loader
Dstv Habarileo  Mobile
Bandari ndogo ya Kipumbwi  daraja kwa wafanyabiashara wengi

Bandari ndogo ya Kipumbwi daraja kwa wafanyabiashara wengi

MOJA ya majukumu ya Bandari ya Tanga ni kusimamia Bandari ndogo zote zinazopatikana katika mwambao wa Bahari ya Hindi katika mkoa huo. Bandari hizo ni Mkwaja, Sahare na Kipumbwi.

Katika makala iliyopita tuliona namna bandari ya Mkwaja inavyotengeneza mapato kupitia usafirishaji wa mifugo na mkaa.

Katika makala haya tunaitazama Bandari ya Kipumbwi inayopatikana katika Wilaya ya Pangani inavyoongeza makusanyo ya fedha kupitia biashara ya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar kadhalika kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara..

Bandari hii ilianzishwa au kurasimishwa Oktoba 2019 na kutokana na umuhimu wake kwa wafanyabiashara imechangamka na kuvutia maelfu ya wananchi pamoja na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam na Bagamoyo kufanya biashara na kuweka makazi yao ya kudumu katika Mji wa Kipumbwi.

Ofisa wa Bandari ya Kipumbwi, Ulenga Ndaro anasema bandari hiyo ni maarufu kwa usafirishaji wa mizigo inayoingia kutoka Zanzibar na inayotoka Tanzania Bara kuelekea Zanzibar kupitia wafanyabiashara wa pande zote mbili.

Anasema Bandari ya Kipumbwi inafanya vizuri katika usafirishaji wa mizigo ya mazao ya misitu kama vile mkaa, mbao, magogo pamoja na mazao ya kilimo kama nazi na mihogo, vyote vikitoka Tanzania Bara kuelekea Zanzibar.

Kwa upande wa bidhaa zinazotoka nje kuja Tanzania Bara kupitia Bandari ya Kipumbwi ni pamoja na vifaa vya umeme, vya majumbani kama majokofu, runinga na bidhaa nyingine nyingi za madukani.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Bandari ya Tanga katika bandari zake ndogo za Kipumbwi, Mkwaja na Sahare zinazoonesha kwamba Bandari ya Kipumbwi ilifanya vizuri kwa mwaka uliopita kwa kupitisha tani 23,459 za mizigo ikilinganishwa na Mkwaja iliyopitisha tani 6,186 na Sahare tani 3,741. Hizi ni takwimu za kuanzia Januari hadi Desemba 2020.

Ndaro anasema haya ni mafanikio makubwa kwa Bandari ya Kipumbwi ambayo awali kabla ya kurasimishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) serikali ilikuwa ikipata hasara kutokana na mizigo hiyo kupita bila kukaguliwa wala kulipiwa ushuru. Athari zake pia ilikuwa ni kutumika kupitisha bidhaa hatarishi kwa maisha ya wananchi.

Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, Donald Ngaile anasema hatua ya kurasimishwa kwa bandari hizo ndogo kwa kuwekwa chini ya udhibiti wa TPA kulitokana na wafanyabiashara kukaidi sheria ya kupitisha mizigo yote katika Bandari ya Tanga kutokana na gharama wanazotakiwa kulipa pamoja na urahisi wa safari kutoka Kipumbwi hadi Zanzaibar.

“Tuliamua kutumia busara ya kawaida kwamba tuwaache wasafirishe mizigo yao kupitia bandari wanayoitaka wao wenyewe lakini wakifika katika bandari hizo watatukuta tunawasubiri na wataipa serikali stahiki zake yaani tumewapa uhuru wa kuchagua bandari waitakayo,” anasema Ngaile.

Ofisa wa Bandari Ndogo ya Kipumbwi, Ndaro anasema anapata ushirikiano mzuri kutoka kwa wafanyabiashara kwa kulipa tozo stahiki baada ya kukagua na kupima mizigo yao tayari kwa kuanza safari.

Anasema utendaji kazi wa Bandari ya Kipumbwi unawavutia wafanyabiashara wengi kusafirisha mizigo yao kwa kuwa hakuna ucheleweshaji wala kupoteza muda.

“Mteja anapofika na mzigo wake katika Bandari ya Kipumbwi ataonesha mzigo wake, utakaguliwa ili kuona kama hakuna kitu kingine kisha mizigo yote itapimwa ili kujua uzito wake na atalipia na kuondoka,” anasema Ndaro.

Anasema kutokana na uchapaji kazi wa haraka wafanyabiashara wengi wamehamia katika bandari hiyo na kufanya mji wote wa Kipumbwi kujaa watu na kuchangamka kwa kiasi kikubwa kulinganisha na bandari nyingine ndogo katika ukanda wa mwamboa wa Bahari ya Hindi katika Mkoa wa Tanga.

Takwimu zinaonesha kuwa katika robo ya mwisho ya mwaka 2019 Bandari ya Kipumbwi ilipitisha mizigo yenye uzito wa tani 3,884 wakati katika robo ya kwanza ya mwaka 2020 bandari hiyo ilipitisha mizigo yenye uzito wa tani 5,988.

Katika robo ya pili ya mwaka 2020 bandari hiyo ilipitisha mizigo yenye uzito wa tani 4,835 wakati robo ya tatu ni tani 4,891 na robo ya mwisho ni tani 3,861. Ndaro anasema kupitia mizigo hiyo bandari iliweza kukusanya fedha za kutosha zinazofika wastani wa Sh milioni 10 hadi 12 kwa mwezi.

“Wakati wa mvua mizigo inapungua kwa sababu inaweza kulowa hivyo bandari huwa inakusanya chini ya malengo. Mfano inaweza kukusanya hadi milioni nane hadi tano kwa mwezi lakini wakati wa kiangazi kuna usafirishaji mkubwa wa mizigo hivyo makusanyo yanapanda hadi kufikia milioni 10 hadi 15,” anasema Ndaro.

Kwa mujibu wa Ndaro bandari hiyo imejiwekea malengo makubwa kupitia utendaji wake ambapo imepanga kuvutia mizigo zaidi hadi kufikia tani 30,000 kwa mwezi.

Anasema ili kufanikisha hayo bandari hiyo inahitaji mambo kadhaa kufanyiwa kazi na Mamlaka ya Bandari Tanga, hatua anayoamini itaharakisha malengo waliyojiwekea.

Kwanza anasema ni vyema wajengewe ofisi ya Bandari ambayo itawezesha kuwepo kwa watumishi zaidi ili kuimarisha utendaji wa bandari hiyo. Suala lingine ni kuimarishwa kwa mitandao ili kurahisisha ukataji wa risiti kwa kuwa kazi yote inafanyika kimtandao.

“Hapa sasa hivi mteja akilipa ninalazimika kwenda hadi katika kijiji jirani cha Sakura ili kupata mtandao ili kumkatia mteja risiti. Hii inachelewesha utendaji kwa zaidi ya dakika tano na kumfanya mteja alalamike,” anaongeza Ndaro.

Anasema katika Bandari ya Kipumbwi kuna majahazi zaidi ya 14 yanayotoa huduma ya mizigo tu bandarini hapo, ingawa wakati mwingine kutokana na uhaba wa usafiri yanalazimika kubeba abiria wachache.

Ndaro anasema uwepo wa bandari hiyo umekuwa wa manufaa zaidi kwa wananchi na serikali kutokana na ukusanyaji wa mapato na kuwezesha kushamiri kwa biashara mbalimbali katika eneo hilo kunakowanufaisha wananchi moja kwa moja.

“Kabla ya ujio wa bandari hapa kulikuwa na vitu vingi sana vinapita kwa njia ya magendo lakini sasa serikali inapata fedha za kutosha na wananchi wamehamasika na kuwa msaada mkubwa kwa serikali kwa kufichua watu wote wanaotaka kupitisha vitu kwa magendo (au vitu hatarishi),” anaongeza Ndaro.

Bandari inatafsiriwa kama eneo lolote la ufukweni mwa bahari, ziwa au mto ambalo vyombo vya majini husimama kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya kubeba abiria na mizigo.

Kwa mujibu wa Sheria namba 17 ya mwaka 2004 iliyoanzisha TPA, bandari zote nchini zinapaswa kusimamiwa na TPA. Kuendesha bandari yoyote nchini bila usimimizi wa mamlaka hiyo ni kosa la kisheria.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/1d858805b8fb51ace95a95c5f1ec0b84.JPG

Mteja anayetaka kutuma mzigo nje au kupitishia ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi