loader
Dstv Habarileo  Mobile
Usalama wa Taifa katika falsafa  ya Rais Samia kupitia wanawake

Usalama wa Taifa katika falsafa ya Rais Samia kupitia wanawake

JUNI 8, mwaka huu (2021) Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na wanawake wa Dodoma waliowawakilisha wenzao wa Tanzania, ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu wake wa kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii.

Katika mkutano huo zilielezwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake nchini na kuwakosesha haki zao za msingi zilizoainishwa kwa mujibu wa Mkataba wa Haki za Binadamu wa mwaka 1948.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Rais Samia alieleza kuwa Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ikiwemo CEDAW 1979, Beijing 1995, Mkataba wa Mtoto 1989, Agenda 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Licha ya kuridhiwa kwa mikataba hiyo sambamba na Itifaki ya Maputo ya mwaka 2003, bado juhudi za dhati zinahitajika kuchukuliwa kumwokoa mwanamke kiuchumi kama alivyoainisha Rais Samia.

Rais ameonesha nia ya dhati kulipigania hili na kuhakikisha serikali yake inaleta usawa wa kijinsia kwa kuahidi kuyalea Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa kuwa kumwezesha mwanamke si tu kunaleta usawa wa kijinsia kama lilivyoainisha lengo namba 5 la SDGs bali pia kunaleta amani na usalama duniani kwa mujibu wa tamko la Umoja wa Matifa la  2015.

Ndiyo maana makala haya yanaitazama dhana ya usalama wa taifa la Tanzania katika muktadha wa mkakati wa Rais Samia wa kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuondoa umasikini.

 

Ni ukweli ulio wazi kuwa tukizungumzia umasikini nchini basi huenda wanawake ndiyo masikini wa kweli kabisa ukilinganisha na wanaume, hivyo changamoto hii ni dhahiri ni kitisho cha kiusalama.

Takwimu za sensa ya mwaka 2002 na mapitio ya mwaka 2021 zinaonesha kuwa kati ya watu 59,441,988 wanawake ni 30,309,750, sawa na asilimia 51 ya watu wote nchini.

Asilimia kubwa ya wanawake hawa milioni 30 wamejiajiri katika kilimo kama ripoti ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (TNBS) ya mwaka 2015 inavyobainisha kwamba kilimo kimeajiri zaidi ya asilimia 70 ya idadi ya watu wote na zaidi ya asilimia 80 ya idadi hiyo ni wanawake.

Hata hivyo, umiliki wa ardhi wanayolima wanawake hawa bado uko kwa wanaume!

Wanawake wengi hata mijini ndio wasio na kipato kwa kutokuwa na kazi au biashara kubwa, wengi wakifanya ujasiriamali kama wa mama lishe na kuchoma maandazi.

Licha ya kwamba takwimu hizi ni za miaka mitano iliyopita na labda huenda kukawa na mabadiliko madogo lakini haziondoi ukweli kuwa wanawake wengi wamejiajiri kwenye kilimo hiki cha kujikimu.

TAFSIRI NI NINI?

Tafsiri ni kwamba mabadiliko yoyote hasi kwenye sekta ya kilimo yakisababishwa na vitu kama vile mafuriko na ukame yana athari ya moja kwa moja kwa wanawake na hivyo kuhatarisha usalama wa taifa. Kwa lugha nyingine mabadiliko chanya kwenye kilimo ni kuimarisha usalama wa taifa.

 

Ili kuona ni kwa kiasi gani kumwezesha mwanamke kiuchumi ni sawa na kuimarisha usalama wa taifa ni vema kwanza tufahamu kwa ufupi dhana ya usalama wa taifa.

Kwa miaka mingi dhana hii ilikuwa ikitazamwa kwa mtazamo asilia (traditional) na wa kidola (state-centric) unaotokana na mrengo wa kulia (realism) kwamba uwepo wa dola moja ni kitisho cha kiusalama kwa dola nyingine na hivyo nchi kutamani zisizungukwe na nchi nyingine pembeni mwao (Rejea Wolfer, 1962; Buzan, 1991; Buzan na wenzake 1998; Nnoli, 2006 na Buzan na Stone, 2009).

Kwa hali hiyo nchi ilipaswa kujihakikishia kuendelea kuwepo (state survival) kwa kulinda mipaka yake dhidi ya vitisho vyovyote kutoka nje.

Lakini ripoti ya Maendeleo ya Mwanadamu ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ya mwaka 1994 ilibadili mtazamo huu kwa kuainisha vitisho vipya vya kiusalama vikijumuisha umasikini, njaa na magonjwa kama tunavyoona sasa ugonjwa wa corona (Covid 19) unavyotesa dunia.

Hivyo basi, kwa maana nyingine usalama wa mwanadamu ndiyo kitovu cha usalama wa taifa.

Kwa tafsiri hii ya UNDP, ni dhahiri kuwa changamoto zilizoainishwa katika risala ya wanawake iliyosomwa na mwakilishi wao, Joyce Kashozi zikiwemo za umasikini, umiliki mali na mitaji, kukosekana usawa katika vyombo vya maamuzi, njaa na maradhi ni changamoto za mwanadamu na kwa kuwa wanawake wapo wengi nchini basi changamoto hizi ni kitishio kwa usalama wa taifa.

NINI KIFANYIKE?

Kwa mtazamo wangu, kuna haja kwa serikali kuangalia namna bora ya kuwekeza kwenye kilimo bora na cha kisasa ili kuwanyanyua wanawake kiuchumi na kuweza kufikia dhana nzima ya usawa kwa sababu zaidi ya wanawake milioni 24 kati ya wanawake wote milioni 30 na ushei wako kwenye kilimo.

Ripoti ya Shirika la Chakula Duniani (FAO) ya mwaka 2002 ilisema "kilimo ndiyo uti wa mgongo wa nchi zinazoendelea katika kuimarisha usalama wa chakula, kuzalisha mapato yatokanayo na kilimo, kusafirisha bidhaa za kilimo na uendelezaji wa maeneo ya vijijini."

Mbali na ripoti hiyo ya FAO, Li (2010: 2011), West na Haung (2017), Bluwstein na wenzake (2018) na Engstrom na Hajdu (2018) wamesema kwamba sekta ya kilimo ndiyo inayoongoza katika nchi nyingi zinazoendelea hasa vijijini, na kwa Tanzania asilimia 70 ya wanawake hupata huduma zao za kimaisha kutokana na shughuli za kilimo (TNBS, 2015).

Hivyo sekta ya kilimo nchini ambayo ndiyo sekta iliyoajiri wanawake wengi ni sekta muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula, kuleta kipato na kuzalisha ajira.

Ripoti ya FAO ya mwaka 2002 inasema kwamba sekta ya kilimo katika nchi zinazoendelea inapaswa kuangaliwa kwa jicho pana wakati huu nchi zinazoendelea zinapoweka umakini katika sera nyingine.

Gautier (2020) katika andiko lake anaeleza kwamba tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Ulaya, Ufaransa imeendelea kuongoza katika uzalishaji na uuzaji wa mazao ya kilimo katika bara zima la Ulaya.

Kama Ufaransa imelikamata soko la Ulaya kupitia bidhaa za kilimo, kwa nini Tanzania isitumie ardhi yake kubwa kukamata soko la bidhaa za kilimo la Afrika na nje ya mipaka yake, manufaa ambayo wanawake milioni 24 waliojiajiri katika kilimo watanufaika zaidi?

Mbali na hili la Ufaransa kuliteka soko la Ulaya kwa bidhaa za kilimo, Jimbo la California limeizidi hata nchi ya Uingereza kiuchumi kutokana na uchumi wa jimbo hilo kubebwa na kilimo.

Takwimu za Wizara ya Biashara ya Marekani za mwaka 2020 zinaonesha kuwa California yenye asilimia 12 ya watu wote wanaoishi Marekani inachangia takribani asilimia 15 ya pato ghafi (GDP), sehemu kubwa ikitokana na kilimo.

Hivyo naamini kama nchi tukiweza kuwa namna bora ya kuyawezesha majukwaa 23 ya uwezeshaji wanawake kiuchumi aliyoyaainisha Rais Samia yaliyopo kila mkoa, 144 katika wilaya, 302 katika kata na 522 katika ngazi ya vijiji na mitaa tutakuwa tumeokoa zaidi ya wanawake milioni 24 waliojiajiri katika kilimo.

Kama nchi tutaweza kuzalisha kwa wingi na kuuza bidhaa nje hasa tukizingatia tuna nchi nane zinazotunguka ambazo ni Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Msumbiji na Zambia. Lakini kuna nchi kama Comoro na Magascar pia zinategemea sana bidhaa za kilimo kutoka Tanzania.

NAMNA YA KUWAWEZESHA WANAWAKE

Serikali inaweza kupitisha misaada yenye masharti na riba nafuu kupitia benki zilizopo nchini ambapo wanawake kupitia majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi watakopeshwa na kwenda kuwekeza kwenye kilimo cha uwekezaji mkubwa.

Majukwaa haya yanaweza kulima mazao kulingana na mazingira ya eneo husika, kwa mfano Kigoma chikichiki, Mwanza pamba, Mtwara korosho, mikoa ya kati alizeti na mengine mengi.

Kwa kufanya hivi tutakuwa tumejenga mfumo imara utakaowezesha wanawake kuwa na nguvu ya kiuchumi, utakaofanya nchi kunufaika kiuchumi kwa kuzalisha ajira zenye kukidhi mahitaji yaliyopo na kuepuka yale aliyosema Osabuohein na wenzake (2019) kwamba, tunahitaji kuwa na mfumo bora wa kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Mfumo huu wa kupitia majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ukijielekeza kwenye kilimo pamoja na kutoa elimu kilimo cha kisasa ndiyo unaweza kuwaokoa wanawake zaidi ya milioni 24 kutoka kwenye umasikini wa kipato na hivyo kuleta usawa wa kijinsia katika nyanja zote pamoja na usawa wa kisiasa kwani  wanawake wakiwa na nguvu za kiuchumi wataweza pia kumudu siasa vilivyo.

Kwa hatu hiyo tutakuwa pia tumekabiliana vema na vitisho vya kiusalama visivyo vya kiasili vya umasikini, njaa na maradhi.

Kwa mantiki hiyo, uamuzi huu wa Rais Samia kuyalea Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ni sawa na falsafa mpya ya usalama wa taifa iliyojikita katika uwezeshaji wa wanawake ambao licha ya wingi wao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliamo yake ni +255 719 258 484.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c26292da67a1ad5d3d8d0d736821ef12.jpg

Mteja anayetaka kutuma mzigo nje au kupitishia ...

foto
Mwandishi: Abbas Mwalimu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi