loader
Wahitimu waliokacha kiapo wamchefua JK

Wahitimu waliokacha kiapo wamchefua JK

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amewataka wahitimu wote wa Shahada ya Udaktari wa Binadamu ambao hawakufika na kula kiapo kwenye Mahafali ya 51 ya chuo hicho jana, kutokujihusisha na shughuli ya udaktari mpaka pale watakapoapa.

Aidha, ameagiza wahitimu hao kuhudhuria kwenye Mahafali ya Ndaki ya Afya na Sayansi Shirikishi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (MUHAS) yatakayofanyika Novemba 27, mwaka huu jijini Mbeya ili kuapa kiapo hicho.

Katika mahafali ya jana, wahitimu 228 wa udaktari walipaswa kuapa miongoni mwa waliohitimu 564 wa kozi mbalimbali.

Kikwete ambaye ndiye aliyekuwa anatunuku shahada kwa wahitimu hao katika hafla hiyo ya katikati ya mwaka, alitoa maagizo hayo na kuwataka wahitimu waliohudhuria kuorodheshwa ili wale wasiohudhuria wasifanye shughuli hiyo sehemu yoyote mpaka watakapoapa.

“Kama hawatakula kiapo hawataruhusiwa kuingia na kufanya kazi katika hospitali yoyote,” alisema Kikwete.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Bonaventure Rutinwa aliwataka wahitimu hao wa udaktari kujiorodhesha ili wale wasiofika wapewe utaratibu wa jinsi gani watakamilisha hilo.

Makamu Mkuu wa chuo, Profesa William Anangisye alisema UDSM imejidhatiti kutoa elimu bora yenye manufaa kwa wahitimu, vizazi vyao pamoja na jamii kuwawezesha kukabiliana na mabadiliko yanayoendelea nchini na dunia.

Alisema chuo hicho kimewaandaa wahitimu hao vya kutosha kwa ajili ya kujumuika na jamii ya Watanzania katika kutafuta maendeleo lakini kimewapatia maarifa ya kutumia katika kuendeleza mabadiliko nchini na duniani.

Aliwataka wahitimu hao kutosubiri kuajiriwa na serikali bali wawe wepesi kuangalia ni wapi ujuzi wao unaweza kutumika kwa ufanisi zaidi hata kama itabidi wafanye kazi za kujitolea.

“Kwa kufanya hivyo mtajenga kujiamini, ujuzi na mchango wao utatambuliwa na kuinufaisha jamii. Kwa wale mnaorudi kwenye vituo yenu vya kazi ni matarajio yetu kuwa mnaenda kuongeza tija katika majukumu yenu ya kila siku,” alisema Profesa Anangisye.

Mwenyekiti wa Baraza la chuo, Damian Lubuva alisema limeidhinisha sera na mapendekezo mbalimbali na kutoa ushauri na maelekezo kwa chuo ili kuhakikisha lengo la utoaji elimu, utafiti na ushauri wa kitaalamu linafanikiwa.

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi