loader
Dstv Habarileo  Mobile
Utafiti waibua malisho bora rafiki wa mazingira

Utafiti waibua malisho bora rafiki wa mazingira

WAFUGAJI wa ng'ombe wa maziwa nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya malisho bora yanayowezesha mifugo yao kutoa maziwa mengi, hasa kipindi cha kiangazi.


Changamoto ya malisho inayopunguza maziwa wakati wa kiangazi imekuwa si tu kwa wafugaji bali hata kwa viwanda vya kuzalisha maziwa.
Kwa kuliona hilo, serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilifanya tafiti mbalimbali ili kuhakikisha wafugaji nchini wanazalisha maziwa kwa wingi kwa mwaka mzima.


Miongoni mwa jitihada na tafiti hizo ni kupitia mradi wa malisho ambayo ni rafiki wa mazingira unaoendeshwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (Taliri), Kanda ya Tanga, na Shirika la Utafiti wa Malisho Afrika (CIAT).


Kupitia tafiti, mradi umekuja na mazao kadhaa ya malisho yanayostahimili ukame na tayari mashamba darasa ya malisho ya mifugo yamefunguliwa ili wafugaji wajifunze kulima malisho kama kilimo kingine cha mazao ili wawe na uhakika wa malisho kipindi chote cha mwaka.


Kutokana na mafanikio ya mradi huo hivi karibuni timu ya wafugaji na wazalishaji wa malisho ya mifugo kutoka mikoa ya Njombe, Mbeya, Tanga na Kilimanjaro walifika jijini Tanga katika Taasisi ya Taliri ili kujifunza juu ya aina za mbegu za malisho yanayostawi maeneo yenye mvua na yale yanayostahimili ukame.


Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Angelo Mwilawa, anasema kuwa serikali inakusudia kuendelea kufanya tafiti zaidi za malisho ya mifugo baada ya kuona matunda ya tafiti ambazo zimeshafanyika.


Anasema serikali itahakikisha inaendelea kuzijengea uwezo taasisi zake ili ziweze kuwasaidia wafugaji kupata malisho yenye ubora ambayo yatasaidia kubadilisha ufugaji wao kuwa wa kisasa na wenye kutoa mazao bora.

 

“Kwa kutumia malisho haya yaliyoboreshwa tunatarajia kuhakikisha mifugo inazalisha maziwa kwa ubora lakini kwa kuzingatia malisho yanayokuwa pia rafiki wa mazingira,” anasema Dk Mwilawa.


Anaongeza: “Kiu kubwa ya Serikali ni kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa malisho kwa wafugaji wetu inamalizika kabisa na tunapata faraja kubwa pale tunapowaona wafugaji wetu wananufaika na matunda ya tafiti mbalimbali za malisho ambazo tumekuwa tukizifanya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.”


Anabainisha kuwa ziara hizo za wafugaji zitaisaidia serikali kupata maoni yao juu ya mambo ambayo wangependa yafanyiwe kazi ili waendelee kuwa na ufugaji na uzalishaji malisho wenye tija na utakaowanufaisha zaidi.


“Napenda niwashukuru wadau wetu ambao wamekuwa nasi katika kufanikisha tafiti mbalimbali zinazolenga kuwasaidia wafugaji wetu likiwemo shirika la CIAT na sisi kama serikali tunawaahidi tutaendeleza yale ambayo wametusaidia hata mara baada ya mradi kuisha,” anasema Dk Mwilawa.
Kwa upande wake, Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Malisho Rafiki wa Mazingira, Dk An Notenbaert, anasema kuwa Taliri kwa kushirikiana na CIAT, waliweza kuendesha mradi huo wa utafiti wa malisho kwa kipindi cha miaka minne.


Anasema kuwa malisho hayo yameonesha tija kubwa kwa wafugaji kwani wameweza kuyavuna katika kipindi chote cha mwaka huku mifugo ikizalisha maziwa kwa wingi tofauti na hapo awali.


“Licha mradi kufikia ukingoni lakini nina furaha kusema kuwa utafiti huu wa malisho umeweza kuwa na matokeo bora kwa wafugaji na hivyo umesaidia kutatua changamoto ya malisho bora kwa mifugo yao,” anasema Dk Notenbaert.


Anasema kuwa wafugaji wamekuwa tayari kujifunza teknolojia hii mpya ya kupanda malisho kwani walianza na wafugaji 36 pekee lakini sasa mbegu zimeweza kusambaa kwa wafugaji wengi zaidi katika kipindi kifupi.


Wafugaji kwa upande wao wanaishukuru serikali kuleta mradi huo ambao wanasema utawasaidia sana kuwa na uhakika wa malisho kipindi chote cha mwaka na tayari wameona faida kubwa ya kupanda malisho hayo.


Mfugaji kutoka Muheza, Ester Makenye anasema kuwa hapo awali waliletewa aina mbalimbali za nyasi kwa ajili ya mifugo yao lakini kupitia mradi huo mbegu ya nyasi aina ya Kobra imeonyesha matokeo mazuri na ya haraka.


“Katika miezi michache tuliyoiotesha tumeona manufaa zaidi kwenye uzalishaji wa maziwa kwenye mifugo yetu, hivyo tupo tayari kuanzisha mashamba zaidi kwa ajili ya kuzalisha nyasi ili mifugo yetu iweze kupata malisho bora,” anasema Makenye.


Mfugaji kutoka Wilaya ya Njombe, Suzan Chagawa anaiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kufanya tafiti kwa ajili ya nyasi asilia ili kuona namna ambavyo wataweza kuziboresha ili nazo ziweze kutoa matokeo bora.


“Teknolojia mpya tunaihitaji lakini hata malisho ya asili yanaweza kufanyiwa utafiti ili kuona kama yanaweza kutoa matokeo bora zaidi kwa wafugaji hususani wale wanaoishi katika maeneo ya vijijini,” anasema Suzan.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Suzan anasema kuwa amefurahishwa na aina nyingi za malisho ya mifugo alizozikuta shambani hapo ingawa amebainisha kuwa hali ya hewa ya baridi iliyopo kwenye mkoa wake inaweza kuwa changamoto inayofanya aina nyingi za malisho zisistawi vizuri.
“Kutokana na changamoto hiyo huwa tunakata malisho tuliyoyapata wakati wa masika kisha tunayakata na kuhifadhi ili yatusaidie wakati wa kiangazi,” anasema.


Gwamaka Mwakiambiki ambaye ni mfugaji kutoka Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, anasema kuwa jambo alilojifunza mara baada ya kufika kwenye shambani darasa ni kuzalisha aina nyingi za malisho ya mifugo badala ya kutegemea aina moja tu ya majani aina ya “brachiaria” ambayo ndio yanayostawi vizuri katika mkoa wake.


“Tunalishukuru sana shirika la CIAT kwa sababu tangu lilipokuja tumejifunza namna ya kupanda malisho bora na yanayoipa mifugo yetu afya bora,” anasema Mwakiambiki.


Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikishirikiana na mashirika mbalimbali ya kimataifa kwenye tafiti za malisho ya mifugo ikiwa ni jitihada za kumaliza changamoto ya malisho ya mifugo nchini.


Mradi wa malisho ambayo ni rafiki wa mazingira umekuwa ukitekelezwa katika wilaya za Rungwe, Njombe, Mufindi, Muheza, Mkinga na Hai na unatarajiwa kufikia ukomo wake mwaka huu. 
 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c2b63402279a752a445b4e53036ac979.jpg

Mteja anayetaka kutuma mzigo nje au kupitishia ...

foto
Mwandishi: Amina Omari

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi