loader
Dstv Habarileo  Mobile
VIWANDA VIDOGO NA BIASHARA NDOGO: Sekta inayofariji na kujibu changamoto za kiuchumi

VIWANDA VIDOGO NA BIASHARA NDOGO: Sekta inayofariji na kujibu changamoto za kiuchumi

“SEKTA hii (viwanda vidogo na biashara ndogo) inatoa faraja kwa sababu kila palipo na viwanda vidogo na biashara ndogo, lazima panambatana na ajira na ongezeko la vipato kwa wananchi.”

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashir Abdallah, anasema hayo anapozungumzia umuhimu wa sekta binafsi katika uchumi wa nchi wakati akifungua warsha ya siku moja kwa wadau kujadili ‘Mwelekeo wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo’ nchini.

Mkurugenzi wa Maendeleo wa Idara ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Consolatha Ishebabi, anasema hiyo ni rasimu ya mwisho kwa ajili ya mapendekezo.

Katika ufunguzi huo wiki iliyopita Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu, Abdallah anasema Serikali inatambua na kuthamini umuhimu wa sekta binafsi hususan thamani ya uendelezaji wajasiriamali katika shughuli za uchumi ndio maana hata sera za nchi zimeweka bayana nafasi na jukumu la sekta binafsi katika shughuli za moja kwa moja za uzalishaji na kufanya biashara.

Anasema hiyo ndio sababu kubwa ya Serikali kuendelea kubaki na jukumu kuu la kujenga mazingira rafiki na wezeshi kwa sekta binafsi kuendelea kuwa injini ya uchumi wa nchi.

“Dira ya Taifa 2025, Ilani ya CCM ya 2020 -2025 na Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano wa Maendeleo, pamoja na mambo mengine inatilia mkazo kuishirikisha ipasavyo sekta binafsi katika kuendeleza au kukuza jasiriamali katika kukuza biashara zinazochochea mauzo ya nje ili kuleta uwiano wa maendeleo,” anasema Dk Abadallah.

Anaongeza: “Nawapongeza na kuwashukuru viongozi wetu wa taifa hususan Rais Samia Suluhu, Makamu wa Rais, Dk Isidory Mpango na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa nafasi tofauti kutilia mkazo uendelezaji wa uchumi kwa kuzipa nafasi na msukumo wa kipekee shughuli za maendeleo ujasiriamali.”

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu, Abdallah, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, pia ameweka suala la uendelezaji ujasiriamali na ujenzi wa uwezo wa taasisi zake kuwa kati ya vipaumbele katika Mpango na Bajeti ya Mwaka 2021/2022.

Anasema kwa kuwa serikali inafanya juhudi kuwezesha Tanzania kufikia hatua ya kati ya uchumi wa kati ambao imeufikia, sekta hii inayojumuisha pia sekta ya viwanda, iwe nguzo kuu katika safari kuelekea hatua hiyo kwani ni mtambuka na inahusisha sekta zote zinazojihusisha na shughuli za kiuchumi.

Sekta hii ya viwanda vidogo na biashara ndogo ndio inayowezesha karibu kila mwananchi anayejitoa kushiriki shughuli za kiuchumi katika sekta yoyote.

Dk Abdallah anasema: “Uzoefu umeonesha kuwa, sekta hii imeziwezesha nchi nyingi duniani kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kwa sababu haibagui wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo hasa kufuatia ukweli kuwa, wananchi wengi wanamudu mitaji na ujuzi unaohitajika kuingia katika shughuli za kiuchumi chini ya sekta hii.”

Uchunguzi wa kihabari umebaini kuwa, baadhi ya shughuli katika sekta hii ni pamoja na uzalishaji viwandani na minyororo yake ya thamani, huduma za usafirishaji, uwindaji, mahoteli, bima, ushauri, fedha na maduka ya rejereja na jumla. Imebainika kuwa, katika mlolongo wote huo, kuna mamilioni ya watu walioajiriwa moja kwa moja na wengine wanachagizika kwenda kujiajiri.

Takwimu kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara zinaonesha kuwa, sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo ina zaidi ya jasiriamali milioni 4.5. Kwa sasa na imewezesha ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya Watanzania milioni 8. “Bahati nzuri zaidi, sekta hii ndio inayobeba takribani asilimia 98 ya viwanda vyote nchini,” anasema Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biasha, Dk Abdallah.

Anaongeza: “Hili ni jambo la faraja kubwa kwa kuwa malighafi za nchi yetu hasa za wakulima zinapata masoko katika viwanda hivyo hasa ikizingatiwa kuwa, viwanda vya sekta hii vimesambaa nchini kote na vingi vikijihusisha katika uongezaji thamani hasa wa mazao ya kilimo.”

Ndio maana anasisitiza: “Kimsingi, sekta hii ni muhimu sana kwa taifa na sera yake inabidi iwe nzuri ili ipate nafasi nzuri zaidi katika kujenga uchumi wa nchi yetu.”

Anaongeza: “Kupitia sekta hii, naamini tunaweza kujimudu kama nchi na kujitosheleza katika mahitaji yetu na hivyo kuweza kuokoa fedha nyingi za kigeni tunazotumia kuagiza bidhaa za kawaida kama mafuta ya kula nje ya nchi wakati tuna ardhi ya kutosha na yenye rutuba ya kuzalisha malighafi, kuongeza uzalishaji na kuanza kuwauzia watu wa nje sambamba na kutatua kilio kikubwa cha vijana wetu ambacho ni ajira.”

Mintarafu suala hili, Mkurugenzi Mkuu wa Uendeshaji kutoka Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Huduma za Fedha (FSDT), Irene Madeje, anasema takwimu za hivi karibuni zinaonesha viwanda vidogo na biashara ndogo nchini huchangia takriban asilimia 35 ya pato la taifa.

“Ukuaji katika uchangiaji pato la taifa, ongezeko la ajira na ongezeko la jumla la miradi ya ujasiriamali ni matokeo ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo ya Mwaka 2003,” anasema. Madeje anasisitiza: “Tutaendelea kushirikiana na serikali na sekta binafsi kusaidia ukuaji wa miradi hii na kuongeza ushiriki wa wakulima, vijana na wanawake kwa kuongeza thamani katika shughuli za kiuchumi.”

Katika warsha hiyo ya kujadili “Mwelekeo wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo,” Naibu Katibu Mkuu huyo anasema: “Kwa kutambua fursa na umuhimu wa sekta hii katika taifa, wizara kwa kuzingatia mahitaji ya wakati ya sekta imeamua kufanya mapitio ya sera hii ili ibebe kikamilifu matarajio ya sekta katika taifa kwa sasa na baadae.”

Anasema wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ilianza mchakato huo kwa kufanya uchambuzi yakinikifu kwa tathmini ya kina ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo ya Mwaka 2003 ili kuona kama bado inakidhi matarajio ya umma kwa sekta kama nchi.

“Tathmini hiyo ilitujulisha kuwa, sera inabidi ifanyiwe mapitio kwa kuwa kulikuwa na mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii ambayo yamejitokeza na hivyo, yalihitaji kuwekwa sawa kisera...,” alisema.

Maeneo hayo mahsusi yaliyojitokeza ni pamoja na udumavu wa miradi ya ujasiriamali na hivyo eneo la kuzikuza litahusishwa katika sera; ushiriki kamilifu wa sekta mpya zilizojitokeza zikiwemo gesi, petroli, madini na sekta za ubunifu na kuangalia kwa kina suala la uanzishwaji viwanda vijijini kwa mtazamo wa uchumi wa viwanda.

Mengine ni ushiriki wa vijana katika sekta hasa ikizingatiwa kuwa takribani asimia 60 ya Watanzania ni vijana, na kuweka vyema sekta ili itumie kikamilifu fursa za masoko zinazotokana na makubaliano mbalimbali yanayofanywa na serikali kikanda na kimataifa.

Naibu katibu mkuu anawambia washiriki wa warsha: “Maeneo hayo yote na yale ya awali yaliyoko katika sera yanahitaji uchambuzi makini ili yalete tija katika sekta.” “Pia, muitazame kwa kina tafsiri ya sekta na mtoe maoni kwa weledi na kwa kuzingatia uhalisia wa mazingira ya sasa na ya wakati ujao... Tukumbuke sekta hii ikifanya vizuri, nchi yetu itaweza kujitegemea kimapato na ajira.”

Anakwenda mbali na kusema: “Serikali inapenda kuona nchi haiendelei kuhamisha ajira na mapato ya kodi kwa kuagiza bidhaa zilizoongezwa thamani kutoka nje ya nchi baada ya kuwapa malighafi tunayoizalisha wenyewe.” Anawataka Watanzania kujenga na kuimarisha utamaduni wa kula (kutumia) wanavyozalisha na kuzalisha wanavyotumia hivyo, kuimarisha soko la ndani ambalo ni ‘mtaji mkubwa” na kuongeza pato la taifa.

Naibu Katibu Mkuu, Abdallah anawahakikishia: “Mimi si mvivu wa kusoma; niwaahidi kuyasoma mapendekezo yenu yote mtakayoyajadili leo na kuyafuatilia katika sera inayoandaliwa...”

Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo aliyekataa jina lake lisitajwe gazetini, anasema katika hatua zilizobaki wadau wa ngazi zote husika waendelee kutazama kwa kina mambo mazuri na upungufu sambamba na tafsiri ya sekta na pia, watoe maoni kwa weledi wakizingatia uhalisia wa mazingira yaliyopo na wakati ujao ili kuiboresha.

Anasema: “Hili litawasaidia Watanzania kufanya vyema zaidi shughuli za kiuchumi ili Tanzania ijitegemee kwa mapato na ajira na hivyo, mapitio ya Sera Maendeleo ya Viwanda Vidogo, Biashara Ndogo yanahitaji kufanyika kwa umakini.”

Mratibu wa Mabaraza ya Kukuza Ujuzi ya Kisekta katika Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Jane Gonsalues, anasema wadau wa sekta binafsi wanaisubiri kwa hamu sera hiyo huku wakitambua ukweli kuwa, sekta binafsi ndio injini ya uchumi wa taifa.

“Bila sekta hii, hatuwezi kupatata maendeleo na tunashukuru juhudi za wizara katika kufanikisha upatikanaji wake ili iwe yenye msaada na manufaa kwa wafanyabiashara ndogo, wenye viwanda dogo na Watanzania kwa jumla,” alisema Gonsalues.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/7b8e36e547b6be77460e0ba00a995183.JPG

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi