loader
Dstv Habarileo  Mobile
WIZARA, IDARA WAAGIZWA KUVILIPA VYOMBO VYA HABARI

WIZARA, IDARA WAAGIZWA KUVILIPA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza wizara na idara zote za serikali ambazo hazijalipia matangazo kwenye vyombo vya habari zifanye hivyo mara moja.

Taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu jana ilieleza kuwa, Waziri Mkuu alitoa aliagiza hilo jana Morogoro wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 10 wa Jukwaa la Wahariri na Kongamano la Kitaaluma.

“Ikiwa tangazo limefuata utaratibu kuanzia upatikanaji wake hadi kuchapishwa linapaswa kulipiwa mara moja. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nataka muangalie tatizo liko wapi na lipatiwe ufumbuzi,” alisema Majaliwa.

Hata hivyo, alivihimiza vyombo vya habari vizingatie uzalendo, utaifa, weledi na maslahi ya nchi katika kufanya kazi na kuonya kuwa serikali haitamvumilia yeyote atakayemkwaza mwandishi wa habari katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Niwahakikishie kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yake na serikali itaendelea kuimarisha misingi ya habari nchini. Kwa upande wenu wanahabari zingatieni sheria za nchi, msitumie vibaya kalamu zenu kuwachafua watu kwa chuki binafsi,” alisema Majaliwa.

Alisema serikali itaendelea kufanya kazi na vyombo vya habari na kuwashirikisha kikamilifu katika utekelezaji wa mipango ambayo hutekelezwa kwa mipango ya muda mfupi.

“Katika kuandaa mkakati wa utekelezaji wa mpango wa maendeleo wanahabari mtashirikishwa kama wadau wengine kwani kwa kufanya hivyo mtaweza kuufahamu na kuwaelimisha wananchi kikamilifu,” alisema Majaliwa.

Aliwataka wahariri wa vyombo vya habari wazingatie weledi na maadili katika uandishi wa habari ili umma upate habari zenye ubora.

Majaliwa alisema utendaji unaozingatia weledi ni chachu ya kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na wamiliki wake.

“Kaulimbiu yenu ya Vyombo vya Habari na Maendeleo inahamasisha uandishi wa uwajibikaji. Vyombo vya habari vinapaswa kutambua katika kila habari vinayoiandika kuwa nyuma yake kuna maslahi ya taifa. Visipofanya hivyo, upotoshaji unaweza kuigawa nchi yetu, kuhatarisha amani na mshikamano wetu,” alisema Majaliwa.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Morogoro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi