loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mwanza na kampeni ya kumfanya mtoto wa kike asikose shuleni

Mwanza na kampeni ya kumfanya mtoto wa kike asikose shuleni

WAHENGA wanasema ukimwelimisha mtoto wa kike unaelimisha jamii nzima lakini ukielimisha mtoto wa kiume unaelimisha mtu mmoja.

Waarabu pia wana msemo wao kwamba al-ummu madrasa wakimaanisha “mama ni shule’ na hivyo ili awe shule, mtoto wa kike anahitaji sana kupata elimu. Hata hivyo, watoto wa kike wamekuwa wakikumbwa na changamoto mbalimbali wanapokuwa shuleni, hususani wale waliopevuka.

Moja ya changamoto ni namna ya kuendelea na masomo huku wakiwa katika hedhi. Ukiachana na tatizo la maji na vyoo wanakoweza kujihifadhi wanapongia kwenye hedhi, ukosefu wa taulo za usafi za kike limekuwa pia ni tatizo ambalo limekuwa likiwafanya baadhi yao kukosa masomo na kulazimika kukaa nyumbani.

Kwa kulijua tatizo hilo, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula hivi karibuni aliamua kusaidiana na wazazi katika kukabiliana na changamoto ya taulo za usafi, ili isiwe sababu ya watoto wa kike kukosa masomo.

Mabula alitoa msaada huo kwa kushirikiana na watumishi katika ofisi yake wakati wa kilele cha siku ya maadhimisho ya hedhi salama duniani yaliyokuwa na kauli mbiu isemayo: “Ni wakati wa kuchukua hatua kwa hedhi salama kwa watoto wa kike na wanawake.”

Alisema aliona ni jambo jema siku hiyo kuanzisha kampeni maalumu ya kugawa taulo hizo za kike katika jimbo lake inayojulikana “Keep girls in school with sanitary towels” inayomaanisha kuwafanya watoto wa kike wabaki shuleni kwa kuwapa taulo za usafi.

Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa taulo hizo kwa wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Igogo, jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Tàasisi ya Wanawake na Hatamu, Flora Magabe ambaye pia ni mratibu wa kampeni hiyo na Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, anasema kampeni hiyo imelenga kuwafikia watoto wa kike 50,000.

Anasema pamoja na kugawiwa taulo za usafi lakini pia wanapewa elimu ya hedhi salama na uhifadhi wa mazingira kwa upandaji miti.

“Hii kampeni ni ya miaka minne (2021-2025) na inawalenga zaidi watoto wa kike walio kwenye mazingira magumu wanaosoma shule za msingi na sekondari katika halmashauri ya jiji la Mwanza,” anasema Magabe na kuongeza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya pili ya mradi wenye lengo la kuhakikisha mtoto wa kike anakuwa na mazingira rafiki na salama ya kusomea shuleni akifuata ratiba ya masomo yake.

Magabe anaongeza kuwa kampeni hiyo inatarajiwa pia kuzifikia shule 30 za halmashauri ya jiji la Mwanza zenye walengwa 3,611. “Naomba pia wadau mbalimbali wa maendeleo wajitokeze kwenye kampeni hii ili tuweze kumnusuru mtoto wa kike dhidi ya changamoto ya hedhi,” anasema Magabe.

Anaongeza: “Elimu kwa mtoto wa kike ni jambo la msingi katika jitihada za kumletea maendeleo yeye mwenyewe na kwa nchi yake kwa sababu mafanikio ya mwanamke kwa upande wa elimu yana faida ya muda mrefu.” Magabe anatamani kampeni hiyo iigwe na kusambaa hadi vijijini kwa maelezo kwamba uhaba wa taulo za kike pengine ni tatizo kubwa zaidi vijijini kulinganisha na mijini.

Anasema kimsingi wazazi wengi hawana uwezo wa kuwanunulia mabinti zao taulo hizo, hali ambayo huwapa wakati mgumu na hivyo kulazimika kukosa masomo.

Anasema wasichana wengi wanapokuwa kwenye kipindi cha hedhi, hujawa na woga ambapo huhofia kupoteza thamani yao na utu wao hasa wawapo shuleni au mbele za watu na ndio sababu ya kuamua kutohudhuria darasani na jibu lake ni kuwapa taulo za usafi.

Anasema ni kutokana na hali hiyo, Mbunge wa Nyamagana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wamejitoa kwa kugawa taulo za usafi kwa wasichana 50,000 kwa shule za msingi na sekondari 30 katika halmashauri ya jiji la Mwanza. Anasema katika kuhakikisha jamii inamthamini mtoto wa kike, taasisi yake na ofisi ya mbunge watafanya kila linalowezekana ili kuelimisha jamii juu ya thamani ya utu kwa mtoto wa kike.

Magabe anaamini kwamba tatizo la usafi wakati wa hedhi limekuwa likichangia watoto wengi wa kike kufanya vibaya darasani kulinganisha na wenzao wa kiume na hivyo kuchangia katika kushindwa kutimiza ndoto zao. “Ni jukumu la jamii kuhakikisha mtoto wa kike habaguliwi na apewe fursa ya kupatiwa elimu kama ilivyo kwa mtoto wa kiume, kwani watoto wote wana haki sawa katika jamii,” anasema.

Kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi na Mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa (Elimu ya watu wazima) Mwalimu Sheja Josephat kwenye kilele cha maadhimisho ya hedhi salama duniani yaliyofikia kilele chake Mei 28. Maadhimisho hayo alifanyikia katika Shule ya Sekondari Igogo, iliyoko katika Kata ya Igogo wilayani Nyamagana.

Josephat anasema hatua ya mbunge wa jimbo hilo kugawa taulo za usafi bure na kuanzisha kampeni hiyo ni jambo la kupongezwa na kwamba ni kiongozi anayejitambua na aliyeamua kuacha alama ya kukumbukwa katika jamii.

Anawapongeza wadau wengine wa maendeleo, ukiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Tàasisi ya Haki Zetu Tanzania Organization pamoja na ile ya Wanawake na Hatamu kuwa sehemu ya kushiriki katika hatua ya kutoa taulo hizo za kike alizoziita ‘baraka kwa msichana’.

Sheja anasema serikali mkoani Mwanza imechukua hatua mbalimbali za kujenga mazingira rafiki na salama kwa mtoto wa kike ili asikie fahari akiwa katika hedhi kwa kuanza kutekeleza miradi mbalimbali inayohakikisha kila shule inapojenga vyoo kunakuwa na chumba maalumu cha mtoto wa kike ili aweze kupata fursa ya kujisetiri vyema.

Anatoa rai kwa wazazi na walezi jijini Mwanza kuhakikisha kuwa wanawajibika na kuhakikisha kuwa watoto wao wa kike wanapata taulo za kike wanapokuwa kwenye hedhi badala ya kudhani ni suala la aibu na kwamba watoto na wazazi hawapaswi kushirikishana katika hilo.

Mwakilishi wa Mbunge, Ahmed Misanga anasema uzinduzi wa kampeni hiyo ni jitihada ya Mbunge Mabula katika kuboresha mazingira ya kujifunzia ya mtoto wa kike na kwamba wengi wakiunga mkono juhudi hizo zitaongeza ufaulu wao katika masomo.

“Katika awamu ya kwanza ya ugawaji taulo za kike 2017-2020 tuliwafikia zaidi ya wanafunzi 10,000 ambapo awamu ya pili ya mradi huu tumelenga kuwafikia watoto wote wa kike katika shule za kutwa na bweni nyingi zaidi. Mbunge wetu anataka wanafunzi wa kike wasome bila bughudha wakati wa hedhi,” anasema Misanga Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki Zetu Tanzania Organization, Gervas Evodius anasema taasisi yake imewiwa kuunga mkono kampeni hiyo kwani ina nia njema kwa maendeleo ya mtoto wa kike.

Anasema kutokana na kukosa taulo za kike, kwa mwaka mtoto wa kike huwa katika hatari ya kukosa masomo kwa siku kati ya 36 na 48 kwa mwaka.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/23f79119290474506e5caeb256c1958a.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi