loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tumeiacha asili yetu ya Uafrika

Tumeiacha asili yetu ya Uafrika

MTU yeyote akijaribu kuitafuta asilia ya Afrika kabla ya ukoloni atakutana na ukakasi mkubwa.

Ukakasi huo unasababishwa na ukweli kwamba historia ya asilia ya Mwafrika imeandikwa na mkoloni yaani beberu ambaye maandishi yote hulenga kuonesha mwafrika ni kiumbe dhaifu. Hulionesha Bara la Afrika kama lilikuwa gizani kabla ya kuja kwa mkoloni. Swali la kujiuliza ni inawezekanaje bara ambalo watu waliishi miaka zaidi ya milioni mbili kuwa bara la giza?

Je, inawezekana asili hii iliyoandikwa na mkoloni ilikuwa na lengo la kufuta uwezo wa kufikiri (brainwash) wa Mwafrika kwa kutumia asili yake ili iwe rahisi kuendelea kutawaliwa milele yote? Kuna mtu aliwahi kuniambia jambo, kwamba hakuna kitu kinachofanyika kwa bahati mbaya duniani bali huwa na hesabu yake hata kabla hakijafanyika.

Wadadisi wa mambo wanaonesha kwamba hata kabla ya kuja kwa mkoloni Afrika ilikuwa imeendelea sana zaidi hata ya Ulaya na Amerika.

Mfano mzuri unaoneshwa kupitia mapiramidi ya Misri na ufuaji wa chuma uliokuwa unaendelea Afrika. Aidha wadadisi hawa wanaonesha kwamba Mwafrika ndiye alikuwa wa kwanza kuendelea katika kila sekta, ikiwemo kilimo, biashara, siasa ya utawala na nyinginezo.

Mfumo wa kiutawala uliokuwepo kabla ya ukoloni inaonesha ulikuwa bora sana kuliko mfumo wa utawala ulioletwa na ukoloni. Mfumo wa kuishi kabla ya ukoloni ulikuwa rafiki kwa asili ya Waafrika wenyewe. Mfumo wa ulaji wa vyakua asili na utumiaji wa dawa za asili ya Mwafrika ulifanya watu waishi pasi na shaka yoyote tena kwa miaka mingi.

Biashara ya utumwa ililichachafya sana bara hilo. Iliondoa nguvu kazi iliyokuwa muhimu kwa mstakabali wake badala yake ikaleta hofu ambayo ilipunguza kiwango cha kufikiri kwa wana asilia wa Afrika. Mpenzi msomaji lengo langu siyo kukukumbusha historia ya Afrika wala kuongeza machungu ya ukoloni bali kuikumbusha jamii ya Afrika kwamba tunaweza kujitegemea pasipo mkoloni iwapo tutakubali asili yetu.

Kifungu cha 84, vifungu vidogo vya (c, d) cha Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025 navinukuu: 84(c) Kuimarisha na kujenga uwezo na utafiti kuhusu magonjwa ya mlipuko katika taasisi ya NIMR, vyuo vikuu na taasisi nyingine za utafiti nchini. 84(d) Kuanzisha kituo kikubwa cha utafiti na uchunguzi wa mimea dawa na kuanzisha kiwanda cha kimkakati cha kuzalisha dawa zitokanazo na mimea yetu.

Mei 12 mwaka huu (2021) baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alieleza kwamba moja ya mambo ambayo nchi yake itafanya ni kuanzisha kiwanda cha chanjo zao za kupambana na magonjwa ya mlipuko. Kiwanda ambacho kitabeba maono ya waganda wenyewe.

Lakini alibainisha kwamba alipoonesha nia yake hiyo ya kutengeneza chanjo au dawa nchini mwake, wakubwa walimuuliza anatengeneza za nini? Maana kazi ya Mwafrika ni kusubiri wao watengeneze kisha tuletewe! Hili jambo alionesha kutopendezwa nalo hata kidogo.

Kwa namna moja au nyinge kizazi cha miaka ya kabla ya 90 ambapo dawa za kibeberu zilianza kushamiri, kiliishi kwa kutumia miti shamba. Mimea hii asilia iliwatibu dhidi ya magonjwa yote na kuwafanya kuishi kwa amani kabisa. Nchi kama China, Korea na nyinginezo pamoja na kutumia dawa za kisasa, wanaheshimu na kutumia dawa za asili kuliko za kigeni.

Swali ni kwanini wanafanya hivyo? Je, ni kulinda asili na utamaduni wao? Je, ni kuonesha kwamba dawa zao zina nguvu kuzidi za kibeberu? Mwanzoni wakati ugonjwa wa Covid-19 unaanza baadhi ya mataifa ya Afrika yalijitokeza hadharani na kutangaza kuwa na dawa za ugonjwa huo.

Inawezekana kwa namna moja au nyingine Shirika la Afya Duniani (WHO) halikuafikiana na mataifa hayo kwa kuwa pengine labda walikuwa hawafaidi kupitia hilo. Lakini je, ni kweli kwamba dawa hizi hazitibu? Je, WHO walijishughulisha kufanya utafiti wa kuona ubora wa dawa hizi? Au hawakujali kwa vile vimetokea Afrika?

Wote tutakubaliana kwamba Afrika ina mimea asilia ambayo Mungu mwenyewe aliiotesha kwa lengo la kuwaokoa watu weusi. Maandiko yanaonesha kwamba wana wa Israel walitumia mimea kwa ajili ya tiba kwa maelekezo ya Mungu. Mimea hiyo hiyo iliendelea kutumika kati ya kizazi na kizazi. Pengine, ndiyo sababu wasabato huamini zaidi kwenye asili kuliko ukisasa? Itakuaje iwapo tutajifanya kutoheshimu asili yetu?

Ni ugonjwa upi ambao mabibi na mababu zetu wangeshindwa kuzuia kwa kutumia mimea? Au vile tumelowea kwenye ukisasa tunaacha asili yetu? Inawezekana CCM iliona hili na ndiyo maana kwenye Ilani yake ya 2020-2025 inabainisha wazi kabisa umuhimu wa kutumia mimea tiba kwa ajili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Cha msingi ni kuifanyia utafiti zaidi na kuboresha viwango vya utumiaji wake. Swali ni je, ni kwa kiasi gani kifungu hiki kimezingatiwa? Ni kwa kiasi gani tumewekeza katika kufanikisha hili? Je, ni nani atafanikisha hili na lini atafanya hivyo? Je, ni kwa kiasi gani chama kimejipanga kushauri mataifa mengine ya Afrika kubeba dhana hii? Je, watatuelewa? Watatuelewaje iwapo Afrika haizungumzi lugha moja?

Niliumia sana siku za hivi karibuni nilipoona kwenye mitandao ya kijamii madai kwamba nchi ya Uganda ilikuwa inazika majeneza matupu kwa kisingizio cha Covid-19 ili tu wapate mikopo ya mabeberu yenye riba nafuu!

Kama ni kweli, inasikitisha na kudhalilisha. Pengine iwe ni igizo. Ya nini kujidhalilisha Waafrika? Kwanini tusitumie asili yetu kujiganga wenyewe na kuitetea pasi aibu? Ni lini tutaacha kuabudu ubeberu? Tunakionesha nini kizazi kipya? Tunawafundisha nini viongozi wajao? Je, tunafanya haya yote kwa ajili ya fedha?

Kwa miaka mingi tumeishi nje ya asili yetu, kuanzia kuvaa, chakula, kufikiri, elimu, mifumo ya utawala, utoaji wa maamuzi kwamba lazima tujue mabeberu wanataka nini, ndipo nasi tufanye kile kinachowafurahisha. Naamini Waafrika tuna kila kitu ndani ya bara letu. Kinachokosekana ni kubadili mfumo wa kufikiri na kujikubali wenyewe.

Nimalizie kwa maneno aliyoyasema Patrice Lumumba mnamo Machi, 1959 katika Chuo Kikuu cha Ibadan, Nigeria; kwamba “Afrika tuamke! Afrika tuungane! Afrika twende mkono kwa mkono katika kulifanya bara letu huru na lenye haki”. Pasipo kufanya hivyo kama Waafrika tutakuwa tumewasaliti waliopigania uhuru wetu na haitakuwa haki kwao na vizazi vijavyo.

Inatosha sasa kushiriki kwenye vita ya mabeberu ambavyo tunajiumiza wenyewe kwa kuwaruhusu watuendeshe na kutupangia namna ya kuishi. Mungu Ibariki Afrika.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/fedf7ad6f7f39189613918ac0431c128.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Felix Lugeiyamu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi