loader
Dstv Habarileo  Mobile
Hawa wamekatwa

Hawa wamekatwa

KAMATI ya Uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) imewaondoa, Ally Mayay, Ally Saleh na Oscar Oscar katika kinyanganyiro cha kugombea urais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa sababu mbalimbali.

Akizungumza na HabariLEO jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Benjamin Kalume alisema wagombea waliopita baada ya kukidhi vigezo vyote ni anayetetea nafasi hiyo, Wallace Karia, Hawa Mniga na Deogratius Mgeusa.

“Kuna sababu mbalimbali zilizowafanya baadhi ya wagombea kuenguliwa katika mchujo wa awali, ikiwamo kushindwa kukidhi matakwa ya kikanuni, kutojaza kikamilifu fomu, kukosa idadi ya wadhamini inayotakiwa na kutoambatanisha nakala za vyeti katika fomu,” alisema Kalume.

Alisema Mayay alipata mdhamini mmoja badala ya watano kama kanuni zinavyosema na pia hakuweza kuthibitisha vyeti vyake kwa kamishna wa viapo na pia hakuambatanisha nakala ya kitambulisho cha uraia.

Kwa upande wa Ally Saleh, alisema hakupata mdhamini hata mmoja na hakudhibitisha vyeti vyake kwa kamishna wa viapo na Oscar Oscar hakupata mdhamini hata mmoja.

“Karia alikidhi vigezo vyote ikiwamo kupata wajumbe 18, Mniga alipata wadhamini sita pamoja na Mgeusa, hivyo wamepita katika mchujo wa awali ila ruksa kuwekewa pingamizi,” alisema.

Katika nafasi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliopitishwa kupitia kanda namba moja ya mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Morogoro na Pwani ni Lameck Nyambaya,  Athuman Kambi  na Hosseah Lugano.

Alisema Liston Katabazi, Elisony Mweladzi na Jimmy Shomari hawakupata udhamini na Saady Khimji alipata udhamini kutoka klabu ya Yanga kitu ambacho siyo sahihi kwani alitakiwa kupata udhamini kutoka chama cha soka cha mkoa.

Kanda namba mbili ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga waliopitishwa ni Khalid Abdallah na Zakayo Mjema, huku Thabity Kandoro hakupitishwa kwa kukosa mdhamini.

Kanda namba tatu ya mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma na Songwe waliopitishwa ni Abousufian Sillia, James Mhagama na Mohamed Mashango, huku Denis Manumbu na Joseph Ngunangwa wakienguliwa kwa kukosa wadhamini.

Kanda namba nne ya mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Dodoma na Singida waliopitishwa ni Osuri Kosuri, Mohamed Aden na Juma Kitila, huku Mrisho Ramadhan akienguliwa kwa kukosa wadhamini.

Kanda namba 5 ya mikoa ya Geita, Kagera, Mara na Mwanza waliopitishwa ni Salum Chama, Vedastus Lufano na Salum Kulunge.

Kanda namba sita ya mikoa ya Tabora, Kigoma, Rukwa na Katavi waliopitishwa ni Blass Kiondo, Issa Bukuku na Keneth Pesambili.

Kalume alisema waliopita kwenye mchujo wa awali wanatakiwa kufika kwenye usaili wakiwa na vyeti halisi pamoja na uthibitisho wa uzoefu wao katika uongozi.

Karia aliingia madarakani Agosti 12, 2017 katika uchaguzi uliofanyika jijini Dodoma, ambapo alipata kura 95 kati ya kura 127, akifuatiwa na Ally Mayay aliyepata kura tisa sawa Shija Richard.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2321a5db170ba54aa7147f87efcb16ec.png

YANGA leo inashuka katika Uwanja wa Benjamin ...

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi