loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ni faraja serikali kujali  miradi ya maendeleo

Ni faraja serikali kujali miradi ya maendeleo

WATANZANIA wamepata faraja kubwa kutokana na uwekezaji mkubwa wa fedha uliofanywa na serikali katika mwaka wa fedha 2021/22, kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambapo Sh bilioni 13,326 zinatarajiwa kutumika ili kugharamia miradi  hiyo sawa na asilimia 37 ya bajeti yote ya serikali.

Jambo hili ni faraja kwa wananchi ambao walikuwa na wasiwasi kuhusu utekelezwaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, lakini sasa wamepata uhakika kuwa hakuna kitakachoachwa na  Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alitoa hakikisho hilo wakati alipokuwa akisoma Bajeti ya Serikali jana jijini Dodoma, ambapo alisema kati ya kiasi hicho, Sh bilioni 6,180.0 ni mapato ya ndani, Sh bilioni 4.190 ni mikopo ya ndani na nje yenye masharti ya kibiashara na Sh bilioni 2.955 ni misaada na mikopo nafuu kutoka nje.

Kwa mantiki hiyo, serikali imewahakikishia wananchi kuwa itaendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya maendeleo kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi na taifa kwa ujumla, ikiwamo kuimarisha biashara ndogo na kubwa miongoni mwa wananchi.

Baadhi ya miradi mikubwa ambayo Watanzania wengi wanaitegemea kunufaisha maisha yao ni pamoja na mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Mwalimu Nyerere ambao unategemewa kumaliza changamoto ya umeme vijijini.

Pia mradi huu unategemewa kupunguza gharama za umeme kutoka bei ya sasa na kuwa ya chini zaidi kwani bei ya sasa inalalamikiwa na watumiaji kuwa ni ya juu sana.

Kwa mujibu wa Dk Mwagulu, sehemu kubwa ya bajeti ya maendeleo itatumika kugharamia utekelezaji wa miradi ambayo ni kielelezo cha uhai wa nchi ambapo, miradi mingine ya maendeleo, itaendelea kugharamiwa kupitia utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), pamoja na utaratibu wa kampuni maalumu.

Jambo jingine la kutia moyo ni kuona serikali inaweka utaratibu wa kuwezesha ukusanyaji wa mapato ili kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha ambazo ndizo zinazotumika katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.

Katika hili, Dk Mwigulu alisema serikali itaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kwa kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji ili kukuza biashara ndogo na za kati kwa ukuaji endelevu wa uchumi utakaowezesha kupanuka kwa wigo wa kodi.

Miradi mingine ambayo inaguswa katika bajeti hiyo ni pamoja na miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro mpaka Dodoma.

Utekelezaji wa miradi hiyo kwa hakika ni hatua kubwa ambayo inahitaji serikali kupongezwa kwa kuweka fedha nyingi ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inasimama na kuwa na manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla kwa kuwa ndio uti wa mgongo wa uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla.

Sote tuna amini kuwa, kwa kuwa Tanzania iliingia katika uchumi wa kipato cha kati kabla ya miradi hiyo ya kimkakati kukamilika, taifa hili litapiga hatua nyingine kubwa kiuchumi baada ya kukamilika kwa miradi hiyo itakayokuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji uchumi.

Hiyo inasababishwa na ukweli kuwa, miradi ya maendeleo ndio kichocheo cha ukuaji wa biashara, uwekezaji, ukuaji wa sekta ya afya pamoja na ukuaji wa sekta ya utalii kwa kuongezeka idadi ya watalii wanaoingia nchini.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/7d369a10bb32163e9437baf162b5c236.jpg

LEO katika mwendelezo wa makala za ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi