loader
Dstv Habarileo  Mobile
UMITASHUMTA NA UMISSETA  Viwanda vya ajira na kukuza uchumi

UMITASHUMTA NA UMISSETA Viwanda vya ajira na kukuza uchumi

APRILI 22, 2021 wakati akilihutubia Bunge, Rais Samia Suluhu Hassan alisema sekta za sanaa, utamaduni na michezo zinakua kwa kasi kubwa na zinatoa fursa ya ajira kwa vijana, hivyo Serikali yake imedhamiria kuziboresha.

 “Vijana wetu wengi wamepata ajira kupitia sekta hizi, hivyo basi kama ilivyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwenye miaka hii mitano, tunakusudia kukuza zaidi sekta hizi hususani kwa kuimarisha usimamizi wa masuala ya hakimiliki ili wasanii na wanamichezo waweze kunufaika na kazi zao,” anasema Rais Samia.

Anasema serikali itaanzisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, ili kuwasidia wasanii nchini kupata mafunzo na mikopo itakayosaidia kukuza uchumi wao na taifa kwa jumla.

Kwa mujibu wa Samia, Serikali imeanza kutenga fedha kidogo kidogo kwa ajili ya timu za taifa zikiwemo za wanawake ili kuhakikisha sekta hiyo inapata msukumo na ari za wachezaji hali itakayoiwezesha Tanzania kuingia kwenye ramani ya michezo duniani ukiwamo wa soka na hivyo, taifa kunufaiki kijamii na kiuchumi.

Akimwapisha Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul, Rais Samia alisema amemteua ili akasimamie na kuendeleza michezo hususani timu za wanawake ili nazo zitumike kuibua na kuboresha vipaji na pia, kutengeneza ajira kwa vijana na kushiriki kuchangia ukuaji wa uchumi na kuongezea pato la taifa.

Kimsingi, michezo ni ajira kwa vijana na michezo ni biashara kwa kuwa katika michezo, watu na taasisi huendesha biashara mbalimbali ikiwamo ya mavazi, chakula, vinywaji na hata kiingilio vitu ambavyo huchingia pato la taifa kupitia kodi.

Hata wanaosafiri kwenda kucheza au kutazama na kuashangilia michezo, hulipa nauli na wengine kununua nishati ya mafuta inayotumika katika vyombo vya usafiri. 

Kwa mtazamo huo mpana wa kiuchumi, mashindano haya ya Umitashumta na Umisseta hayana budi kupewa kipaumbele kwa kuwa ni kiwanda cha ajira, biashara na huchangia kukua kwa uchumi wa watu na taifa kwa jumla.

Kimsingi, serikali imeamua kuzipa sekta hizi kipaumbele kupitia mashindano baada ya kubaini zaidi umuhimu wake katika kujenga afya za washiriki, kujenga na kuimarisha urafiki kiongoni mwa jamii, kuibua vipaji vya vijana na kuchangia ukuaji wa uchumi ili michezo itumike kama moja ya nyenzo za kujengea uchumi wa nchi.

Kutokana na kipaumbele hicho cha Mkuu wa Nchi katika michezo, wasaidizi wake nao akiwamo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wamepata ari na kasi mpya kwa kutoa maelekezo madhubuti mintarafu kuendeleza sekta ya michezo ambayo ni moja ya chemichemi za kuichumi.

Aprili 13, 2021 wakati akiwasilisha Hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 bungeni Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa aliitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuandaa mkakati wa kuendeleza wataalamu wa michezo, sanaa na burudani nchini. 

Hata Mei 21,2021 wakati akizindua Kongamano la Kuenzi Mchango wa Tanzania katika Ukombozi wa Afrika  lililofanyika Dar es Salaam, Majaliwa aliielekeza  Wizara ya Habari, Wizara ya Utumishi na TAMISEMI (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) kukaa na kutatua changamoto za kimuundo katika sekta za utamaduni na michezo.

Kuhusu maagizo hayo, hivi karibnuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Abbasi amesema: "Tayari kikao hiki kimejadili na kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu aliyotoa Mei 21,2021 ikiwemo la kufanya marekebisho ya muundo wa kada za maofisa utamaduni na michezo, na kwa kushirikiana na Tamisemi na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, tumemaliza."

Kimsingi, Majaliwa ni mwanamichezo aliyetoa mchango mkubwa katika taifa hili. Wakati Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hii Aprili 31, mwaka huu, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema wizara hiyo haina budi kutumia uzoefu mkubwa wa Waziri Mkuu Majaliwa kuboresha sekta ya michezo nchini.

Hapa ni wazi kuwa, Serikali ya Awamu wa Sita chini ya Rais Samia imejipanga kimkakati kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya michezo nchini.

Maboresho makubwa katika mashindano ya Umitashumta na Umisseta ya mwaka huu kwa kushirikisha wizara mbalimbali yanaleta matumaini makubwa kwamba, sekta ya michezo itaibua na kunoa vipaji vingi vitakavyoinua sekta hii kimataifa na kuchangia vilivyo kukua kwa uchumi wa Watanzania.

Ndio maana leo Juni 8, 2021 Waziri Mkuu, Majaliwa anafungua mashindano haya ya Umitashumta na Umisseta katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona hapa mjini Mtwara. 

Haya ni mashindano ya kwanza kwenye historia ya Tanzania yakiwa yameboreshwa kwa kiwango cha juu na kuratibiwa na wizara tatu tofauti na miaka yote tangia kuanzishwa.

Akiwasilisha hotuba ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo bungeni hivi karibuni, Waziri Bashungwa, anasema Serikali imeratibu mashindano hayo kwa kuzishirisha wizara tatu zinazohusika yaani, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na MichezoWizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Tamisemi.

Bashungwa anasema huu ni mkakati wa serikali kuboresha na kukuza sekta ya michezo ili kuibua vipaji, kuongeza ajira na hatimaye sekta ya michezo kuchangia ipasavyo kukuza uchumi wa nchi maana michezo ni uchumi na michezo ni afya.

Makatibu wakuu wa wizara hizo wametoa taarifa kwa umma mintarafu serikali ilivyojipanga kuhakikisha mashindano ya mwaka huu yanafanyika katika ubora wa kiwango cha juu tofauti na awali.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema, mashindano ya Umitashumta na Umisseta yanayofunguliwa leo na Waziri Mkuu Majaliwa na yatafungwa Julai 3, mwaka huu.

Mashindano hayo yatafanyika katika viwanja vya Nangwanda Sijaona, Chuo cha Walimu Mtwara, Chuo cha Ufundi Mtwara na katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Mtwara.

Profesa Shemdoe anasema umuhimu wa Umitashumta na Umisseta  ni pamoja  kuvumbua vipaji na kisha kuweka mikakati endelevu ya kuviendeleza ili kupata wachezaji wa timu za taifa kwa michezo mbalimbali pia wataalamu wa michezo ambao watatokana na misingi imara ya taaluma ya michezo.

Mwenyekiti Mweza wa Kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi, anasema mashindano hayo yameboreshwa ili kuhama kutoka tukio la kawaida la michezo shulen hadi kuwa tukio kubwa la kimichezo la kitaifa na kuwa kitovu cha mawakala wa vipaji kusaka nyota wa michezo mbalimbali.

Abbasi anasema: "Tumejipanga, tutaendelea kuboresha michezo hii ili iwe kitovu cha kuandaa, kukuza na kuuza vipaji vya vijana wetu duniani." 

Anasema serikali imejipanga kusaidia kuwaendeleza wanamichezo watakaofanya vizuri ili kuwanoa kwenye taaluma ya michezo kupitia vyuo vya michezo nchini.

Dk Abbasi anasema serikali inatekeleza mradi wa kupanua na kuboresha Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya ikiwa ni mkakati maalum wa kuanzisha kituo cha kimataifa cha kuendeleza vipaji vya michezo nchini kinachoweza kutumika kuivisha vipaji kutokana na mashindano haya.

Anaongeza kuwa, serikali inaweka mazingira wezeshi kwa taasisi na watu binafsi ndani na nje ya nchi kuwekeza katika kuendeleza vituo vya kuvumbua na kuendeleza vipaji nchini.

Kwa mujibu wa uchunguzi, tayari serikali imeanza mazungumzo na balozi mbalimbali kama za Brazil, Uturuki, Cuba na Misri na zote zimeonesha nia ya kuwekeza  katika eneo hili.

Dk Abbasi anasema: “Ni matumaini ya Serikali kuwa jitihada zote hizi zitazaa matunda ya kuwa na wachezaji wengi katika michezo mbalimbali na hivyo, kuwa washindani wakubwa katika mashindano makubwa ya kimataifa kama Olympic, All Africa Games na Jumuiya ya Madola.”

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk James Mdoe, anasema wizara hizi sasa zinafanya kazi kwa kushirikiana.

Anasema wizara hizo zimekuja na mkakati wa kutenga shule mbili katika kila mkoa zitakazofundisha Somo la Michezo katika ngazi ya kidato cha tano na zitatumika kama vitalu vya kukuza na kuendeleza vipaji vitakavyo vumbuliwa. 

Anafahamisha kuwa, vyama vya michezo vya kitaifa vimealikwa ili kutambua vipaji vya wanamichezo na vitashiriki kwa namna mbalimbali kuendeleza vipaji hivyo kupitia fursa mbalimbali.

Mdoe anasema: "Serikali imekwishaelekeza kuendelea na uimarishaji wa ufundishaji wa michezo shuleni sambamba na kuendeleza na kuimarisha mashindano ya Umitashumta na Umisseta katika ngazi zote ikiwemo hii ya Taifa." 

 

Mwandishi wa makala haya  aliyepo Mtwara kwa sasa, ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Anapatikana kwenye  HYPERLINK "mailto:jmapepele1@gmail.com" jmapepele1@gmail.com  na 0784441180

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/3b191b811e9fcd4d4720dd7fe21b4334.jpeg

Mteja anayetaka kutuma mzigo nje au kupitishia ...

foto
Mwandishi: John Mapepele

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi