loader
Dstv Habarileo  Mobile
Maagizo mazito kwa Ma-RC

Maagizo mazito kwa Ma-RC

RAIS Samia Suluhu Hassan amewaapisha wakuu wa mikoa na wakuu wa taasisi aliowateua Mei 15 mwaka huu na muda mfupi, baadaye akafanya nao kikao kazi, Ikulu Dar es Salaam.

Aidha, Rais Samia amefanya mabadiliko kwa wakuu wa mikoa wawili akiwemo John Mongella aliyemuhamishia Simiyu kutoka Mwanza, lakini akamuhamisha tena hiyo jana kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

David Kafulila aliyekuwa ameteuliwa awali kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, amehamishiwa katika Mkoa wa Simiyu.

Alisema sababu ya kuwabadilisha mikoa yao ni kutokana na uzoefu wa kazi kwa kuwa Mongella alitoka kwenye Mkoa wa Mwanza ambao ni mkubwa, lakini pia ni jiji, hivyo akampeleka Arusha ambao pia ni jiji.

Kwa mujibu wa Rais Samia, kwa kuwa Kafulila aliwahi kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, amempeleka katika Mkoa wa Simiyu.

Samia aliwataka viongozi aliowaapisha jana kumtanguliza Mungu kwa kuwa majukumu waliyokabidhiwa ni mazito.

Miongoni mwa viongozi aliowaapisha jana ni Pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine.

Wengine ni Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kamishina wa Polisi Salum Hamduni.

Wengine aliowapisha ni wakuu wa mikoa 10 akiwemo Amos Makala anayekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Mongella (Arusha), Omary Mgumba (Songwe), Stephen Kagaigai (Kilimanjaro), Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (Ruvuma), Makongoro Nyerere (Manyara), Meja Jenerali Charles Mbuge (Kagera), David Kafulila (Simiyu), Rosemary Senyamula (Geita), Mwanamvua Mlindoko (Katavi) na Queen Sendiga Mkoa wa Iringa.

Rais Samia pia alimwapisha Joseph Pande kuwa Naibu DPP na Neema Mwakalyelye kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru.

Makamu wa Rais

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliwataka wakuu wa mikoa wasimamie uchumi katika mikoa yao, waongeze uzalishaji wa kilimo, wahakikishe viwanda vinakuwa na kuongeza tija; pamoja na kusimamia masoko ya wananchi hasa wakulima.

Dk Mpango pia aliwataka wakuu hao wa mikoa kuyaelewa, kuyajali na kuyashughulikia matatizo ya wananchi pamoja na kufanya maamuzi kwa kuzingatia sheria na miiko ya kazi zao.

“Mkawashughulikie wazembe, wabadhirifu na wale wasio na nidhamu. Ila angalizo langu ni  moja tu, msitumie madaraka yenu vibaya, msionee watu, mkatende haki, “ alisema Dk Mpango.

Akasisitiza: “Kiongozi lazima uwe hodari wa kazi na mfano wa tabia. Viongozi ambao mmepewa dhamana hii leo na wengine mliopo, tusiende huko kwenye vituo vyetu vya kazi halafu tukawa mifano mibaya, hatuchapi kazi kama tunavyopaswa, sitarajii kwamba kutakuwa na walevi kati yenu au wazinzi.”

Waziri Mkuu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema mbali na kusimamia masuala ya ulinzi na usalama katika mikoa yao, wakuu wa mikoa pia wakasimamie ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na matumizi yake.

“Pia zipo fedha kutoka Serikali Kuu kuja kwenye maeneo yenu kwa ajili ya miradi, hakikisheni fedha hizo zinatumika kwenye miradi kama ilivyokusudiwa,” alisisitiza Majaliwa.

Spika wa Bunge

Pamoja na kuwapongeza kwa uteunzi walioupata na kiapo walichokula jana, Spika wa Bunge, Job  Ndugai, aliwataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kutojiita marais katika maeneo yao kwa kuwa katika nchi yupo Rais mmoja pekee ambaye ni Samia Suluhu Hassan.

“Wapo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya wanaamini kabisa kule waliko wao ni marais, utawasikia mimi rais wa mkoa huu, mimi rais wa wilaya hii, nani amesema? Katika Jamhuri ya Muunngano wa Tanzani Rais ni Samia Suluhu Hassan tu, usije ukajidanganya kuwa we ni rais…,” alisema Ndugai.

Jaji Mkuu

Katika kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa haraka mahakamani, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, aliwataka DPP Sylvester Mwakitalu na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishina Hamduni kuhakikisha masuala ya upelelezi hayawi kikwazo kwa mahakama kutekeleza wajibu wake.

Profesa Juma alisema mnyororo wa haki unaanza na ngazi ya upelelezi na kuhitimishwa mahakamani, hivyo ucheleweshaji wowote wa upelelezi unaathiri utoaji haki mahakamani.

“Ninyi ndiyo mnavaa viatu vya utoaji wa haki, tunapozungumzia haki, haki inaanzia kwenye ngazi ya upelelezi na haki ya mwisho inapatikana mahakamani, DPP wewe ni mtu muhimu sana katika mfumo wa utoaji haki na kikatiba hupaswi kuingiliwa na mtu yeyote,” alisema Profesa Juma.

Alisema kazi za DPP ni pamoja na kuwa na nia ya kutenda haki, wajibu wa kuzuia matumizi mabaya ya taratibu katika mfumo wa utoaji haki pamoja na kuangalia maslahi ya taifa, hivyo anapaswa kuwa mtu wa busara ya hali ya juu.

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi