loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tusipuuze hadhari dhidi ya corona

Tusipuuze hadhari dhidi ya corona

SIKU chache zilizopita, serikali ilitoa hadhari kwa umma ikiwataka kuchukua hatua dhidi ya ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19); huku ikisema upo uwezekano wa kutokea wimbi la tatu la maambukizi ya ugonjwa huo hapa nchini.

Katika tahadhari hiyo, imewataka wananchi wote kuchukua tahadhari za jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa juu ya hatua hizo ikiwemo uvaaji wa barakoa na kuepuka msongamano.

Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Dk Leonard Subi alitoa tahadhari hiyo kwa niaba ya serikali na kusisitiza hatua hizo zimetokana na ongezeko la maambukizi ya virusi hivyo, katika nchi za Afrika na nchi jirani na Tanzania.

Katika kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake, serikali ilizitaka taasisi zote binafsi na serikali, halmashauri na maafisa afya wanaotoa huduma mipakani kuendelea kuimarisha udhibiti wa magonjwa katika maeneo hayo kwa mujibu wa miongozo husika na kufuatilia magonjwa na matukio hatarishi kwa afya kwenye maeneo hayo.

Aidha, baada ya tahadhari hiyo ya serikali kutolewa, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuanzia jana imeweka utaratibu wa kujikinga na ugonjwa wa virusi vya corona ambapo watu wote wanaokwenda hospitalini hapo, wanatakiwa kuvaa  barakoa huku pia idadi ya wasindikizaji wa mgonjwa na wale wanaokwenda kuangalia wagonjwa ikipunguzwa.

Kadhalika, kwenye ofisi mbalimbali binafsi na za umma, utekelezaji wa agizo hilo unaendelea na kwamba nia hasa ni kuona wananchi wote wanafuata maelekezo hayo kwa sababu endapo kutatokea uzembe wa mmoja wetu, athari zake ni kubwa.

Ugonjwa wa corona ni hatari na kila mtu anapaswa kuelewa hivyo kwasababu unasambaa haraka na sio wote wenye miili yenye kinga imara inayoweza kupambana na virusi hivyo na kuvishinda na kwa sababu hiyo hatuna budi kufuata njia zote za kujikinga.

Katika Mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC), uliofunguliwa mjini Maputo,Msumbiji na Rais wa nchi hiyo , Filipe Nyusi ambaye sasa ndiye mwenyekiti wa jumuiya hiyo,alitoa mwito wa nchi hizo kushirikiana kupambana na janga hilo.

Katika hotuba yake, alisema hakuna serikali inayoweza kupambana peke yake katika janga la mlipuko wa virusi vya corona bila kusaidiana na wengine na ndiyo maana jumuiya hiyo imepitisha  maamuzi  ya jinsi ya kukabiliana na corona  kwa pamoja.

Kauli hiyo inatukumbusha umuhimu wa sisi zote kuungana na kuchukua tahadhari na kuwakinga wengine na tuhakikishe tunavaa barakoa tunapoenda kwenye misongamano pale kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.

Natoa mwito kwa watanzania tushikamane katika kujilinda na kuwalinda wengine dhidi ya corona na hata magonjwa mengine.

Sasa basi tuamke, tujue kuwa tishio la wimbi la tatu la corona liko na linatunyemelea, tusipuuze, tuvae barakoa kila inapobidi na tuzivae kwa usahihi tujue uzembe kidogo unaweza leta madhara makubwa  yenye maumivu makali .

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/61c0b2299a16604e2a79918012221eb2.png

TAARIFA za matukio ya mimba na ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi