazo visivyo vya kodi kati ya nchi hizo mbili ili kurahisisha biashara na kukuza uwekezaji na utalii.

Viongozi hao pia walikubaliana kuharakisha utekelezaji wa mtandao wa usafiri wa anga, reli, majini na wa barabara, na pia kuongeza ushirikiano katika utamaduni, sanaa, ujumuishaji wa kijamii na urithi wa kitaifa pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, hususan ujenzi wa barabara ya kutoka Bagamoyo, katika Pwani ya Tanzania hadi Malindi, katika Pwani ya Kenya.

“Pia tumesema tutaweka kipaumbele cha kuharakisha barabara kutoka Malindi, Lungaluunga mpaka tufike Bagamoyo. Pia tutaanzisha safari za Ziwa Victoria wakati wananchi na mizigo inayopita kutoka Jinja, Kisumu, Mwanza na Bukoba, ili kurahisisha biashara za wananchi wetu,” alisema Rais Kenyatta.

Aidha, pia marais hawa wa nchi hizi mbili walikubaliana kuendelea kuimarisha sekta za biashara na uwekezaji, madini, nishati, mifugo, uchukuzi, ulinzi na usalama, pamoja na kupambana na ugaidi na uhalifu uliopangwa kimataifa, kwa faida ya pande mbili za nchi hizi na watu wao.

Mahindi kuruhusiwa Kenya

Akihutubia kongamano la wafanyabiashara lililofanyika jijini Nairobi, Rais Uhuru Kenyatta katika hatua ya kumhakikishia mgeni wake nia ya Serikali yake ya kuzuia kabisa uwezekano wa biashara kati ya nchi hizo kudhoofika, aliagiza mahindi yaliyozuiliwa mipakani kutoka Tanzania kuruhusiwa kuingia Kenya.

‘’Hayo mahindi yaliyozuiliwa mpakani, Waziri anayehusika mimi nakupatia wiki mbili… Yote yafunguliwe na hayo maneno yaishe,’’ alisema.

Maaguzo na uamuzi huo wa Rais Uhuru ulipokelewa kwa mtazamo chanya na wakulima na wafanyabiashara wa mahindi kutoka Tanzania.

Viza za biashara

Hatua ya Kenya kutangaza kuwa wafanyabiashara wa Tanzania waruhusiwe kuingia nchini Kenya bila ya kuhitaji viza za kibiashara ili mradi tu wahahakishe kuwa sheria, taratibi na kanuni zinazingatiwa imeonekana kuwafurahisha wafanyabiashara na wawekezaji wengi wa Watanzania waliokuwepo ukumbini kwani wengi wao walilalamika kucheleweshwa kutokana na suala hilo la viza za kibiashara.

Rais Samia katika hotuba yake na wafanyibiashara hao wa Tanzania na Kenya alisema Serikali ya Tanzania itatathmini na kuhakikisha kwamba utaratibu wa kuwekeza na kufanya biashara nchini Tanzania unarahisishwa na kuwa na mazingira mazuri ili kuwavutia wawekezaji wengi.

Rais Samia alisema Tanzania kwa sasa inatekeleza mageuzi kadhaa ili kuhakikisha kwamba mazingira ya biashara yanaboreshwa.

Aliema mageuzi hayo yanahusu tathmini mpya ya kodi, kurahisisha utoaji wa vibali vya kufanya biashara na uwekezaji kwa wawekezaji wa kigeni na kutathmini usimamizi mzuri wa mfumo wa kodi na wawekezaji kupatiwa maeneo (ardhi) ya kuwekeza kwa wakati.

Utangamano wa kila mara

Rais Kenyatta alisema walikubaliana kuwa Tume ya pamoja ya mawaziri wa nchi hizo mbili iwe inakutana mara kwa mara ili kutatua changamoto za kibiashara na uhusiano zinatazotokea.

“Wakati wawekezaji wanakuja kutoka Tanzania au Kenya, tuhakikishe kwamba tumeimarisha masuala ya kibiashara, kiuchumi na kitamaduni ambayo yatatusaidia kujenga mataifa yetu kwa manufaa yetu sote,” alisema Rais Kenyatta.

Rais Samia alitumia ziara hiyo kumwalika Rais Uhuru kuwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yatakayofanyika Desemba 9, 2021.

Akihutubia Mabunge ya Kenya wakati wa ziara yake hiyo, Rais Samia alieleza kufurahishwa kwake na uamuzi wa mabunge ya Kenya kutumia lugha ya Kiswahili wakati wa kuendesha shughuli zao.

“Niwaeleze wazi kuwa tulifurahishwa sana na uamuzi wenu wa kuanza kutumia lugha ya Kiswahili bungeni. Hiyo ndiyo inayonifanya nisikilize vikao vya Bunge la Kenya. Ninapenda Kiswahili chenu... Ni burudani ya kutosha. Nilikuwa nikisikiliza hapa wakati Spika akijitahidi kutaja nambari za mwaka kwa Kiswahili,” alisema Rais Samia.

Kuboresha Jumuiya ya Afrika Mashariki

Katika ziara hiyo Rais Samia aliweka wazi kwamba dhamira yake ni kuboresha uhusiano sio tu wa Taifa lake na Kenya bali kuboresha ushirikiano wao kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Kila mara panapotokea kutoelewana kati yetu tunadhoofisha uhusiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, bila kukusudia pia tunaathiri umoja wa Afrika Mashariki, hivyo hatuna budi kuendelea kuelewana na kushikamana kama wanachama wa jumuiya moja,” alisema Rais Samia.

Ziara ya Rais Samia nchini Kenya imeleta matumaini makubwa kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki bado ipo imara na katika mkondo wa pamoja kufanikisha malengo yake na majukumu yake kwa jamii ya wanaAfrika Mashariki kimataifa.

Ni wazi kuwa kufanyika kwa ziara hiyo kulipokelewa kwa shangwe kubwa nchini Kenya ambako wananchi wake walionesha kufurahishwa na ziara hiyo ya siku mbili.

Katika siku hizo mbili takribani vyombo vyote vya habari, hususani redio na televisheni nchini humo vilijikita katika kuzungumzia ziara hiyo.

Mwandishi ni Ofisa Habari, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

 

 

foto
Mwandishi: Sheiba Bulu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi