loader
Dstv Habarileo  Mobile
Samia: Mwanza kuwa kitovu cha biashara

Samia: Mwanza kuwa kitovu cha biashara

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema utekelezaji wa miradi mikubwa mkoani Mwanza ukiwemo wa Reli ya Kisasa (SGR), Daraja la John Magufuli, ujenzi wa meli za mizigo na abiria na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, una nia ya kuifanya Mwanza kuwa kitovu cha biashara kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Ameyabainisha hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi wa ujenzi wa SGR kipande cha tano kutoka Mwanza hadi Isaka chenye urefu wa kilometa 341 kwa gharama ya Sh trilioni 3.1.

Rais Samia alisema tayari tathmini imeshafanyika na inaonesha kuwa miradi hiyo itakapokamilika, hakuna nchi itakayoweza kushindana na Tanzania katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

“Tunataka Dar es Salaam iwepo Mwanza kwa sababu hakuna haja ya wafanyabiashara wa nchi jirani kwenda mpaka Dar es Salaam kufuata mizigo yao, mizigo italetwa hapa na wataichukua hapa kwenda kwenye nchi zao. Miradi hii italifanya Jiji la Mwanza kuwa kitovu cha biashara na jambo hili litatupatia sifa sana katika ushindani Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika,” alisema Rais Samia.

Rais Samia aliridhishwa na ujenzi wa Daraja la Magufuli ambalo ujenzi wake unagharimu Sh bilioni 716 na limefikia asilimia 27, akieleza kuwa litafungua milango ya biashara siyo kwa Watanzania tu, bali kati ya Tanzania na nchi jirani na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa mbali mbali za biashara zinazojitokeza sasa na zitakazojitokeza.

 

Kuhusu ujenzi wa meli, alisema leo atashuhudia utiaji saini mikataba mitano ya ujenzi na ukarabati wa meli kwa ajili ya kutoa huduma katika Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika yenye thamani ya Sh bilioni 438.8.

“Kwa Ziwa Victoria miradi itakayosainiwa itahusu ujenzi wa meli mpya ya kubeba mabehewa yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 na kukarabati meli ya mabehewa ya Mv Umoja yenye uwezo wa kubeba tani 1,200. Pia tumekarabati meli ya Mv Victoria na tukamilisha ujenzi wa cherezo,” alifafanua Rais Samia.

 

Katika azma ya kuifanya Mwanza kuwa kitovu cha biashara, alisema serikali inakamilisha ujenzi wa jengo la Kiwanja cha Ndege Mwanza, itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mwamanga-Misasi-Kahama yenye urefu wa kilometa 149, barabara ya Magu-Ngudu-Jorijo kilometa 64 na Kamanga-Sengerema kilometa 35.

Alisema kujengwa kwa SGR kutoka Mwanza hadi Isaka kutatoa ajira 11,000 kwa Watanzania na kuongeza kuwa reli yote kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza itakapokamilika, itapunguza muda wa kusafiri kutoka saa 17 za sasa hadi kufikia saa nane tu, kupunguza gharama za usafirishaji mizigo kwa asilimia 40, kuongeza mapato ya serikali, na italinda barabara.

Alisema kutokuwepo kwa miundombinu madhubuti ya usafiri na usafirishaji barani Afrika, kunakwamisha maendeleo na kuongeza gharama za bidhaa kwa asilimia 40 na ukuaji wa biashara kuwa chini ya asilimia 20 ikilinganishwa na Mabara ya Asia, Ulaya na Amerika.

Aliwataka Watanzania wasibaki kuwa watazamaji bali wachangamkie fursa za biashara zitakazotokana na kukamilika kwa miradi hiyo ili kujiletea maendeleo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei, Michael Zhang alisema kwa sasa kampuni hiyo inashirikiana na TRC kutoa vifaa vya mawasiliano na huduma kwenye mradi wa SGR ikiwemo Mfumo Teknolojia ya Mawasiliano-Reli (GSM-R), ambayo baadae itabadilika kuwa mfumo wa LTE- R.

"Niimani yetu kwamba chini ya uongozi mpya wa Rais Mama Samia Suluhu , Huawei itaendelea kujenga Miundombinu ya TEHAMA kulingana na Dira ya maendeleo ya Tanzania 2025," aliahidi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/9e35de957601e7014b716ad81283722e.png

ALIYEKUWA Mbunge Mteule wa Jimbo la Konde ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi