loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wateule wamsaidie vyema Rais Samia

Wateule wamsaidie vyema Rais Samia

JANA Rais Samia Suluhu Hassan aliwaapisha makatibu tawala wa mikoa mbalimbali nchini, huku akiwapa ujumbe mzito wa kuongeza juhudi ya kufanya kazi na sio  kutumia nafasi hizo  kwa maslahi yao wenyewe.

Miongoni  mwa wateule hao sio wapya katika utendaji, wanajua vyema majukumu yao, bali wanachotakiwa ni kusimamia kiapo walichokula siku ya kuapishwa.

Wateule hao wanajua vyema ni kipi wanachotakiwa kufanya na yale ambayo hawatakiwi kufanya,  lakini kubwa wajue kuwa kuwatumikia wananchi kwa haki pamoja na kufanya nao kazi  ni jambo lenye manufaa  kwao na hata kwa kizazi kijacho.

Matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi yanajulikana kwa viongozi mbalimbali na wakati mwingine yakitofautiana kutoka eneo moja hadi nyingine, lakini  wateule hao wanapofika katika vituo vyao vya kazi wasiwatenge wananchi bali washughulikie kero zao kama  inavyostahili.

Wapo baadhi ya wateule wanapokuwa kwenye majukumu yao hawajishughulishi kushughulikia kero za wananchi na wengine wakiwatisha, kuwatia hofu na wakati  mwingine kuvuruga hata shughuli zao zinazowaingizia kipato.

Ni muhimu wateule wakaweka  mazingira bora ya utendaji kazi kwa wanaokwenda kuwatumikia jambo ambalo litarahisisha kufikia malengo waliyojiwekea, lakini pia kurahisisha utekelezwaji wa miradi mbalimbali katika maeneo yao. 

Katika baadhi ya mikoa nchini yapo maeneo ambayo unaweza kukuta migogoro ya ardhi baina ya kiongozi na wananchi, huku kiongozi badala ya kutafuta suluhu anagombana na wananchi kuhusu umiliki wa eneo hilo, huku wananchi wakiachwa wakilalamika.

Kw mantiki hiyo, wateule mnapoenda kwenye maeneo yenu ya kazi mnaenda kukutana na wananchi, wasikilizeni, waelimisheni kadri inavyostahili ili waweze kufuata kinachotakiwa kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi.

Mtatakiwa kuhakikisha mnaishi katika yale mlioapa kwa vitendo ili maeneo mnayokwenda kuyafanyia kazi muweze kuacha alama zilizo nzuri zenye kuigwa na kukumbukwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Ni vyema wateule  wakakumbuka kuwa pindi uteuzi unapofanywa na kiongozi wa nchi, wananchi huamini ni watu waaminifu, waadilifu na wenye kuzingatia maadili mema kwa wanaowatumikia na nchi kwa ujumla.

Haitarajiwi wateule kuingia katika nafasi hizo kwa nyuso zenye bashasha, zenye kuonesha furaha ya uteuzi wa Rais, lakini wakajikuta wakiondolewa katika nafasi zao kwa aibu kwa kutotekeleza yaliyokusudiwa ama kutumika isivyostahili.

Aidha, ni vyema kutambua kuwa kulingana na mabadiliko  mbalimbali ya uongozi wa nchi, wananchi  wa Tanzania  nao wamekuwa wakibadilika kifikra na hata kimtizamo kutokana na kuelimishwa  kujua wajibu wao wa kuchangia maendeleo ya nchi bila kujali misuguano ya vyama vya siasa, hivyo wateule  wasikubali kamwe kuwa sehemu ya siasa za kuwagawa wananchi bali wawe wabunifu na kuwashirikisha katika mambo mbalimbali yanayowahusu.

Viongozi hao watakapo wajibika, ni wazi kuwa yapo mabadiliko yatakayoonekana kwa kuwa miradi itasimamiwa inavyostahili na kero za wananchi zitatafutiwa ufumbuzi.

Wateule na watendaji wengine wa serikali wanatakiwa  kumsaidia Rais na si  kumuangusha katika majukumu mbalimbali.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/28d86702e6134f8965edf4d0746e45ec.jpeg

TAARIFA za matukio ya mimba na ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi