loader
Dstv Habarileo  Mobile
TMDA wataweza kusaidia kupunguza matumizi ya tumbaku?

TMDA wataweza kusaidia kupunguza matumizi ya tumbaku?

SIGARA ina kemikali zaidi ya 4,000 ambazo zina uwezo wa kudhuru afya ya binadamu; zaidi ya kemikali 40 katika tumbaku zimethibitishwa kusababisha saratani na takriban watu milioni nane hufariki kila mwaka duniani; zaidi ya watu milioni saba vifo vyao ni matokeo ya matumizi ya moja kwa moja wakati takribani milioni 1.2 ni matokeo ya uvutaji usio wa moja kwa moja.

Takwimu hizo ni matokeo ya utafiti mbalimbali uliofanyika duniani na taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu moja ya bidhaa ya tumbaku inayopendwa sana duniani, sigara.

Tunapozungumza bidhaa za tumbaku maana yake ipo sigara wengine wanaiita sigareti, majani, siga pamoja na bidhaa nyingine za aina hiyo zinazotengezwa kwa kutumia tumbaku au mbadala wake zinazovutwa au kutafunwa.

Inapaswa ikumbukwe kwamba tumbaku ipo duniani kwa zaidi ya miaka elfu nane na kwamba watu wa zamani wa Mexico ndio walikuwa wa kwanza kutumia tumbaku kama sehemu ya kujistarehesha, kwani hakuna faida ya msingi katika mwili wa binadamu zaidi ya kujistarehesha tu. Lakini pamoja na ukweli huo sigara imeanza kupigwa vita siku za karibuni kutokana na kuongezeka kwa madhara yake.

Katika utafiti mwingi umebaini kuwa matumizi ya tumbaku yamekuwa yakihusishwa na madhara mbalimbali katika mwili wa binadamu pamoja na kuwa matumizi yake yamekuwepo kwa muda mrefu.

Kuna zaidi ya aina 70 ya tumbaku lakini inayojulikana vyema ni ile inayolimwa kibiashara ya N. tabacum ingawa pia kuna aina nyingine ya tumbaku N. rustica inayotumika kwa watu wengine ingawa si kwa wengi.

Tumbaku iliyokaushwa mara nyingi hutumika kwa ajili ya kuvuta katika mfumo wa sigareti, cigars, viko na shisha. Pia tumbaku inaweza kutumika kwa kunusa na kutafuna.

Kwenye tumbaku kuna uraibu wa alkaloid na harmala alkaloids. Tumbaku kwa mujibu wa WHO husababisha vifo na magonjwa ambayo yanaweza kuzuilika.

Inaaminika kwamba tumbaku ilianza kutumika katika bara la Amerika nchini Mexico miaka ya 1400–1000 BCE na ilikuwa inatumika katika sherehe na pia ilikuwa inatumika katika masuala ya kidini pia.

Kama ilivyo mambo yote ya starehe yanavyoleta kero katika dunia ya sasa, utumiaji ambao unaweza kusema wa holela umeanza kuleta athari na kulazimisha nchi kadhaa duniani kuanza kudhibiti matumizi yake kwa kutunga sheria na pia kuunda mamlaka za kufuatilia shughuli hiyo.

Nchini Tanzania zipo Sheria, Kanuni na Miongozo kadha inayohusu tumbaku. Sheria hizo ni Sheria ya Sekta ya Tumbaku, 2001; Kanuni za Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku, 2003; Kanuni za Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku za 2014 na Ilani ya Uteuzi wa Mamlaka ya Kudhibiti Bidhaa za Tumbaku (Kanuni) (Uteuzi wa Wakaguzi), 2021. Na watu waliopewa mamlaka hayo ni Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Kanuni za Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku ya mwaka 2003 zimempa waziri mwenye dhamana ya afya kuchagua wakala mwenye jukumu la kusimamia udhibiti kuhusu utengenezaji, uwekaji lebo, usambazaji uuzaji, utumiaji pamoja na matangazo ya bidhaa za tumbaku kwa lengo la kupunguza matumizi yake pamoja na madhara yake.

"Kifungu cha 18, kimempa Waziri wa Afya mamlaka ya kuteua mtu au chombo kuwa Mkaguzi kwa madhumuni ya utekelezaji wa Sheria ambapo mamlaka ya mtu au chombo kilichoteuliwa chini ya kifungu cha 19 kinakuwa na mamlaka ya kuingia mahali ambapo biashara ya bidhaa za tumbaku hufanyika.

“Kwa mfano, inapotengenezwa, kuhifadhiwa, kufungashwa au kuuzwa; kuchukua kitu chochote kinachoaminiwa kwa sababu za msingi kutumiwa au kusababisha kosa chini ya sheria hiyo," anasema Kaimu Mkurugenzi Udhibiti wa Dawa na Vifaa Tiba wa TDMA, Dk Yonah Mwalwisi wakati akizungumza na wahariri katika kikao kazi kilichofanyika Arusha hivi karibuni.

Anasema lengo kubwa la mamlaka yao kupewa jukumu hilo pamoja na sheria kutungwa mwaka 2003 ili kukabiliana na uraibu ambao kati ya watu 10 wanaovuta kwa sasa saba walianza kuvuta wakiwa wadogo. Nia kubwa kwa sasa ni kulinda watu chini ya miaka 18 na wengine wasio wavutaji sigara kutoka kwa ushawishi wa kuvuta na kulinda wasio wavutaji sigara dhidi ya moshi wa tumbaku.

Kwa kuwa inatambulika pasi shaka kwamba saba kati ya wavutaji sigara 10, huanza uraibu huu wakiwa wangali watoto, huku wanaoendelea kuvuta sigara kwa muda mrefu hufupisha maisha yao kwa miaka 20 hadi 25, TDMA wameanza kujipanga katika mnyororo wa udhibiti kwa kuangalia madhara ya kiafya kwa kuweka udhibiti unaostahili katika bidhaa hizi na hasa matangazo.

Ingawa madhara ya matumizi ya bidhaa za tumbaku yanajulikana ikiwamo kung’oka kwa nywele, macho, ngozi, masikio, meno, kuharibu mapafu na upumuaji, kuleta saratani za mapafu, pua, ulimi, tumbo, figo na zinginezo huku kutu ya sigara ikikusanyika na kuganda kwenye kucha na vidole vya mvutaji na hukauka na kuwa ngumu sababu ya joto na kemikali za sigara, matumizi ya tumbaku hayawezi kumalizwa kwa kukata uwapo wake bali watu kutambua madhara na kujiweka kando nayo.

Katika mafunzo hayo kwa wahariri ilielezwa kuwa kuna madhara makubwa kwa wake na wanaume kwa utumiaji wa sigara pamoja na ukweli kuwa biashara hii ilikuwapo duniani zaidi ya miaka 8000 iliyopita.

Kwa wanawake matumizi ya tumbaku huongeza hatari ya kupata saratani ya mfuko wa uzazi kushika ujauzito na mimba kuharibika, kuzaa mtoto aliyekufa au aliye na uzito usio wa kawaida; sigara pia inaweza kumfanya mwanamke kuwa tasa.

Madhara ya matumizi ya bidhaa za tumbaku kwa wanaume na watoto ni pamoja na kupunguza nguvu za kiume kwani uathiri mzunguko wa damu; pia huharibu mbegu za wanaume na kwa hiyo watoto wanaowazaa kuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kupata magonjwa ya saratani; na sigara pia huwafanya wanaume kuwa tasa.

Aidha madhara zaidi ya nusu ya vifo vya watoto wachanga vinahusishwa na uvutaji wa sigara wa wazazi kwani moshi wa tumbaku huharibu viungo vyote vya mwili mchanga; huingia kwenye njia ya upumuaji na kuongeza uzalishaji wa kamasi ambayo inasababisha kuziba na kukohoa na pia mwili unakuwa dhaifu na uwezekano wa magonjwa ya kupumua huongezeka.

Pia huleta hupata shida ya neva na kupata magonjwa ya ENT, kwa mfano, rhinitis tonsillitis; na ukuaji wa akili na mwili hupungua;

TDMA wana kazi kubwa ya kushawishi wananchi wasiendelee kuingiza hewa chafu kwenye mapafu kwa kuhakikisha kuwa umma unaelimishwa vya kutosha juu ya hatari ya kutumia bidhaa za tumbaku na moshi wa sigara na kuangalia faida zilizopo za kuacha kuvuta sigara.

Katika udhibiti inatarajiwa kwamba TDMA itahakikisha kuwa bidhaa za tumbaku zimebadilishwa ili kupunguza madhara kwa kiwango kinachoweza kiteknolojia na kivitendo; na kukuza mazingira ambayo yataondoa kabisa uvutaji wa sigara katika nyanja zote za maisha.

Baada ya tangazo la serikali, TDMA imepewa kazi ya udhibiti wa bidhaa za tumbaku na katika hili mamlaka hiyo imeanza kufanya hatua za utekelezaji ambapo ni kuunda Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Uthibiti wa Bidhaa za Tumbaku na kuwataka wafanyabiashara wa bidhaa za tumbaku kuwasilisha taarifa za bidhaa zao ili zitambuliwe na TMDA.

“Wadau watapewa muda maalumu wa kufuata maelekezo na tunawataka wadau wanaofanya biashara ya utengenezaji, kufungasha; usambazaji, uuzaji na matumizi au matangazo ya bidhaa za tumbaku kutoa taarifa na kuanza kutoa vibali vya kuagiza na kusafirisha nje; kuanza kufanya tathmini na idhini ya uuzaji wa bidhaa mpya zilizoletwa sokoni,” anasema Dk Yonah Mwalwisi.

Miongoni mwa kazi ambazo TDMA wanatakiwa kuzifanya ni upimaji wa bidhaa za tumbaku kwa kuangalia ubora wa bidhaa za tumbaku kuhakikisha bidhaa za tumbaku zina kiwango cha nikotini kinachokubalika na kuhakikisha kuwa kemikali hatarishi hazizidi kiwango kinachokubalika.

 

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/d76e602e29a4637368e152f8c6558ea1.jpg

Mteja anayetaka kutuma mzigo nje au kupitishia ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi