loader
Dstv Habarileo  Mobile
Pongezi kwa serikali kwa kusimamia maneno yake

Pongezi kwa serikali kwa kusimamia maneno yake

JULAI 2019, Rais Johm Magufuli, alizindua mradi mkubwa wa uzalishaji umeme katika Mto Rufiji licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa mataifa ya kigeni na asasi za mazingira zinazoukosoa  kwa madai kuwa unatekelezwa huku ukiharibu mazingira.

Mradi huo unaotarajiwa kuanza uzalishaji wa nishati hiyo Juni mwakani, utakuwa mradi mkubwa kuliko yote nchini wa umeme kwa sababu unategemewa kuzalisha megawati zaidi ya 2,000 na unajengwa kwa gharama ya shilingi trilioni 6.5 fedha za ndani.

Kutekelezwa kwa mradi huo kunatoa mwanga nchini kwani wazo lake lilikuwepo yapata miaka 40 sasa na lilibuniwa na Rais Julius Nyerere wa awamu ya kwanza.

Ujenzi wake sasa unatekelezwa chini ya wakandarasi kampuni ya Misri ambao nao kabla ya kuanza kuutekeleza walitoa taarifa yao wakisema hauna madhara yoyote ya mazingira kama ilivyodaiwa hapo awali na baadhi ya wanaharakati wa mazingira na mataifa ya kigeni.

Kutekelezwa kwake ni hatua nzuri, kwa sababu nchi inahitaji umeme wa uhakika kuendesha viwanda, migodi, biashara mbalimbali, matumizi ya nyumbani na hata shughuli nyingine za uzalishaji mali.

Hivi juzi Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani akifuatana na Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Misri, Dk Assem El-Gazzar walitembelea mradi huo mkoani Pwani na kuona shughuli za ujenzi zikiendelea na kwa sasa ujenzi wake maeneo muhimu ya kuzalisha umeme umefikia asilimia 52.8.

Hivyo Dk Kalemani akasema mradi huo utakamilika kwa wakati na kuanza uzalishaji wa umeme Juni mwakani kama ulivyopangwa.

Hiyo ni taarifa njema kwa watanzania, kwa sababu baadhi ya watu walikuwa wakinong’ona iwapo mradi huo utakamilika kwa wakati kama ulivyotajwa wakati wa uzinduzi wake.

Jambo la msingi kwa watanzania na mamlala mbalimbali ni kuhakikisha kuwa mradi huo unapokamilika, unalindwa na mamlaka husika zianze mapema maandalizi ya kuimarisha mifumo na usafirishaji umeme kwa sababu kilio kikubwa cha sasa ni uchakavu wa miundombinu ya kusafirishia nishati hiyo.

Hivyo ni vyema basi, Shirika la Umeme Tanzania , wizara na serikali kwa ujumla ikajipanga kuhakikisha inafumua mifumo yote ya usafirishaji wa umeme ya zamani na kuweka mifumo mipya ambayo itakuwa na uwezo wa kupokea na kusafirisha umeme bila kikwazo ili kuifanya nchi iwe na nishati ya uhakika isiyokatika mara kwa mara kutokana na hitilafu mbalimbali.

Nasema hayo kwa sababu hivi karibunu maeneo mengi ya nchi yalipata tatizo la kukatika kwa umeme kunakosababisha na matengenezo au kufanyiwa ukarabati kwa njia za umeme ambazo nyingi kwa mujibu wa Tanesco wenyewe na hata wizara zimechakaa na za zamani.

Sasa basi, kwa  huu umeme unaotarajiwa mwakani kutoka Mto Rufiji tuanze kujipanga mapema kwa kuweka mifumo yetu ya kusafirishia umeme vizuri  ili uzalishaji ukianza kusiwe tena na vikwazo kwenye hilo bali uzalishwe na kusambazwa kwa wingi maeneo yote na kuibadilisha nchi.

Tanzania imepiga hatua katika ukuaji wa kipato kutoka cha chini kwenda cha kati hivyo kuendelea kupanda na kuwa juu zaidi kiuchumi kutatokana na kuboreka pia kwa huduma muhimu kama nishati, afya,elimu ,maendeleo ya jamii na mengine kama hayo.

Viwanda vingi hivi sasa vinaendelea kujengwa na Tanzania imekuwa kivutio kwa wawekezaji wa ndani na nje kutokana na mazingira bora ya uwekezaji, ardhi yenye rutuba, siasa safi, demokrasia ,uhuru, utulivu na amani hivyo uhakika wa nishati ya umeme ni muhimu zaidi kuhakikisha viwanda hivyo vinapata nishati ili kufanya kazi zao kwa uhakika.

Kauli ya Dk Kalemani ya kuhakikishia umma kuwa umeme utaanza kuzalishwa Juni mwakani , inatia faraja na inaonesha jinsi serikali inayvosimamia ahadi zake katika kuwaletea maendeleo wananchi na hivyo watanzania nao wanapaswa kujipanga ili uzalishaji wa umeme huo utakapoanza ulete tija .

Hiyo ina maana viwanda viunganishwe nishati hiyo na kuongeza uzalishaji, wananchi wabuni miradi inayotumia nishati hiyo  kuongeza tija na thamani, viwanda vya kuongeza thamani ya mazao vijengwe ili kuondoa ule utaratibu wa kuuza malighafi kwa bei ndogo na kuuza bidhaa kamili kwa bei nzuri yenye tija kwa wazalishaji.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6f891bfa40245fd4f1ffd550510896da.jpeg

TAARIFA za matukio ya mimba na ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi