loader
Dstv Habarileo  Mobile
Usalama wa chakula ni jukumu la jamii nzima

Usalama wa chakula ni jukumu la jamii nzima

LEO ni siku ya kimataifa ya chakula, Shirika la Afya Duniani (WHO) linataka kuimarishwa zaidi kwa juhudi za kuhakikisha kuwa chakula ambacho kinaliwa ni salama.

Taarifa ya WHO inasema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa sababu kila mwaka watu milioni 600 duniani kote wanaugua ilhali wengine 420,000 wanafariki dunia baada ya kula chakula kilichoharibiwa na bakteria, virusi, vimelea au dutu zenye kemikali.

Kando ya hayo, chakula hicho kinadumaza maendeleo katika nchi nyingi za kipato cha chini na cha kati ambazo hupoteza takriban dola bilioni 95 kila mwaka kutokana na watu hao kushindwa kufanya kazi kwa sababu ya kuugua na ulemavu utokanao na vyakula visivyo salama.

Ni kwa kuzingatia athari hizo, Shirika la Afya Duniani pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), mashirika yanayoratibu siku hii, yametoa mapendekezo matano ya kuhakikisha chakula kina usalama.

Mapendekezo hayo ni pamoja na serikali kuhakikisha chakula kinakuwa kuwa salama na hivyo wakulima na wazalishaji watumie mbinu bora. Chakula kihifadhiwe salama na hivyo wafanyabiashara wahakikishe usalama kinaposafirishwa, kinapohifadhiwa na kuandaliwa.

Walaji nao wana jukumu kwa kuwa wanatakiwa wakipate kabla hakijaharibika, wapate taarifa sahihi kuhusu lishe na athari za magonjwa zihusianazo na chakula husika.

Kwa upande wake serikali na wadau washirikiane kuhakikisha chakula kinabaki salama.

Akizungumzia siku hii yenye ujumbe kuwa usalama wa chakula ni jukumu la kila mtu, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa FAO, José Graziano da Silva anasema kwamba, awe mkulima, msambazaji, mchakataji au msafirishaji wa chakula, kila mtu ana jukumu kwa kuwa hakuna uhakika wa chakula bila usalama wa chakula.

Ni kwa mantiki hiyo WHO na FAO wanashirikiana kusaidia nchi kuzuia, kusimamia na kuchukua hatua za muda mrefu kwenye mnyororo mzima wa uzalishaji chakula ambapo wanashirikiana na wazalishaji, wauzaji, mamlaka za usimamizi, mashirika ya kiraia kuona usalama wa chakula, iwe kinaagizwa kutoka nje au kinazalishwa ndani ya nchi.

Kwa mujibu wa mashirika hayo, uwekezaji katika elimu ya mlaji kuhusu usalama wa chakula umesaidia kupunguza magonjwa yahusianayo na sumu au vijidudu kwenye chakula na hivyo kurejesha uwekezaji wa kila dola 10 iliyowekezwa.

Ukosefu wa chakula

Ikiwa leo ni siku ya chakula duniani na mwito ukiwa ni kutokomeza njaa na kuwa na dunia ambayo chakula chenye lishe bora kinapatikana kwa bei nafuu na kwa watu wote na kila mahali, Umoja wa Mataifa unahoji iweje leo hii zaidi ya watu milioni 820 hawana chakula cha kutosheleza mahitaji yao?

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hii anasema kuwa haikubaliki kwamba njaa inaongezeka wakati ambapo dunia inatupa takriban tani bilioni moja ya chakula kila mwaka.

Guterres anasema cha kustaajabisha ni kwamba katika dunia yenye utajiri, bado kuna mamilioni ya watu wanaolala njaa kila usiku. 

Hali imekuwa mbaya zaidi wakati wa sasa wa janga la ugonjwa wa virusi vya corona (Covid-19) ambalo limezidi kuongeza kiwango cha njaa na ukosefu wa chakula ambao haujawahi kushuhudiwa miongo kadhaa. 

“Takribani watu milioni 130 wako hatarini kutumbukia kwenye njaa mwishoni mwa mwaka huu hii ikiwa ni nyongeza ya watu wengine milioni 690 ambao tayari hawana mlo. Na wakati huo huo zaidi ya watu bilioni 3 hawawezi kumudu mlo wenye afya,”  

Kutokana na Covid-19, mizozo ya vita na hata mabadiliko ya tabianchi, mamilioni ya watu wanategemea msaada wa chakula ambapo Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) husambaza kwa njia mbalimbali ikiwemo kurusha angani, huku Shirika la Chakula na Kilimo Duniani linapatia wakazi wa dunia stadi bora za kilimo endelevu na cha kuhakikisha upatikanaji wa chakula. 

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu Guterres anasema, “Hatuna budi kuimarisha juhudi zetu za kufanikisha dira ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Hii ina maana kuwa na mustakabali ambamo kwao kila mtu, kokote pale aliko anapata lishe bora anayohitaji.

Tunahitaji kuhakikisha mifumo ya chakula ina mnepo dhidi ya hatari zozote na pia mabadiliko ya tabianchi. Tunahitaji kuhakikisha kila mtu anapata lishe bora na tupunguze utupaji wa chakula. Inahitajika mifumo ya chakula ambayo itaweza kupatia wafanyakazi mbinu za kujipatia kipato ambazo ni salama na zenye utu.” 

Anakumbusha kuwa dunia hivi sasa ina teknolojia na uwezo wa kuunda dunia endelevu zaidi, yenye usawa na mnepo kwa hiyo katika siku ya leo kila mtu aweke ahadi ya kukuza, kustawisha na kuendeleza kwa pamoja. 

Kama hiyo haitoshi, Guterres  anasema watu bilioni mbili, wanaume, wanawake na watoto wana uzito kupita kiasi au ni matipwatipwa na kwamba, “milo isiyo bora inazua hatari ya magonjwa na vifo.”

Katibu Mkuu huyo anasema, “ni wakati wa kubadilisha namna ambavyo tunazalisha, tunatumia ikiwemo kupunguza gesi chafuzi. Kubadilisha mifumo ya chakula ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.”

Kila mwaka Makao Makuu ya FAO huzitaka nchi wanachama kuhamasisha wadau wote wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuchangia katika kuhakikisha kila mtu anawezeshwa kupata chakula bora na cha kutosha wakati wote wa maisha yake.

Wizara ya Kilimo katika taarifa yake inasema kuwa hali ya uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya chakula nchini imeendelea kuwa nzuri katika kipindi cha miaka mitano mfululizo kufuatia uzalishaji wa ziada wa mazao ya chakula ambapo kwa msimu wa mwaka jana nchi imejitosheleza ikilinganishwa na mahitaji.

Katika kufanya tathmini ya hali ya chakula, hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na usalama wa chakula, wizara imekuwa inaangalia baadhi ya mazao muhimu yanayohitajika zaidi kama vile mahindi, mtama na ulezi, mchele, mikunde, ngano, ndizi, muhogo na viazi.

Katika kipindi hicho, nchi imekuwa na kiwango cha utoshelevu kati ya asilimia 120 hadi 125 na imekuwa ikizalisha ziada kati ya tani 2,582,717 hadi 3,322,689.

Mafanikio hayo yanatokana na sababu mbalimbali ikiwemo hali ya hewa nzuri, pamoja na usimamizi na utekelezaji mzuri wa sera na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na serikali pamoja na wadau wengine wa masuala ya kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji.

Wizara ya Kilimo ilifanya katika Tathmini ya Hali ya Uzalishaji wa Mazao ya Chakula kwa msimu wa 2018/2019 na Upatikanaji wa Chakula kwa mwaka 2019/2020 katika mikoa yote 26 Tanzania Bara kwa lengo la kubaini uzalishaji na mahitaji.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, uzalishaji wa mazao ya chakula yanayojumuisha mahindi, mpunga, mtama/uwele, mikunde, ngano, ndizi, muhogo na viazi kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 umefikia tani 18,196,733.

Jambo hili linaifanya Tanzania kuepuka baa la njaa ambapo FAO limesema takribani mataifa 41 yanaendelea yanahitaji msaada wa chakula kutoka nje, sababu kuu ikiwa ni mizozo na hali mbaya ya hewa.

FAO kupitia ripoti yake kuhusu matarajio ya mazao na hali ya chakula inasema kati ya nchi hizo 41, 31 ni kutoka Afrika.

Hata hivyo, uhaba wa mvua hasa kwenye maeneo ya nchi za Afrika Mashariki umechochea ukosefu wa chakula ikielezwa kuwa kwa ujumla uzalishaji wa nafaka kwenye ukanda umepungua kwa asilimia 5.6 kutoka kiwango cha mwaka jana.

Ripoti hiyo inasema anguko kubwa la uzalishaji wa nafaka linatarajiwa katika nchi za Kenya na Sudan huku bei za mazao kama vile mahindi na mtama zikiwa zimeongezeka kwa kiwango kikubwa na uhakika wa chakula ukipungua kwa kiasi kikubwa Kenya na Somalia.

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi