loader
Dstv Habarileo  Mobile
Uwekezaji wa kilimo wa Jatu wawavutia vijana wengi

Uwekezaji wa kilimo wa Jatu wawavutia vijana wengi

“JEMBE halimtupi mkulima” ni miongoni mwa misemo kati ya mingi iliyozoeleka katika jamii ya Watanzania ikilenga kuhamasisha, kuonya au kutoa elimu katika masuala mbalimbali kwa lengo la kuifanya jamii husika kuchukua hatua muhimu ya kujiletea mabadiliko kulingana na usemi husika.

Taasisi ya Jenga Afya Tokomeza Umasikini (Jatu) ni moja ya taasisi zilizoamua kusimama na kuonesha kwa vitendo dhana halisi ya msemo wa “Jembe halimtupi Mkulima” kwa kuamua kufanya uwekezaji katika kilimo kwa kuwahusisha wananchi kutoka matabaka yote wakiwemo wafanyakazi na wafanyabiashara kuwekeza katika kilimo hicho.

Hata hivyo pamoja na serikali kuwahimiza wananchi wake kufanya shughuli za kilimo, kwa kiasi kikubwa bado wananchi wengi wamekuwa wakisuasua kufanya shughuli hiyo na pengine ni kutokana na kutokuwepo kwa mazingira ya kuvutia ya kuwawezesha wananchi kulima hususani suala la upatikanaji wa pembejeo za kisasa kurahisisha kilimo hicho.

Kilimo ambacho katika taifa kinatajwa kuwa ni “Uti wa mgongo” katika kukuza uchumi, kinahusisha alisimia kubwa ya Watanzania, wengi wao wakifanya kilimo kwa ajili ya mahitaji ya chakula na asilimia ndogo wakifanya kilimo hicho kwa ajili ya biashara.

Kilimo cha biashara kinafanywa na watu binafsi, kampuni mbalimbali na taasisi zilizojipambanua kwa ajili hiyo ikiwemo Jatu iliyofanya uwekezaji ya kilimo cha mazao mbalimbali kwa ajili ya biashara.

Jatu imewekeza katika mikoa mbalimbali nchini, taasisi hiyo iliyorodheshwa pia katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), malengo yake kwa kipindi cha mwaka huu ni kukusanya kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 7.5 zitakazoisaidia kuongeza tija katika kilimo ikiwemo ununuzi wa zana mbalimbali kama matrekta ili kufanikisha malengo yake.

Taasisi hiyo yenye wanachama 30,000 na wateja wanaokadiriwa kufikia 70,000 nchi nzima kwa sasa, wengi wao wakiwa vijana walioajiriwa na kujiajiri katika taasisi mbalimbali, imewekeza kwenye mashamba yenye ukubwa wa zaidi ya hekari 17,678 katika mikoa ya Manyara, Morogoro, Tanga, Ruvuma, Singida na Njombe.

Inaendesha kilimo cha mazao ya mahindi, mpunga, alizeti, maharage, machungwa, parachichi, lakini pia mboga mboga na matunda.

Kupitia mashamba hayo, wamekuwa wakizalisha takribani tani 8,670 za nafaka ambazo huchakatwa katika viwanda vidogo vidogo walivyoanzisha katika maeneo ya Mbingu Morogoro na Kibaigwa mkoani Dodoma, hatimaye kuuzwa kupitia maduka makubwa ‘Supermarkets’ yakiwemo baadhi yanayomilikiwa na taasisi hiyo katika mikoa ya Arusha, Mtwara, Mwanza, Dar es salaam na Dodoma.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Jatu na mwanzilishi wa taasisi hiyo Peter Gasaya, matarajio yao ni kuendelea kuongeza ubunifu zaidi katika kilimo na miradi itakayowawezesha kuwa na viwanda vingi vya kuzalisha bidhaa ambazo wataziuza kupitia mifumo na kukifanya kilimo hicho kuwa cha kisasa kwa kutumia wataalamu mbalimbali na zana za kisasa zitakazowasaidia kuongeza mavuno.

Akizungumza wakati wa mkutano na wanahisa wa taasisi hiyo mwishoni wa wiki, Gasaya anasema matumaini ya pamoja ya uongozi wa taasisi hiyo na wanachama wake ni kuona wanafikia malengo waliyoyakusudia ya kuondokana na umasikini kupitia kilimo kutokana na umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi.

Anasema kwa sasa hapa nchini wapo baadhi ya watu, makundi ambayo kwa kutambua umuhimu wa kilimo yamekuwa yakitumia mbinu mbalimbali ili kufikia malengo yao na hivyo kujikwamua kutoka katika umasikini ikiwemo taasisi hiyo ya Jatu ambayo baada ya kufanya uwekezaji katika mashamba imeongea hatua zaidi kwa kuwashirikisha wananchi wote kupitia mfumo wa uuzaji wa hisa.

“Ili kuwashirikisha Watanzania wengi katika uwekezaji wetu huu katika kilimo kupitia hisa, tumezindua mpango ujulikano ‘Buku 5 inatosha’ ambao lengo lake ni kumuwezesha kila Mtanzania kuwa mmiliki wa kampuni hii angalau kwa kununua hisa kumi; malengo yetu ni kumfanya kila Mtanzania kuwa sehemu ya Jatu ili kwa pamoja tuweze kujikomboa kutoka katika umasikini,” anasema Gasaya.

Anasema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2017 ikiwa na wanachama 12 imeendelea kujipatia mafanikio ambayo anatamani yaiwe kwa Watanzania wachache bali wengi kwa kuwa mbali na kusaidia kuijenga taasisi hiyo pia kutalisaidia taifa kuzidi kupiga hatua kiuchumi na kupunguza tatizo la ajira.

 

Anasema tangu kuorodheswa katika soko la hisa, Jatu imekuwa kimbilio la watu waliopo maofisini, katika biashara mbalimbali ambao wameona vyema kutumia fursa ya uwepo wa taasisi hiyo kwa kuamua kuwekeza kwa kununua hisa na kuwa sehemu ya wakulima wengi nchini.

“Tumeamua kuwa na mfumo huu ili kuwafikia vijana wengi kwa kuwahusisha na kilimo, vijana wengi wapo mijini jambo linalowapa ugumu hususani kwa kwenda mashambani moja kwa moja na kulima ila kwa kupitia taasisi hii tumeweza kuwafanya nao kuwa wakulima na wawekezaji kwa wakati mmoja” anasema Gasaya.

Aidha anasema kupitia utaratibu uliopo katika taasisi hiyo, wameweka njia nzuri za kumuwezesha kila mkulima kumiliki ardhi na kuwa na matumizi bora ya ardhi hiyo wakizingatia utunzaji wa mazingira wakiwa na lengo hilo hilo la kumuhakikishia analima kwa tija ili kumsaidia kupambana na umasikini.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/5ab37005343fcf94fd5233d9f97685a3.jpg

Mteja anayetaka kutuma mzigo nje au kupitishia ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi