loader
Majaliwa awapa kazi wakandarasi wazawa

Majaliwa awapa kazi wakandarasi wazawa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania itaanza kutumia wakandarasi wake katika kujenga miradi mikubwa yakiwemo madaraja kwa sababu wameonesha kuwa wanaweza.

Alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD), Patrick Mfugale kuanza kutunza kumbukumbu za wafanyakazi wote katika miradi mbalimbali ikiwemo wasifu wao ili waweze kupewa miradi mikubwa wasimamie na kutekeleza wenyewe.

Majaliwa aliyasema hayo jana kutokana na taarifa ya Mtendaji Mkuu wa Tanroad kuwa wafanyakazi 886 kati ya 960 wanaojenga daraja la Selander ni Watanzania ambao ni sawa na asilimia 92 huku wageni wakiwa 74 sawa na asilimia 8 ya wafanyakazi wote.

Katika ziara hiyo iliyokuwa na lengo la kukagua maendeleo ya mradi huo, Majaliwa alisema serikali iliiagiza Tanroad kuhakikisha kuwa idadi ya Watanzania wanaoajiriwa katika miradi mikubwa wanakuwa wengi ili kuwapa fursa ya kujifunza na kutumia maarifa waliyopata vyuoni kuweza kutekeleza kivitendo na kuwa na ujuzi wa kutosha kiasi cha kuweza kufanya kazi bila msaada kutoka kwa wataalamu wa nje.

Pia Waziri Mkuu alisema lengo lingine kwa serikali kutaka Watanzania wengi zaidi katika miradi mikubwa ni kutoa faida kwa wazawa kupata ajira kwa wingi zaidi na kuwanyima wageni nafasi ya kuajiri watu kutoka nje ya nchi wakati Watanzania wenye uwezo wapo.

“Watanzania wote walioajiriwa katika miradi hii wahakikishe kila mmoja katika sehemu yake ajifunze vizuri ajue kila kitu. Kama wewe kazi yako ni kukoroga zege hakikisha unapata maarifa ya kutosha, kama ni kupima vipimo mbalimbali hakikisha kuwa unapata maarifa ya kutosha ili siku moja tuone mradi mkubwa kama huu unaendeshwa na nyie wenyewe bila kuhusisha wazungu,” alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Watanzania katika mradi huo,hakuna sababu ya kutafuta wataalamu wajenzi kutoka nje ya nchi kwa sababu Watanzania wanedhihirisha kuwa wanaweza,

Alisema amefurahi kuona Watanzania wamemthibitishia kuwa wanaajirika na ni waaminifu kutokana na kukosekana kwa taarifa za upotevu wa vitu mbalimbali kama nondo, saruji na vingine vingi.

Kiongozi huo ambaye pia ni Mbunge wa Rwangwa Mkoani Lindi alimuagiza Mfugale kuangalia afya za Watanzania wote wanaofanyakazi kwa sababu bila kuwa na afya njema hawataweza kufanya kazi wala kupata maarifa ya kiujenzi kutoka kwa wataalamu viongozi wa mradi.

“Nataka uangalie afya zao na pia ujali maslahi yao kwa sababu mradi huu ni wa Watanzania na kwa bahati nzuri unajengwa kwa asilimia kubwa na Watanzania, lazima tujali afya zao kwa karibu,” aliongeza Majaliwa.

Alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kufika leo saa nne asubuhi na watu wa utumishi kusikiliza kero za kiutumishi na nyingine kutoka kwa Wafanyakazi ili kuhakikisha kuwa wanafanyakazi kwa furaha na upendo kwa nchi yao.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanroad Patrick Mfugale alisema mradi wote wa ujenzi wa daraja la Selander umegharimu dola za Marekani milioni 123 zilizotolewa kwa mkopo kutoka Serikali ya Korea Kusini wakati Tanzania imetoa dola za Marekani milioni 4.23 kwa ajili ya kodi na gharama za uendeshaji na tozo mbalimbali stahiki katika utekelezaji wa mradi.

Alisema Mradi huo uliofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na Kampuni ya Yooshin Engineering Corporation kutoka Korea Kusini ikishirikiana na Afrisa Consulting Ltd ya Tanzania unajumuisha daraja lenye urefu wa kilomita moja na mita 30 na upana wa mita 20.5 likiwa limeunganishwa na barabara kwa pande zote mbili zenye urefu wa kilomita 5.2.

Kwa mujibu wa Mfugale, mkandarasi anayejenga mradi huo ni Kampuni ya GS Engineering Corporation kutoka Korea Kusini kwa gharama ya dola za Marekani milioni 107.4 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 243.75 katika kipindi cha miaka mitatu ambapo mradi unatarajiwa kukamilika Desemba 14, 2021.

Kwa upande wa Kampuni zinazosimamia ujenzi ni Yooshin Engineering Corporation kutoka Korea Kusini ikishirikiana na Afrisa Consulting Ltd ya Tanzania kwa gharama ya dola za Marekani milioni 3.4 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 7 .72.

Mfugale alisema mkandarasi alianza kazi rasmi Oktoba 2018 ambapo hadi kufikia Juni 16, 2021 utekelezaji wa kazi ulikuwa umefikia asilimia 83.5 zaidi ya malengo yaliyowekwa ambapo utekelezaji ulitakiwa katika kipindi hicho kuwa asilimia 81.9.

“Mpaka sasa mkandarasi amelipwa jumla ya shilingi bilioni 175.5 sawa na asilimia 72.02 ya fedha zote anazostahili kulipwa, mhandisi mshauri amelipwa shilingi bilioni 4.9 sawa na asilimia 80 na mpaka sasa fidia iliyotolewa kutokana na watu na taasisi ambazo ziliguswa na mradi ni shilingi bilioni2.4,” alisema Mfugale.

Mhandisi wa daraja la Selander, Lulu Dunia alimweleza Waziri Mkuu kuwa mkandarasi mpaka sasa amekamilisha ujenzi wa chini kwa maana ya nguzo 16 kwa asilimia 100 na kinachoendelea sasa hivi ni ujenzi wa juu kuunganisha nguzo kutoka mwanzo wa daraja hadi mwisho.

Alisema daraja hilo lina nguzo kubwa katikati ambayo itawekwa nembo ya mwenge juu na litakuwa likishikiliwa kwa kamba kutoka katika nguzo zake ambazo zitakuwa zikiwasha taa wakati wa usiku hali itakayoleta mvuto wa kipekee kutoka ardhini, majini na angani.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c736f9d5637692621c02e39139ec8268.JPG

RAIS Samia Suluhu Hassan amehutubia taifa ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi