loader
Siku 100 za Samia na umeme wa 27,000/-

Siku 100 za Samia na umeme wa 27,000/-

JANA Rais Samia Suluhu Hassan ametimiza siku 100 tangu alipoapishwa kuongoza nchi Machi 19, mwaka huu baada ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli kilichotokea Machi 17.

Katika kipindi cha uongozi wake, Rais Samia amedhihirisha kwa vitendo falsafa yake ya ‘Kazi Iendelee’ kwa kuendeleza mazuri ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo yeye pia alikuwa sehemu kupitia cheo cha Makamu wa Rais.

Katika kumulika siku 100 za uongozi wake na mantiki ya falsafa yake, hotuba yake ya Aprili 23 mwaka huu bungeni inadhihirisha pia kutimia kwa vitendo kutokana na mambo mbalimbali yanayofanyika ikiwamo usimamizi wa raslimali za nchi, utekelezaji miradi ya maendeleo na uwajibishaji katika utumishi wa umma .

Nanukuu sehemu ya hotuba yake:“…wanaodhani kwa usimamizi wa mali za umma, kusimamia ukwepaji wa kodi, kusimamia uzibaji wa mianya ya kupoteza mapato, kukemea uzembe na wizi, yameondoka kuendana na kuondoka kwa Mheshimiwa Hayati Dk Magufuli, nataka niseme hayati mpendwa wetu amekwenda peke yake.

Na kama nilivyosema siku ile, tunamsindikiza kwamba maono, falsafa na mikakati aliyotuachia, tunaendelea kuifanyia kazi. Hivyo basi wale wanaodhani yale yamekwenda naye, wamejidanganya . Yapo na tunayatekeleza. Nimeona niliseme hili Mheshimiwa Spika kwa sababu tayari, kuna baadhi ya watu , mashirika wameanza kulega lega kwenye utendaji.

Wizi umeanza kushamiri katika baadhi ya maeneo lakini kuna wawekezaji ambao walikuwa kwenye njia nzuri ya majadiliano na serikali, wameanza kuvuta nyuma. Nataka niwaambie mwendo ni ule ule. Watanzania walio wengi ni mashuhuda wa mambo makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Orodha ya mafanikio ni ndefu kwa maana ya kuanisha kila sekta. Lakini kwa ufupi, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli na Makamu wake, Samia, itakumbukwa ilivyotimiza wajibu wa kuwatumikia Watanzania kwa kudumisha umoja, amani na kuimarisha Muungano.

Itakumbukwa ilivyoongeza mapato, kupanua wigo wa kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, kujenga vituo vya afya, zahanati na hospitali za wilaya na mikoa, utekelezaji miradi ya maji, kujenga barabara na utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Serikali ya Awamu ya Tano ilifanikiwa kudhibiti na kukomesha uhalifu, iliimarisha maadili na nidhamu na utendaji kazi serikalini. Watumishi wazembe walioshindwa kufanya kazi kwa weledi walichukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwamo kuwatumbua au kuwashusha vyeo na mishahara au kupewa onyo kali.

Kwa upande wa Serikali ya Awamu ya Sita, ni faraja kubwa kuona ambavyo katika siku 100 za Samia madarakani zilizotimia jana, akiendelea kuthibitishia Watanzania kwamba mwendo ni ule ule kwa maana ya kuendeleza mambo mazuri ya serikali zilizotangulia.

Kazi inaendelea katika kudhibiti uzembe, ubadhirifu, wizi miongoni mwa watumishi wa umma kama alivyofanya mtangulizi wake, jambo ambalo limeendelea kushuhudiwa likiendelea kufanyika.

Viongozi na watendaji wameendelea kuwajibishwa hatua ambayo watu wa kada tofauti wakiwamo wanasiasa , wasomi walinukuliwa hivi karibuni na HabariLEO wakipongeza kwa kusema, Rais Samia amedhihirisha kwa vitendo falsafa yake ya ‘Kazi Iendelee’.

Katika kipindi kifupi cha uongozi wake, tumeshashuhudia watendaji na viongozi wengi waliowajibishwa ama kwa kusimamishwa kazi au kuvuliwa nyadhifa na Rais mwenyewe, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri mbalimbali.

Licha ya kuwajibisha watumishi wa umma, Rais Samia amefanya jambo kubwa zaidi la kuupa utumishi wa umma heshima kwa kupandisha madaraja kwa maelfu ya watumishi sambamba na kulipa malimbikizo ya madai yao ya muda mrefu.

Wameshuhudiwa watu wa kada tofauti vikiwamo vyama vya wafanyakazi vikipongeza hatua hiyo kuwa ni ya aina yake. Jambo lingine kubwa lililofanywa na Serikali ya Samia ikiwa ni mwendelezo wa kuwatumikia na kuwaletea wananchi maendeleo, ni uamuzi wa kupunguza gharama za uungajisha umeme uliotangazwa hivi karibuni.

Ndani ya siku 100, tumeshuhudia maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita yaliyoweka bayana kuwa sasa bei ya kuunganisha umeme ni Sh 27,000 kwa nchi nzima; iwe kijijini au mjini badala ya Sh 340,000 iliyokuwepo. Akizungumza bungeni hivi karibuni, Waziri wa Nishati, Medard Kalemani alisisitiza, “iwe ni kijijini anapeleka REA au mjini anapeleka Tanesco bei ni hiyo Sh 27,000.”

Kalemani alielekeza Tanesco atakayesuasua kutekeleza agizo hilo atakuwa hajitaki na hana kazi. Aliweka bayana kwamba kwamba pamoja na kwamba kazi hiyo si ndogo, lakini serikali imejipanga kupeleka umeme kwa wananchi. Wakati huo huo serikali imepiga marufuku Tanesco kuwataka wateja kununua nguzo ikisema, imegharimia nguzo kwa asilimia 100 na kwamba zipo za kutosha.

Kwa mujibu wa Kalemani, mahitaji ya nchi kwa mwaka ni nguzo milioni 2.8 na sasa zilizopo ni milioni 4.9. Kalemani aliwasisitiza wakandarasi na mameneja wa Tanesco kutojiingiza kwenye mtego wa kuwataka wananchi wanunue nguzo.

“Kwa hiyo jipangeni haiwezekani Watanzania wote waishi kwenye meta 30 kutoka kwenye nguzo. Lazima muwe wabunifu,” Waziri Kalemani aliagiza. Maelekezo haya ni ukombozi mkubwa kwa wananchi ikizingatiwa kwamba, wapo watu wengi walioshindwa kuunganisha umeme kutokana na kiwango cha awali kuwa kikubwa ikilinganishwa na uwezo wao.

Naamini maelfu ya Watanzania yatamiminika Tanesco kuomba kuunganishiwa umeme. Ni imani kwamba, Tanesco itaendeleza kasi ya kuwaunganishia wananchi umeme bila vikwazo vyovyote kwa kuwa Waziri Kalemani amethibitisha kwamba serikali imejipanga juu ya hilo na nguzo zipo za kutosha.

Hongera Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendeleza na kuanzisha mambo mazuri mapya kwa maendeleo ya Taifa na wananchi.

Endeleza mwendo huo huo wa kuendeleza mambo mazuri ya serikali zilizotangulia na hata kuanzisha mapya yenye maslahi mapana kwa Taifa kama suala hili la kupunguza gharama za kuunganisha umeme kutoka Sh 340,000 hadi Sh 27,000. Shime Rais wetu. Kazi Iendelee.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/03244135ec27a9111fc420256ce6bb2f.jpg

NIPO nyumbani kwa Baba na Mama Chichi. ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi