loader
Dstv Habarileo  Mobile
SIKU YA WAJANE DUNIANI:  Serikali isikie kilio cha wajane kuhusu Sera

SIKU YA WAJANE DUNIANI: Serikali isikie kilio cha wajane kuhusu Sera

LEO ni Siku ya Kimataifa ya Wajane, ambayo mataifa duniani kote yanatambua vurugu, ubaguzi na unyanyapaaji unaofanywa dhidi ya wajane na kusherehekea mchango muhimu wa wajane.

Siku hii huadhimishwa kila Juni 23 ya kila mwaka. Ni siku ambayo serikali zote ikiwemo ya Tanzania zinatakiwa kuchukua hatua za makusudi kulinda haki za wajane.

Katika siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres anamtaka kila mtu kutafakari “changamoto za kiuchumi na matatizo wanayopitia wajane na kuhakikisha kwamba hawaachwi nyuma”.

Katibu Mkuu anasema hakuna mwanamke anapaswa kupoteza hadhi, utu, ustawi au kipato chake eti kwa sababu amefiwa na mumewe.

Na kwamba, suala hilo ni dhahiri lakini bado mamilioni ya wanawake duniani wanakumbwa na manyanyaso, ukatili na hata kuenguliwa kwenye urithi wa mali pindi wanapofiwa na waume wao.

Anatolea mfano suala la wanawake kuchomwa moto au kurithiwa na ndugu wa waume wao kwa fikra potofu ya kuwatakasa akisema kuwa mila hiyo inachukiza, imepitwa na wakati na inaongeza uwezekano wa mjane kuambukizwa HIV.

Katibu Mkuu anasema athari hizo zinagusa pia watoto wa mjane pamoja na ndugu wanaotemtegemea. Na ni jukumu la kila mtu kulinda haki za binadamu na utu wa wajane kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa kutokomeza ubaguzi dhidi ya wanawake na ule wa haki za mtoto.

Anamalizia kwa kusema kuwa katika siku hii ya leo ni vyema kila mtu kuahidi kuchukua hatua thabiti kuwezesha wanawake, kuendeleza usawa wa kijinsia na kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Umoja wa Mataifa unaonesha kuwa kati ya asilimia 7 na 16 ya wanawake wote duniani ni wajane.  

Na hivyo, jamii imetakiwa kuendeleza mipango na kuongeza juhudi zaidi katika kukabiliana na vitendo vya ukatili, unyanyasaji na kuwainua wajane ili wapate uwezo wa kiuchumi wa kuzihudumia familia na wategemezi wao kwa kuwa ndio muhimili pekee wa familia iliyoachwa.

Siku ya kimataifa ya wajane ilibuniwa mwaka 2005 kupitia usaidizi wa wakfu wa Loomba na kutambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa mwaka 2010.

Wakfu wa Loomba ulibuniwa mwaka 1997 na Lord Raj Loomba kama njia ya kumkumbuka mamake ambaye alibaki mjane akiwa na umri wa miaka 37 eneo la Punjab nchini India.

Wakfu huo unalenga kuwaelimisha watoto wa wajane masikini na kuwainua wajane kote duniani. Tangu kubuniwa kwa siku ya wajane duniani wakfu huo umewaelimisha maelfu ya watoto wa wajane masikini na kuwasaidia zaidi ya watu 27,000 wa familia zao.

Katika kuadhimisha siku hii, mwaka 2019 wajane nchini waliiomba serikali kuandaa Sera ya Taifa itakayowatambua kama kundi maalumu katika jamii ili haki zao ziweze kulindwa.

Walitoa kauli hiyo wakati wa maandamano yaliyohitimisha maadhimisho ya siku hii yaliyofanyika katika Uwanja wa Nyerere Jijini Dodoma.

Walisema kuanzishwa kwa sera ya taifa kwa ajili ya wajane kutasaidia kutoa msukumo kwa jamii juu ya haki na madhila wanayopitia wajane na kwamba kundi hilo limekuwa likidhulumiwa mali pindi wenzi wao wanapofariki.

Mwaka 2015 yalifanyika maamuzi ya kihistoria ambapo Kamati ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia haki za wanawake iligundua ukiukwaji wa haki za wajane uliofanywa na Serikali ya Tanzania.

Wajane wawili, waliofungua majalada ya kesi kwa majina ya E.S na S.C, walipeleka kesi zao Umoja wa Mataifa baada ya mahakama za Tanzania kukataa madai yao ya haki sawa katika kurithi na kusimamia mali.

Kamati ya Umoja wa Mataifa iligundua matatizo kadhaa kwa wanawake hawa na katika mfumo mzima wa sheria za Tanzania. Hata hivyo, Tanzania iliahidi kurekebisha matatizo hayo.

Mume wa E.S alifariki dunia mwaka 1999. Shemeji yake alimfukuza nyumbani na kumlazimisha yeye na watoto wake wadogo watatu kuhamia kwa wazazi wake.

S.C na mwanawe mchanga waliachwa katika hali kama hiyo baada ya mumewe kufariki dunia mwaka 2000 na wakwe zake kuchukua nyumba na mali nyingine.

Chini ya sheria za kimila katika Mkoa wa Shinyanga ambapo wanawake hawa walikuwa wanaishi, wajane hawana haki ya kurithi kutoka kwa waume wao kama kuna mtoto wa kiume au ndugu wa damu wa mume.

Sheria za kimila katika mkoa huo ambazo zilisimikwa mwaka 1963, zinaeleza kwamba mjane “hana mgao wa mirathi kama marehemu ameacha ndugu wa ukoo wake; mgao wake husimamiwa na wanawe kama anavyowatunza.”

Sheria za kimila humtaka mrithi wa marehemu kumtunza mjane, lakini kiuhalisia, ndugu wa marehemu humfukuza mjane katika ardhi yao.

Sheria za kimila pia huzuia wajane kusimamia mali zisizohamishika: husema kwamba mali hizo lazima zisimamiwe na kaka mkubwa wa marehemu, baba au ndugu wa kiume, au dada pale ambapo hakuna ndugu wa kiume.

Hakuna mwanamke ambaye anaweza kurithi au kumiliki ardhi ya ukoo, ikiwa ni pamoja na wajane. Hali ni tofauti kwa wanaume, ingawa sheria za kimila zinatoa hisia kwamba mwanaume harithi kutoka kwa marehemu mkewe.

Tume ya Marekebisho ya Sheria Tanzania inadokeza kwamba mwanaume hana haja ya kurithi kwa sababu ya dhana ya kimila kwamba “mume pekee ndiye mwenye maslahi katika mali ambayo imepatikana kwa pamoja na wanandoa katika kipindi cha ndoa.”

Makala katika jarida la sheria juu ya mirathi Tanzania, inainukuu Tume ikisema kwamba dhana hii ndiyo inayosababisha kutokuwa na umuhimu wa kumteua mwanaume kuwa msimamizi wa mali au kugawa mirathi wakati wa kifo cha mke.

Mume hana haja ya kurithi. Mke anapofariki tayari mume humiliki kila kitu. Mume anapofariki, mke hamiliki chochote na hivyo huhitaji kurithi kwa hali na mali ili kuendelea na maisha.

Katiba ya Tanzania inatambua na kulinda haki za wanawake. Ibara ya 13 inatoa dhamana ya usawa wa wanawake chini ya sheria bila ubaguzi wa kijinsia, na ibara ya 107A (2) inatoa dhamana ya fidia kwa waathirika wa uvunjifu wa sheria. Kwa kuzingatia hayo, E.S na S.C walitafuta msaada katika mahakama za Tanzania.

Mahakama Kuu ilikuwa inatambua kwamba sheria za kimila zina ubaguzi dhidi ya wajane lakini hata hivyo ilikataa madai yao mwaka 2006. Mahakama ya Rufaa ilichukua miaka minne kusikiliza kesi na kisha kuitupilia mbali kwa sababu za kitaalamu.

E.S na S.C hawakukata tamaa. Wakiwakilishwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake Tanzania, na Kliniki ya Kimataifa ya Haki za Wanawake ya Chuo cha Sheria cha Georgetown, Washington DC, wajane hawa walifikisha kesi zao mbele ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake (Kamati ya CEDAW).

Katika maamuzi ya mwaka 2015, Kamati ya CEDAW iligundua kwamba Serikali ya Tanzania ilikiuka haki za wajane hawa kwa kuwanyima “usawa katika kurithi na kushindwa kuwapatia aina nyingine ya suluhisho.”

Pia iligundua kwamba mahakama za Tanzania zilikiuka haki za wajane hawa kupata haki za kisheria na fidia. Kamati ilipendekeza Serikali ya Tanzania kufidia wajane wote wawili kwa kukiuka haki zao na kutoa wito wa marekebisho ya Katiba na Sheria za Kimila na kuchukua hatua za vitendo kutokomeza ubaguzi wa aina hii.

Katika maadhimisho ya siku hii, namnukuu Annastazia Christopher Lwekila, mjane na mama mwenye watoto 5 anayeishi Kijiji cha Isoso kitongoji cha Karume, ambaye ameishi kwa zaidi ya miaka 6 bila mume wake na sasa anajishughulisha na ukulima na utengenezaji mapambo ya ndani.

Annastazia anasema kuwa wamekuwa wakikutana na changamoto za kutaka kurithiwa baada ya kufiwa na waume wao huku wajane wasio na watoto wakinyanyaswa na kufukuzwa kutokana na kuwa hawahesabiki katika familia ya upande wa mwanamume na anatoa wito kwa wanawake kujishughulisha na biashara na kuondokana na utegemezi.

“Hali ya kunyanyaswa ipo kwa baadhi kwani siku ya matanga anachaguliwa mtu wa kuilinda familia na baadaye anatumia zile mali vibaya na matokeo yake zikiisha basi anaondoka, na kwa wajane ambao hawakubahatika kuzaa yaani hawana thamani kabisa…” anasema Annastazia na kuongeza.

“Namshukuru Mungu sasa nina uwezo wa kujisimamia kiuchumi licha ya kuwa nina watoto wanaonitegemea, kutokana na ukulima ninaoufanya pamoja na ususi wa bidhaa mbalimbali za asili najipatia kipato mbali na kuwa sikuwa nikijishughulisha wakati mume wangu angali hai, ila nawashauri jamii iwapende na kuwathamini wajane lakini pia wanawake wafanye kazi hata kama bado wanawaume wao wapo maana kifo hakina hodi.”

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e2f041ff1733c0cfbc5ceb7036d83fc2.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi