loader
Dstv Habarileo  Mobile
‘Wagonjwa wa saratani jioneni mashujaa, msihofu’

‘Wagonjwa wa saratani jioneni mashujaa, msihofu’

NIPO katika viwanja vya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) ambako kuna kusanyiko la mamia ya watu wanaoonekana kuwa ni wenye furaha.

Wakiwa wamevalia fulana nyeupe, miongoni mwao wanacheza muziki unaosikika kutoka spika kubwa zilizopo kwenye viwanja hivi vilivyopo nyuma ya majengo haya ORCI. Mbele yangu namwona mwanadada ambaye anajitambulisha kuwa ni Gloria Kida, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Shujaa Cancer Foundation (SCF).

Namuuliza nini maana ya kusanyiko hili, anasema: “Hawa ni mashujaa wa saratani ambao wanasheherekea siku yao muhimu sana maishani mwao.” Anasema kwa hakika ni siku yao ya kufurahia maisha wakati na baada ya tiba kama ilivyo kwa watu wanaofanya sherehe ya kuzaliwa au kukumbuka tukio muhimu la maisha husheherekea kwa namna mbalimbali.

“Na hawa ndivyo ilivyo. Wako pamoja na madaktari wao, wauguzi, ndugu zao na wadau wanaotoa huduma mbalimbali kuwasaidia wagonjwa wa saratani.” Anaelezea kuwa sherehe hii inajumuisha madaktari na wauguzi waliofanya kazi kubwa ya tiba ambazo zinawafanya sasa wajione ni mashujaa.

Gloria anasema wagonjwa hawa wa saratani wana kila sababu ya kufurahia kwa sababu haikuwa rahisi kufikia hatua hii ambayo iliandamana na changamoto nyingi. Kuna baadhi ya wagonjwa ambao walifikishwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya ya kuwa na vidonda kinachotoa usaha na hata kuwa na wadudu kiasi cha kuwafanya ndugu na jamaa zao kuwamkimbia.

“Lakini walipofikishwa hapa wahudumu na madaktari waliwapokea vizuri na kuhangaika kuwasaidia na kuwapa huduma za tiba na sasa hali zao ziko vizuri na hata familia zao sasa wanakaa nao na kula nao,” anasema. Chimbuko la siku hii, anasema, ni maadhimisho ambayo yamekuwa yakiadhimishwa na mataifa mbalimbali duniani, ikiwapo Marekani.

Kwa Tanzania, anasema, kwa mara ya kwanza imefanyika mwaka huu na kuanzia sasa kila mwaka, Jumapili ya kwanza ya Juni, itakuwa ikiadhimishwa nchini sawia na mataifa mengine duniani. Hamasa ya maadhimisho haya, anasema imeanzishwa na asasi yao ya SCF ambayo imesajiliwa nchini kwa lengo la kuwahudumia mashujaa wa saratani ya via vya uzazi, yaani ya matiti, tezidume na mlango wa kizazi.

“SCF analenga katika kuainisha changamoto wanazopitia mashujaa wa saratani na kuratibu njia mbalimbali za kuwasaidia kukabiliana navyo,” anasema Glory akifafanua: “Hii ni kwa sababu tiba wanazopitia siyo nyepesi na zinaandamana na kupata maumivu makali na shida mbalimbali.

“Hata baada ya tiba kuna athari ambazo huwa zinajitokeza na kuzidi kumweka mgonjwa katika wakati mgumu kama vile kunyonyoka nywele, uchovu na changamoto mbalimbali za kimaisha. “Kwa sababu hiyo SCF inajaribu kuona ni njia zipi wazitumie ili kumpunguzia shujaa huyu wa saratani madhila yanayomwandama wakati wa tiba na hata baada ya kumaliza.

“Lengo ni kuwafanya mashujaa wa saratani waweze kuendelea kuishi maisha bora, yenye utulivu, amani na hata kutimiza ndoto ambazo mtu alikuwa amejiwekea kabla hajaanza kuugua saratani. “Huu ni mkakakati wa kuwafanya mashujaa wa saratani wajiamini na kujiona kwamba kuugua saratani siyo mwisho wa maisha wala kushindwa kutimiza malengo na ndoto zao za kimaisha.

“Kwa sababu hiyo, SCF inajaribu kukaa na mmoja mmoja au katika vikundi ili kuwasikiliza na kuwashauri namna ya kupata suluhisho.”

Saratani ni nini? Mkurugenzi wa Tiba ORCI, Dk Mark Mseti anasema saratani ni ugonjwa unajumuisha magonjwa mengi ambayo yanafanana kwa kuwa na sifa mbili kubwa: “Kwanza kuna chembechembe hai za mwili zinazozaliana kwa haraka bila udhibiti. Pili chembechembe hizo zinaweza kusafiri ndani ya mwili na kwenda kuzaliana eneo jingine.

“Seli za kawaida haziwezi kufanya hivyo, mfano ukichukua seli za ulimi ukiziweka kwenye mkono haziwezi kuendelea kuishi. Lakini seli ya saratani popote utakapoiweka inaweza kuendelea kuishi na kuzaliana.” Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasoambukiza (TANCDA), Profesa Andrew Swai anasema zipo dalili mbalimbali za saratani lakini jambo la msingi ni kuchunguzwa hospitalini ili kuzibaini.

Anasema magonjwa ya saratani hutibika na kupona kiwepesi, bila kuchukua muda mrefu iwapo yatabainika mapema. Baadhi ya dalili za saratani, anazitaja kuwa ni kukosa hamu ya kula, kupungua uzito bila sababu, uchovu bila kufanya kazi na uvimbe wa zaidi ya wiki tatu shingoni, kwapani, tumboni, kwenye ngozi au via vya uzazi.

Dalili nyingine anazitaja kuwa ni kubadilika kwa kawaida ya kupata choo (kufunga choo), kutokwa na ute, majimaji au usaha ukeni, kutokwa na damu kwenye choo, mkojo, makohozi au puani. Kwa wanawake ni kutokwa damu ukeni baada ya tendo la ndoa, baada ya kukoma mzunguko wa hedhi au nje ya mzunguko wa hedhi.

Profesa Swai anasema dalili nyingine ni shida au maumivu wakati wa kumeza chakula au vinywaji, kukohoa au sauti ya kukwaruza kwa zaidi ya wiki tatu, matiti kubadilika umbile, uvimbe, ngozi au kutoa majimaji. “Hisia za saratani pia zinaweza kuwa ni ile hali ya kukojoa mara nyingi zaidi ya kawaida au mkojo kutoka kwa shida,” anasema Profesa Swai.

Kwa kuwa dalili za awali haziambatani na maumivu, Profesa Swai anasema husababisha wagonjwa wengi kuchelewa kwenda kutafuta matibabu. Kwa sababu hiyo anashauri jamii kujijengea utaratibu wa kujichunguza ugonjwa wa saratani angalau mara moja kila baada ya miaka miwili.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/272909934f6e949d6764f7bbaddd8372.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Leon Bahati

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi