loader
Programu ya ‘Kilimo Viwanda’   inavyochangia ukuaji uchumi

Programu ya ‘Kilimo Viwanda’  inavyochangia ukuaji uchumi

KILIMO ni sekta kubwa kuliko zote nchini na ndio sekta inayoongoza kwa kutoa ajira nyingi kwa Watanzania. 

Mwandishi Philipo F. Mrutu katika kitabu chake ‘Kilimo Biashara na Ujasiriamali’ kilichopo mtandaoni anasema: “Kilimo kinatoa fursa ya mtu kujiajiri mwenyewe, kuajiriwa au kuajiri watu wengine.”

Anaongeza: “Wapo wataalamu wanaoajiriwa kutokana na fani zao ili kutoa ushauri wa kitaalamu (consultancy), kufundisha, utafiti au ajira kwa vibarua wa kawaida kufanya shughuli za uzalishaji shambani n.k. Takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 65 ya watu wanapata ajira kwenye kilimo moja kwa moja au kupitia njia nyingine (indirect).”

Aidha, takwimu kutoka vyanzo mbalimbali zinaonesha kuwa, takribani asilimia 70 ya ajira nchini, zinaanzishwa na kutengenezwa na kilimo. 

Wakati sekta hii ikichangia asilimia 27 ya pato la ndani la taifa, vyanzo mbalimbali vinasema pia inachangia kwa takriban asilimia 60 ya upatikanaji malighafi za viwandani. Ikumbukwe kuwa, Tanzania ipo katika kasi ya kuelekea katika uchumi wa viwanda.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewahi kunukuliwa akisema haridhishwi na tija iliyopo katika sekta ya kilimo. 

Alisema hekta moja huzalisha tani 1.9 tu na kuonesha kusikitishwa na hali hii na kuongeza kuwa, Serikali itatilia mkazo kilimo chenye tija kwa kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji kinafanyika kwa zaidi ya hekta milioni moja kufikia mwaka 2025.

Aprili 22, 2021 wakati akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia alisema serikali yake itaboresha sekta mbalimbali ikiwemo kilimo kwa kujenga miundombinu imara ya kilimo na kutafuta masoko ili kuwezesha wakulima kufanya kilimo kikubwa na chenye tija zaidi.

Hata viongozi wengine yaani wasaidizi wa Rais, akiwamo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wamekuwa wakiwahimiza Watanzania kuachana na kilimo cha mazoea na badala yake, wajikite na kuendesha kilimo cha kisasa, kilimo cha kitaalamu; kilimo chenye tija.

Akiwa mkoani Singida Septemba 15, 2020, Majaliwa alisema: “Wananchi ingieni kwenye kilimo chenye tija ili muinue kipato chenu.”

Viongozi na wataalamu wa uchumi sasa wanasisitiza Watanzania kujikita katika kilimo hicho kinachotumia eneo lilelile, kupata mazao mengi zaidi kutesheleza mahitaji ya chakula na hata biashara yaani, ‘kilimo biashara.’

Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba zaidi ya asilimia 60 ya mali ghafi za viwandani, hasa kwa nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, zinatoka shambani; katika kilimo hivyo, ni sekta inayohitaji kuungwa mkono na watu na taasisi mbalimbali ili kifanyike nchini kwa tija. 

Ikumbukwe kuwa, ili kuendeleza viwanda, lazima kuongeza nguvu ya uzalishaji katika kilimo ili mazao yatokanayo na kilimo yatosheleze mahitaji ya viwanda na mahitaji ya watu kwa chakula na vitu vingine, hivyo licha ya  uzalishaji, lazima pia kuangalia na kuzingatia ubora wa bidhaa. 

Kufanikisha hili, lazima wakulima wapate elimu na waifuate tangu hatua za awali katika kulima, mbolea, palizi, ukuzaji, uangalizi, usafirishaji, upakiaji au uhifadhi hadi mlaji anapopata mzigo katika mnyororo wa thamani wa bidhaa husika.

Jambo hili muhimu linaitaka nchi kuwa na wataalamu wengi wa kilimo katika ngazi na maeneo mbalimbali. 

Kufanikisha hili nchini, wapo wadau wanaoiunga mkono serikali kwa namna mbalimbali ikiwamo ya utoaji elimu na hata upatikanaji wa soko kwa wakulima kupitia utumiaji wa mazao ya kilimo kutoka kwa wakulima na kuyatumia kuzalisha bidhaa mbalimbali, inayowezesha serikali kwa kuwapa wakulima soko la uhakika.

Wadau hao muhimu kwa uchumi wa nchi ni pamoja na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) ambayo ni moja kati ya watumiaji wakubwa wa malighafi zinazotokana na kilimo zinazotumika kuzalisha bia nchini yaani shayiri, mahindi na mtama.

Mbali na utoaji wa soko la uhakika kwa wakulima wa mazao hayo, SBL pia imekuwa ikijitahidi kuunga mkono jitihada za kuendeleza kilimo kwa namna tofauti tofauti ikiwa ni pamoja na kuchangia maendeleo ya sekta hii kwa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaosoma kilimo kupitia programu inayojulikana kama ‘Kilimo Viwanda.’

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari na vyanzo mbalimbali, kupitia programu hii SBL imewezesha wanafunzi 71 kupata fursa ya kulipiwa gharama zote za masomo katika vyuo vinne nchini.

Hivyo ni Chuo cha Kaole Wazazi (Kaole Wazazi College of Agriculture) kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani, Chuo cha Mtakatifu Maria Goretti (St. Maria Goretti Agriculture Training Institute) kilichopo Iringa, Chuo cha Kilimo na Mifugo Kilacha (Kilacha Agriculture Training Institute) kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro na Chuo cha Igabiro (Igabiro Training Institute of Agriculture) kilichopo Muleba mkoani Kagera.

Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Mark Ocitti, anasema, ufadhili wa masomo unaotolewa na SBL unalenga kuunga mkono jitihada za serikali kuongeza wataalamu wanaohitajika katika sekta ya kilimo ili kuchochea kasi ya ukuaji.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, ufadhili unaotolewa chini ya programu hiyo ni kwa wanafunzi wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini zisizoweza kumudu kuwalipa ada watoto wao kusomea masomo ya kilimo katikangazi ya diploma katika vyuo vya ndani.

Ocitti anasema pamoja na msaada wa kifedha wanaopata wanufaika wa Programu ya Kilimo Viwanda, pia hupata fursa kujifunza zaidi kwa vitendo kupitia programu za kuelekezwa na wataalamu mbalimbali, na kupewa nafasi ya kufanya kwa vitendo jambo linalosaidia zaidi kuwandaa wataalamu wenye weledi wa kutosha.

Wadau mbalimbali wanasema jambo hili husaidia kuwandaa vyema vijana hao kuwa wataalamu wenye weledi wa kutosha katika sekta hii muhimu ya kilimo hasa kipindi hiki taifa lipojielekeza katika uchumi wa viwanda.

Mkurugenzi huyo anasema, SBL ni mzalishaji wa bia mkubwa nchini kwa hutumia nafaka za ndani kutengenezaji bia zake hivyo, kuchangia pato la taifa.

Hivi karibuni alinukuliwa akisema: “Hadi sasa SBL inafanya kazi na mtandao wa wakulima 400 katika mikoa minane nchini.”

Anaongeza: “Tunanunua nafaka kama shayiri, mahindi na mtama kwa ajili ya uzalishaji wa bia zetu. SBL inatumia takribani tani 17,000 sawa na asilimia 70 na mahitaji yao kwa mwaka huku ikilenga kufikisha asilimia 85 kufikia mwaka 2025.”

Pamoja na mambo mengine, programu hii huwapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo kwa kuwapa nafasi ya kutembelea mashamba makubwa yaliyopo chini ya Programu ya Kilimo Biashara; pamoja kutembelea viwanda vya kampuni hiyo kuona namna malighafi kutoka shambani zinavyotumika kutengeneza bia.

Ikumbukwe kuwa, uzalishaji na uuzaji wa bia hutoa ajira tangu shambani, katika mchakato wa usafirishaji wa mazao hayo ambayo ni malighafi, utengenezaji wa bia na hata uuzaji wake, hivyo kuchangia juhudi za serikali kukabili tatizo la ukosefu wa ajira huku uuzaji wa kinywaji hicho ukichangia pato la taifa kupitia kodi.

Katika tukio lililofanyika Mwanza kuwapongeza wanafunzi 17 waliopata nafasi za ufadhili kupitia Programu ya Kilimo Viwanda kutoka Chuo cha Igabiro Training Institute of Agriculture hivi karibuni, Mkuu wa Chuo hicho, Sadock Stephano, anaipongeza SBL kwa kuwa mstari wa mbele kushiriki kuwaandaa vyema vijana watakaokuwa maofisa kilimo wenye ujuzi na maarifa ya kutosha.

“Maarifa hayo watayatumia kuwasaidia wakulima kufanya kilimo chenye tija na hivyo, kupata mazao mengi zaidi,” anasema Sadock.

Anaongeza: “Kwa kweli ipo haja kubwa kampuni nyingine (zinazotegemea mazao ya wakulima) ziige mfano kwa kuwasaidia wanafunzi kutoka familia masikini nchini na zijitokeze kuiga mfano huu wa SBL kusaidia sekta hii mama ili azma ya kufikia uchumi wa kati wa juu ifikiwe mapema.”

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/dcaaf5f36b7b906bb728ad2c232256ad.jpg

NDUGU msomaji katika makala yangu ya leo nimeyakumbuka ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi