loader
Mbowe ataka Chadema wasilipize kisasi

Mbowe ataka Chadema wasilipize kisasi

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametoa rai kwa wanachama wake kutobeba visasi ndani ya mioyo yao, bali kumshukuru Mungu kwa mambo yalitokea mwaka jana.

Amesisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kudai Katiba mpya na kutoshiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 endapo marekebisho ya Katiba mpya hayatafanyika.

Mbowe aliyasema hayo jana jijini hapa wakati wa uzinduzi wa “Chadema Digital App” ambayo ni kadi maalumu aina tano za uanachama wenye rangi tofauti na viwango vya ulipiaji kadi hizo sanjari na kupata wanachama nchi mzima.

Alisema kisasi hakijengi na endapo wana-Chadema wakiamua kulipiza visasi, atajiondoa uenyekiti kwa madai hapendi kuona visasi vikiendelea kwani Mungu wanayemuamini hujibu kwa wakati au kwa namna tofauti tofauti.

Alisema endapo wataamua kulipiza visasi kwa madhila yaliyokutana nayo ni kukosa baraka za Mungu kwani yeye mwenyekiti wao alifanyiwa visasi vingi, lakini ana imani kubwa kuliko jana.

“Binafsi nimefanyiwa visasi vingi, lakini nimeimarika leo kuliko jana na nawaomba msilipize kisasi, bali Mungu anajibu kwa njia tofauti, lakini pia tunadai Katiba mpya na hatushiriki uchaguzi wowote ule hadi katiba irekebishwe maana iliyopo inakandamiza baadhi ya mambo,” alieleza kiongozi huyo.

Alisema chama hicho kitafanya siasa za ushindani na haki lakini bila uwepo wa Katiba mpya hawatashiriki katika chaguzi zote huku akisisitiza kutoa nafasi kwa tume huru ya uchaguzi kujitafakari na kusahihisha mapungufu yaliyopo

“Tuna imani na Rais Samia Suluhu na tunamuomba atengeneze amani na tupate suluhu ndani ya mioyo yetu kwani kauli zako za kutaka uwepo wa amani ni njema bali tunaomba tupone katika maumivu tuliyopitia,” alisema Mbowe.

Akisisitiza msamaha, alisema “Lazima tuwe majasiri…msiogope wanaohama vyama hiyo ndio siasa kila mtu anaingia na kutoka. Sasa wanaokuja tuwapokee hatuwezi kujua huko walipoondoka kwenda kwenye vyama vingine walipata madhila gani na nawaambia Mzee Lowassa alikuwa ni mtaji mkubwa kwetu sababu alitusababishia kupata wabunge wengine alipojiunga na Chadema.”

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/b342cd6386ca91bce3e8d5df9b92e7ae.jpeg

UMOJA wa Vijana wa Chama ...

foto
Mwandishi: Veronica Mheta, Arusha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi