loader
MAJALIWA ATOA MAAGIZO 7 KULINDA MAZINGIRA

MAJALIWA ATOA MAAGIZO 7 KULINDA MAZINGIRA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo saba katika kulinda mazingira ikiwamo ya kuziagiza wizara, taasisi na wakandarasi wanaosimamia ujenzi wa majengo nchini, kuyawekewa mfumo maalumu wa kupitisha gesi kama nishati mbadala kwa matumizi ya kupikia.

Pia ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuanzisha kampeni ya upandaji miti kwa maeneo yote yaliyopimwa ambako kila mmiliki wa kiwanja au nyumba atapaswa kupanda mti katika eneo lake.

Majaliwa alitoa maagizo hayo jana jijini hapa wakati akitoa tamko la serikali katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika Juni 5 kila mwaka ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Dodoma.

“Wizara, taasisi na wakandarasi wanaosimamia ujenzi wa majengo, wahakikishe majengo yanayojengwa yanahusisha mifumo ya kupitisha nishati mbadala kama gesi kwa ajili ya matumizi ya kupikia,” alisema Majaliwa.

“Shule, vyuo, hospitali na taasisi za kijeshi nazo zitumie gesi kama nishati mbadala badala ya kutumia kuni na mkaa.”

Alisisitiza kuwa matumizi ya nishati mbadala yatasaidia kuzuia ukataji miti ambao kwa kiasi kikubwa inatumika katika matumizi ya kupikia kama kuni na mkaa.

Pia aliwaagiza watafiti na taasisi za elimu kuendelea kufanya tafiti mbalimbali kubaini njia bora za matumizi ya nishati mbadala, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza teknolojia ya uzalishaji wa mkaa mbadala.

Alisema maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kitaifa yanafanyika Dodoma kutokana na matokeo ya Ripoti ya Hali ya Mazingira nchini 

ya Mwaka 2019, ambayo ilieleza mkoa huo kuwa na eneo kubwa kame kwa sababu ya ukataji miti hovyo, hususan kwa matumizi ya kupikia.

Kwa sababu hiyo, Majaliwa aliuagiza uongozi wa mkoa huo kuweka mkakati wa kuhakikisha maeneo yote yaliyopimwa yanapandwa miti na kila mmiliki wa kiwanja au nyumba kupanda miti katika eneo lake.

Pia alisema kampeni ya utunzaji mazingira ni muhimu pia ikawahusisha wanasiasa kufahamu umuhimu wa kutunza mazingira na kuwaelimisha wafuasi wao pindi wanapowahutubia majukwaani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, alisema kampeni ya mwaka huu kuhusu mazingira itakuwa kabambe kutokana na kuhusisha wadau mbalimbali.

“Tutatoa mafunzo maalumu kwa maofisa mazingira kutoka mamlaka za serikali za mitaa na wizara kwa sababu tumebaini hakukuwepo muunganiko baina ya watendaji hao wa ngazi ya serikali za mitaa na wizarani.”

Alisema kutakuwa na kongamano litakalowakututanisha wataalamu na wadau wa mazingira ili kupata maoni yao kuhusu sera na mikakati ya utunzaji mazingira nchini.

“Kampeni haitoacha kitu. Tunataka kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya kupigiwa mfano katika utunzaji mazingira duni,” alieleza Jafo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/1d300e9cd8eda9399d57a5badc509129.jpeg

RAIS Samia Suluhu Hassan amehutubia taifa ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi