loader
Dstv Habarileo  Mobile
Khadija Hemed Mwenda, Mtendaji aliyejipanga kuipaisha OSHA kimataifa

Khadija Hemed Mwenda, Mtendaji aliyejipanga kuipaisha OSHA kimataifa

UKIZUNGUMZIA mafanikio yanayoendelea kuonekana ndani ya Taasisi inayojihusisha na masuala ya Usimamizi ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi nchini (OSHA), nyuma yake kuna Khadija Hemed Mwenda anayeitumikia nafasi ya Kaimu Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo tangu alipojiunga nayo Mwaka 2012 kama Mkurugenzi wa Fedha, Utawala na Mipango.

Khadija mzaliwa wa Kijiji cha Ngujini-Kilaweni kilichopo Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro anasimama kama mwanamke mwenye uthubutu mkubwa ndani ya OSHA tangu alipojiunga nayo akiletea mafanikio yaliyoendana na mabadiliko mbalimbali ndani ya taasisi kiasi cha kuwafanya watumishi wote kuwa kama watu wa familia moja.

Anasema alipojiunga na OSHA akitoka kuitumikia nafasi ya Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Tanzania Investment Bank (TIB), kwa pamoja na wafanyakazi wa taasisi hiyo wamesimama kuwa kitu kimoja zaidi akitumia uzoefu wake wa zaidi ya miaka 17 katika taasisi mbalimbali za kifedha kuibadilisha OSHA ambayo kwa kipindi hicho ilikuwa ‘taabani’ tofauti na muonekano wake wa sasa.

“Nilikuja na kukuta hali si nzuri kabisa, kuanzia mazingira ya Ofisi, vitendea kazi, hali ya kazi na maslahi ya watumishi lakini zaidi uwezo wa taasisi kuwajibika katika utekelezaji wa majukumu yake, hatua hiyo na nyingine nyingi ziliifanya taasisi kuwa kama mtoto aliyekuwa amepoteza dira, kwa sasa tunamshukuru Mungu mambo yanakwenda vizuri kiasi cha kuifanya OSHA kutambulika hadi kimataifa” anasema Mwenda.

Anasema mara baada ya kuteuliwa kushika nafasi ya Kaimu Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, malengo yake makuu yalikuwa kuhakikisha taasisi hiyo inajijenga kiuchumi kwa kuweka mikakati mbalimbali ya kuiingizia fedha kupitia taratibu za usajili na utozaji tozo wa taasisi hatua iliyoiwezesha OSHA kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kutoka Sh bilioni nne katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 hadi Sh bilioni 22 mwaka 2019/2020.

Anasema katika kipindi hicho pia waliweza kufanya ukaguzi wa masuala ya usalama na afya kutoka kaguzi 22,470 katika kipindi mwaka 2013/2014 hadi ukaguzi 173,116 katika kipindi cha mwaka 2019/2020 sambamba na kuongezeka kwa ukaguzi sehemu zilizofanyiwa ukaguzi kwa mwaka kutoka 5,549 kipindi cha mwaka 2013/ 2014 hadi kufikia sehemu 20,026 katika kipindi cha mwaka 2018/2019.

Anasema pamoja na hilo pia taasisi hiyo imeweza kuongeza kiasi cha utoaji wa gawio Serikali kutoka Sh bilioni mbili katika kipindi cha mwaka 207/2018 hadi kufikia Sh bilioni 8.3 katika kipindi cha mwaka 2019/2020 na kusisitiza kuwa anaamini kadri siku zinavyokwenda OSHA inapiga hatua zaidi katika suala hilo kwa lengo la kuisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake.

“Ukiacha hao pia taasisi yetu imeweza kuanzisha mifumo mbalimbali ya usajili, mafunzo na ukaguzi katika sehemu za kazi yaani Work place Information Management System (WIMS) ambayo kimsingi inatupunguzia majukumu ya kwenda maeneo husika na kufanya ukaguzi huo. Lakini kubwa zaidi OSHA inajivunia kuwa kampuni iliyopata hati safi ya ukaguzi kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo” anasema Mwenda

Kaimu Mtendaji Mkuu huyo wa OSHA anasema mbali na mafanikio katika kipindi hicho pia ameiwezesha taasisi hiyo kuongeza miundombinu kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Mwanza, Mtwara pamoja na Dodoma ambapo kwa sasa wanaendelea kukamilisha ujenzi wa jengo la ghorofa tano kwa ajili ya Ofisi za taasisi hiyo linalotarajiwa kukamilika wakati wowote kuanzia sasa.

Hayo ni baadhi lakini anasema kubwa kwao OSHA ni lengo lao kufahamika katika Bara zima la Afrika katika eneo hilo la usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahala pa kazi ili kuzidi kuitangaza Tanzania huku akisisitiza kuwa kwa sasa hakuna taasisi yenye jukumu la kutekeleza suala hilo katika ukanda huo zaidi ya OSHA Tanzania.

“Tumekuwa tukipata wageni kutoka mataifa mbalimbali wanaokuja katika ofisi zetu ili kujifunza namna tunavyofanya kazi, ukweli tumekuwa mahili sana katika eneo hili na kutokana na hilo niliweza kufanya ushawishi kwa baadhi ya viongozi wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili kuwa na dawati la pamoja la masuala ya usalama na afya mahala pa kazi, ombi ambalo lilikubaliwa” anaongeza Mwenda.

Anasema kimsingi anasimama katika taasisi hiyo na kuamua kuzichukua aina zote za changamoto na kuzifanya kuwa fursa huku akisifu suala la uelewa kuhusu suala la usalama na afya lilivyojengeka kwa sasa miongoni mwa taasisi mbalimbali na watanzania kwa ujumla tofauti na ilivyokuwa miaka miaka ya nyuma huku akisisitiza kuwa malengo yake ni kwenda mbali zaidi kwa kufungua chuo kitakachokuwa kikifundisha masuala hayo.

Anasema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwa na taifa linalotambua umuhimu wa usalama na afya maeneo ya kazi, ikizingatiwa kuwa asilimia kubwa ya ajali zinazotokea hapa nchini huhusisha maeneo hayo hususani ndani ya sekta binafsi ambayo yameajiri watu wengi na zaidi akisifia namna ambavyo taasisi hiyo imeweza kubadilika kutoka kuwa msimamizi wa sheria hadi kuwa mshirikishaji katika utoaji wa elimu ya masuala ya usalama na afya mahala pa kazi.

Anasema hiyo ndiyo dhamira yake na zaidi amesisitiza anazidi kupata matumaini na moyo wa kuipeleka mbele taasisi hiyo akivutiwa zaidi na kuiga utendaji kazi wa Rais Samia  Suluhu Hassana ambaye anasema kwake yeye amekuwa kama mfano halisi kwa namna anavyowajibika katika utendaji wake tangu alipokuwa Waziri katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Mastaafu Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais katika Serikali ya awamu ya tano chini ya Hayati Dk John Magufuli, hadi  anaposimama kuliongoza Taifa kwa nafasi ya Urais.

“Ukweli Mama Samia ni mfano wa viongozi katika Bara hili mwenye aina ya kipekee ya uongozi, kwa kipindi kifupi tangu aanze kuliongoza taifa hili wengi wameona matunda yake, amekuwa kiongozi mahili mwenye weledi wa kutosha ambaye wengi tunaamini kuwa atatufikisha mbali mahali ambapo kila mtanzania anapataka, ameonesha kwa vitendo kauli ya mama ni mama, tupo nyuma yake na kama watanzania tutazidi kumuunga mkono,” anasema Mwenda.

Anasema aina ya uongozi wa Rais Samia ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine wakiwemo watendaji na wakuu wa taasisi mbalimbali akiamini kuwa kwa kufanya hivyo kutazidi kuhimarisha misingi ya kiutendaji jambo ambalo litamsaidia Rais kutimiza malengo aliyoyaweka katika kuwatumikia Watanzania sanjari na kuliletea taifa mafanikio.

 

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2ac0cb7eab1c51beb53ec3a34f3472f6.JPG

Mteja anayetaka kutuma mzigo nje au kupitishia ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi