loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wanyantuzu; Wasukuma wanaojua kuchakarika kutafuta mali

Wanyantuzu; Wasukuma wanaojua kuchakarika kutafuta mali

LEO katika mwendelezo wa makala za utamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali ya Tanzania, tunaangazia jamii ya Bhanantuzu (Wanyantuzu), mojawapo wa makundi ndani ya kabila la Wasukuma.

Wanyantuzu ni Wasukuma wenyeji wa Wilaya za Bariadi na Itilima mkoani Simiyu. Lakini kabla hatujaangalia kwa undani kuhusu jamii hii ya Wanyantuzu tuliangazie kwanza kabila lote la Wasukuma.

Msukuma ni mtu wa Kaskazini kwani jina “Wasukuma” lina maana ya watu wa Upande wa Kaskazini, lakini kabila la Wasukuma halimaanishi tu watu wa kaskazini bali wanajumuishwa pia watu wa Mashariki “Bhanakiya” (Mkoa wa Simiyu); Kusini “Bhadakama” (hawa wanaweza kuwa Shinyanga au Tabora kutegemea na mahali ulipo); na Magharibi “Bhanang’weli” (Mkoa wa Geita na sehemu ya Wilaya ya Kahama).

Wasukuma wamegawanyika katika pande kuu nne za dunia na jina la upande mmoja wa Kaskazini (Sukuma) ndiyo lililochukua nafasi ya pande zingine zote.

Kabila la Wasukuma linapatikana mikoa mitano ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Tabora japo Wanyamwezi asili ni wachache na wanachukua Wilaya ya Sikonge na Urambo, wilaya zingine za Igunga na Nzega ama mchanganyiko kama Uyui zinakaliwa na Wasukuma.

Wasukuma wengi pia wanapatikana katika Mikoa ya Rukwa, Mara, Katavi na Morogoro ambapo wamehamia huko kwa ajili ya kufuata kilimo na malisho ya mifugo. Hata hivyo, Msukuma wa Mwanza ndio hujiona yupo kaskazini hasa kuliko wote, kwa hiyo kuwaita waliopo Mkoa wa Shinyanga wa Kusini (Wadakama) hawezi kuwa amekosea.

Na ukiwa Shinyanga utawasikia watu wa Shinyanga wakisema wao wapo kaskazini hivyo ni Wasukuma na eneo la kusini (Mkoa wa Tabora) ndiko kuna Wadakama (Wanyamwezi). Usukumani hakuna kabila la Wanyamwezi bali wanaitwa Wadakama.

Japo ukifika Tabora Wilaya za Sikonge na Urambo ndiko hasa penye Wanyamwezi huku wilaya zingine zikiwa kwa kiasi kikubwa zimekaliwa na Wasukuma waliolowea toka Shinyanga na Mwanza miaka mingi iliyopita. Ni kama ilivyo upande wa Magharibi ambako kuna Bhanang’weli (Wasumva/ Wasumbwa).

Wasumbwa kama ilivyo kwa Wanyamwezi wao wanaonekana kama si sehemu ya Wasukuma lakini ni sehemu ya Wasukuma na karibu kila kitu kinafanana kuanzia lugha, mila na desturi, na utamaduni wao. Kwa kifupi, historia ya kabila la Wasukuma ni tata sana pengine ndiyo maana watafiti wengi wa mambo ya kale na wanahistoria wengi wanashindwa kuandika historia ya kabila hili kwa undani zaidi.

Hata wanaothubutu kuandika hukomea kuelezea tu kuhusu mila na desturi za Wasukuma pamoja na maeneo wanayopatikana na msambao wao. Wanyantuzu Sasa turudi kwenye hoja, Wasukuma wa Mashariki “Bhanakiya” (Wanyantuzu) ndio jamii ya Wasukuma waliotapakaa kila kona ya nchi hii.

Na pengine bila ya Wanyantuzu kabila la Wasukuma lisingekuwa linajulikana sana kwa namna linavyojulikana leo. Wanyantuzu wanajua sana kuchakarika katika kutafuta mali. Hawaogopi kitu na wala hawamwogopi mtu yeyote. Si unamfahamu Andrew Chenge? John Momose Cheyo? Au umepata kumsikia Danni Makanga? Kwa vyovyote mambo yao unayajua.

Hao ndio Banantuzu. Wanyantuzu ndio Wasukuma pekee wanaothubutu kwenda kupora ng’ombe za Wamasai. Wanyantuzu ni Wasukuma wenye dharau na mikogo mingi. Na kama unasikia watu wanaopenda sana utani na masihara, basi Wanyantuzu ni kiboko.

Hata ule usemi wa kwamba Wasukuma hupenda kuoa wanawake weupe basi huwahusu Wanyantuzu, kwani wanaume wa Kinyantuzu hupenda kuoa wake weupe. Kama mwanamke si mweupe basi lazima awe na sifa za ziada. Michepuko kwa mwanaume wa Kinyantuzu ni kitu cha kawaida sana.

Hata hivyo, katika makala haya suala la ni Msukuma wa wapi anaongoza kwa ushamba na ukilaza si lengo langu. Lugha ya Kinyantunzu (Ginantuzu) Kinyantuzu ni miongoni mwa lahaja zinazopatikana katika lugha ya Kisukuma. Lahaja hii kwa jina jingine inajulikana kama “Kimnakiiya”.

Kinyantuzu ni lahaja ya Kisukuma ambayo imetokana na mchanganyiko wa makabila mengi yanayozunguka Mkoa wa Simiyu ambayo yalifika katika eneo husika kwa malengo tofauti tofauti na kujikuta wameunda jamii iliyosheheni utajiri wa misamiati mingi kutoka kwenye makabila hayo.

Lahaja ya Kinyantuzu inazungumzwa mashariki mwa eneo la Usukumani katika Wilaya ya Bariadi, Itilima na baadhi ya maeneo ya Wilaya za Meatu, Maswa na Busega. Wapo waliofika katika eneo husika kwa ajili ya ufugaji, wengine walifika kwa ajili ya biashara na wengine walifika kwa malengo ya uwindaji.

Wapo pia waliofika kwa ajili ya utawala, wengine kwa ajili ya kilimo na wengine kwa ajili ya kusaka makazi salama kulingana na changamoto zilizowasibu huko kwao. Baadhi ya makabila hayo ni pamoja na Wamasai, Wataturu, Wanyiramba, Watindiga, Wanyaturu, Washashi, Wanyamwezi na Wasukuma.

Kisukuma cha lahaja ya Kinyantuzu hakina ‘shi’ bali hutumia ‘si’ kwa mfano, Wasukuma wengine hutamka shikolo (vitu) wao hutamka sikolo, au shiliwa (chakula) wao hutamka siliwa… Koo za Wanyantuzu Lahaja ya Kinyantuzu imeundwa na koo zipatazo 19.

Koo hizo ni Babinza (Minza), Babungu (Mungu), Bachama (Nchama), Banega (Nega), Bahunda (Ng’hunda), Baasi (Ng’wasi), Basaabi (Ng’wisabi), Bagolo (Ngolo), Bakamba (Nkamba), Bakela (Nkela), Bakwaya (Nkwaya), Bakwimba (Nkwimba), Basega (Nsega), Baselema (Nselema), Bashola (Nshola), Bashoma (Nshoma), Basiya (Nsiya), Balong’we (Long’we) na Bayemba (Nyemba).

Majina yote yaliyopo katika mabano ndio waanzilishi halali wa koo za Kinyantuzu ambapo majina haya yanabebwa na wanawake.

Hii inabainisha kuwa koo za Kinyantuzu ni za mama yaani mwanamke, na baba hana ukoo wowote. Hivyo, mfumo wa maisha katika koo za Kinyantuzu ni mfumo jike ikimaanisha kuwa mwanamke ndiye mlezi na mtawala wa familia na baba kazi yake ni kuzalisha na kutafuta kipato kitakachomudu kuiendesha familia yao.

Waanzilishi wa koo hizi kwa mujibu wa Wanyantuzu wenyewe ni kuwa, wanawake hawa walitoka sehemu na makabila mbalimbali ambao walifika katika eneo husika kwa malengo tofauti tofauti. Kwa hali hii katika koo za Kinyantuzu utasikia wanasema sisi asili yetu ni Wataturu, wengine wanasema sisi ni Washashi na wengine wanasema sisi ni Wanyanyembe.

Hii ndiyo maana lahaja hii ina misamiati mingi kuliko lahaja zingine za Kisukuma kwa sababu ya kukopa maneno mengi ya makabila mengine na hata majina ya asili ya watu wao yamechukua maana ya makabila yao. Majina ya asili ni majina ambayo chimbuko, historia na maana yake hutokana na vigezo, taratibu na kanuni zilizobeba maana kulingana na mila, desturi na utamaduni wa jamii husika.

Majina hayo hutolewa katika familia baada tu ya mtoto kuzaliwa na hutolewa kulingana na mila na desturi za jamii husika kwa kurithi kutoka kwenye majina ya ukoo, majina ya utani au matukio yaliyojitokeza katika jamii. Shughuli za koo za Kinyantuzu Koo za Kinyantuzu zinajishughulisha na shughuli mbalimbali kama vile shughuli za kiuchumi, kisiasa, kitaaluma, kijamii na kiutamaduni.

Shughuli hizi zote ni kwa ajili ya kupambana na maisha katika sehemu wanayoishi. Baadhi ya shughuli za kiutamaduni zinazofanyika katika koo za Kinyantuzu ni pamoja na kuabudu Mungu/ miungu na kucheza ngoma (maarufu kama mbina) ambazo zinahusisha uchezaji na uimbaji wa nyimbo kulingana na matukio yanayojitokeza katika jamii.

Na shughuli za kiuchumi zinazofanywa ni pamoja na kilimo cha mazao ya chakula na biashara (kama mahindi, mtama, mpunga, maharage, viazi vitamu, kunde, pamba, mihogo, ufuta, karanga, dengu, mbaazi, alizeti na choroko). Shughuli nyingine ni ufugaji wa wanyama (ng’ombe, mbuzi, kondoo, mbwa, paka, kuku, bata, njiwa na punda), uwindaji wanyama, uchimbaji madini, uvuvi na biashara mbalimbali.

Shughuli za kitaaluma zilizofanyika ni pamoja kufundishwa mbinu za kilimo, ufugaji na uendeshaji wa familia huku shughuli za kisiasa zinazofanywa ni pamoja na mambo ya utawala na uongozi katika jamii zao.

Kimsingi shughuli za kiuchumi, kisiasa, kitaaluma, kijamii na kiutamaduni huathiri uitaji, utoaji na utumiaji wa majina ya asili katika koo za Kinyantuzu kwa kiasi kikubwa kwani majina yaliyo mengi yanaakisi katika nyanja za kiuchumi na kiutamaduni na machache yanaakisi katika nyanja za kisiasa, kitaaluma na kijamii. Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au bhiluka@ gmail.com.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/006d453508a59f47520fb291833279c4.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi