loader
Wanasiasa bado wanademka kwa ngoma ya mitandaoni

Wanasiasa bado wanademka kwa ngoma ya mitandaoni

WAHENGA wanasema panapofuka moshi panaficha moto; ukimuona zinduna ambari yupo nyuma; lisemwalo lipo, na kama halipo laja.

Pia wanasema, si kila madai ni ya kweli; pia si kila kanusho ni la kweli. Unaweza kushutumiwa kuwa unazo, lakini ukawa huna. Lakini pia unaweza ukakanusha kwamba sina kumbe unazo tena nyingi tu.

Kwa nyakati tofauti Oscar Kambona alishika nafasi tofauti za uongozi ndani ya serikali na chama cha TANU. Maandiko kadha wa kadha yanaonesha kwamba alishindwana na Mwalimu Nyerere baada ya kuanzishwa kwa Azimio la Arusha pengine hata kabla. Tofauti zao zilisababisha Kambona kukimbilia Kenya kisha Uingereza.

Maandiko yanaonesha kwamba baada ya Kambona kuikimbia nchi jina lake lilichafuliwa sana. Uchafuzi huo ulikuwa kila mahali. Jeshini, mashuleni na kila mahali. Kila mtu alimuona kama mtu mbaya sana kwa taifa la Tanzania. Swali kwamba yaliyosemwa juu yake yalikuwa na ukweli ama la ni ngumu kuthibitisha kwa sasa, japo inawezekana moja kati ya kweli au si kweli lilikuwa sahihi.

Mnamo tarehe 23 Januari, 1968, Kawawa alilitaarifu Bunge kwamba; “Wote mnajua kwamba Kambona alikimbia nchi mwaka jana, 1967. Kabla hajaondoka, tarehe 6 Desemba, 1966, Sh 500,000 ziliingizwa kwenye akaunti yake kutoka benki moja ya Uingereza.

“Uchunguzi wa BoT (Benki Kuu ya Tanzania) kutoka Kambona atoroke umeonesha kuwa tangu Juni 1965 na Desemba 1966, Kambona aliingiza katika akaunti yake jijini Dar es Salaam Sh 896,800." Kambona pia alikuwa anamiliki majumba mengi.

Baada ya kuchafuliwa jina, Kambona aliitisha vyombo vya habari akiwa Uingereza na kufahamisha umma kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa na fedha nyingi kwenye akaunti huko Uswizi. Na aliahidi kurejea Tanzania na kuzitaja akaunti hizo. Pia katika hili ni ngumu kuthibitisha kama ni kweli ama la; ni ngumu kuthibitisha kwasababu hata Kambona hakuthibitisha hilo hata aliporejea nchini!

Wakati anatoroka Tanzania alikuwa anaongoza kitengo cha usalama wa taifa lakini kilikuwa ni kitengo kinachofuata taratibu za nchi za magharibi kwa kuwa wakati huo tulikuwa tunafuata siasa za kibepari tulizorithi kutoka kwa waingereza ambao walikuwa wanatawala nchi.

Kuondoka kwake pia kulitokana na uamuzi wa Mwalimu Nyerere kufuata siasa za kikomunisti. Alipoondoka Nyerere alibadilisha mfumo mzima wa kitengo hicho.

Ndugu msomaji wa makala haya wote tutakumbuka kwamba tarehe 17 machi, 2021, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli, aliitwa na muumba wake na hivyo kutangulia mbele ya haki. Kufuatia kifo chake wananchi wengi walilia sana.

Maombolezo yalikuwa mengi mno, kila kona ya nchi majonzi yalioneshwa wazi pasipo kificho. Wakati hali ikiwa hivyo kuna baadhi ya watu walikuwa wanafurahia kifo hicho. Mitandao ya kijamii ilitumika vibaya katika kipindi hicho hasa na baadhi ya vikundi vya watu wenye nia ovu na nchi yetu.

Pamoja na kwamba wengine tulikuwa tunaomboleza kifo hicho, baadhi walikuwa wanabeza hali hiyo. Mitandao ikatumika kufanikisha hilo.

Tunashukuru Mungu hilo nalo lilipita. Tulivuka salama kwa ushupavu wa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muunganoo wa Tanzania.

Kama ilivyo kawaida kila zama za utawala na mambo yake. Baada ya Magufuli kufariki dunia baadhi ya watu walianza kulinganisha tawala hizi mbili yaani ya Samia na hayati. Pasipo Rais Samia kutokea na kukomesha jambo hilo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ingeendelea kukuza jambo hilo ambalo halina afya kwa mustakabali wa taifa letu.

Kama ilivyo kawaida kwa nyakati tofauti mitandao ya kijamii imekuwa ikitumiwa vibaya hasa kuwachafua watu fulani fulani kwa maslahi yao lengwa. Bahati mbaya baadhi yetu badala ya kuyafikiria kwa kina yale yanayojadiliwa kwa mitandao hiyo, tunaishia kuyavalia njuga hata kama hatujajua ukweli kwa kina.

Mitandao hii imegeuzwa kuwa mshtaki, msikiliza kesi na mtoa hukumu kwa watu lengwa pasipo kujali maisha ya mlengwa ya baadae.

Bahati mbaya wakati mwingine hata vyombo vyetu vya mamlaka vimekuwa vikifanya kazi kwa kufuatisha matakwa ya mitandao hii. Swali ni tunapofanya hivyo ni kwa maslahi ya nani? Na je, wanaotumia vibaya mitandao hii wanalenga kumfurahisha nani?

Kwenye siasa jambo la kutengeneza propaganda (framing) za kumchafua au kumsafisha mtu ni jambo la kawaida. Lakini kila linapofanyika linakuwa na malengo mapana ambayo mwanzilishi wake ndiye aujuaye mwisho wake.

Ni wazi kwamba utawala wa Magufuli haukupendwa sana na upinzani kwa sababu kadha wa kadha. Kwa nyakati tofauti baadhi ya wateule wake walitumia teuzi hizo kufanya yaliyotakiwa kufanyika aidha kwa nafsi zao au kwa vingine.

Kazi ya kuuondoa upinzani kwenye maeneo sugu haikuwa kazi nyepesi na wakati mwingine kuna baadhi ya njia ilizotumika hazikuwa sahihi lakini kunahitajika staha katika kila jambo. Swali la kujiuliza ni je, ni nani alinufaika kwa haya yote? Ni, nani wa kulaumiwa kwa hayo yote? Je, inawezekana kesi zao ni za kutengeneza? Na je. Ni kwa kumnufaisha nani?

Hofu ni iwapo tukianza kuendeshwa na mitandao ya kijamii utafika wakati Watanzania wengi watapotezwa kwa njia hii ya kufuata propaganda hizi za kimtandao. Na pindi zikituendesha upinzani utazidi kuzitumia kwa manufaa yao wenyewe. Hili, likitokea, nani wa kupoteza?

Kuna wakati Bunge letu lilianza kuendeshwa na mitandao ya kijamii, kama alivyosema Rais, wabunge walidemka sana kwa ngoma inayopigwa mitandaoni. Kauli ya Rais ilitosha kurejesha Bunge kwenye mstari. Swali ni je, kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii kwa sasa ni nani atakayekomesha ili wananchi wa kawaida wasiendelee kudemka? Kuna umuhimu mkubwa kama taifa kuangalia upya matumizi ya mitandao hii hasa inapotumika vibaya.

Najua kuna sheria ya makosa ya kwenye mitandao pengine ni wakati wa kuona meno ya sheria hiyo ing'ate ipasavyo sasa.

Waliopata taabu kwa sababu ya ‘framing’ ya mitandao hii ndiyo wanaoipata joto ya jiwe. Inawezekana wengine tunashangilia yanayotokea lakini ikumbukwe kwamba mabepari hutumia mijadala ya kwenye mitandao hiyo hiyo kufanya uamuzi wa kisiasa juu ya nchi zetu maskini.

Wakati mwingine propaganda hizi huzianzisha wao wenyewe kupitia watu wao waliowapandikiza kwenye nchi zetu kwa maslahi yao. Tunahitaji kujipanga upya kwa maslahi ya kitaifa hasa linapokuja suala la ‘fraiming’ na Mungu atusaidie.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili.

 

Mawasiliano yake ni +255 712 246 001; flugeiyamu@gmail.com

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/1c74b2f476a1d04feafbdb70e7dc4ace.png

NIPO nyumbani kwa Baba na Mama Chichi. ...

foto
Mwandishi: Felix Lugeiyamu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi