loader
Dstv Habarileo  Mobile
MAONESHO YA 45 YA SABASABA: Kuna fursa lukuki viwanda vya kuzalisha mbolea nchini

MAONESHO YA 45 YA SABASABA: Kuna fursa lukuki viwanda vya kuzalisha mbolea nchini

MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), pamoja na jukumu la kudhibiti ubora wa mbolea, pia husimamia biashara ya mbolea na kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na bei nafuu kwa mkulima.

Vilevile husimamia uzalishaji wa mbolea wa ndani, ikihamasisha wafanyabiashara wa ndani na nje kuwekeza katika biashara na utengenezaji wa mbolea nchini. Wakati Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yakiwa yameanza Juni 28 na yatamalizika Julai 13, 2021.

Mwandishi Wetu katika makala haya anaeleza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ili kuhakikisha Tanzania inakidhi mahitaji ya mbolea kwa wakulima. Wakulima nchini hutumia kati ya tani 350,000 na 500,000 za mbolea kwa mwaka.

Lakini asilimia 90 ya mbolea yote inayotumika nchini hutoka nje ya nchi huku wawekezaji wa ndani wakizalisha asilimia 10 tu. Kiasi hicho kinachozalishwa ndani, takribani asilimia 80 yake huzalishwa na kiwanda cha Minjingu kilichopo Mkoani Manyara.

Ni katika muktadha huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dk Stephan Ngailo anasema ni muhimu kwa serikali kuchukua hatua madhubuti ili kuona uzalishaji wa mbolea nchini unaongezeka na wakulima wakipata mbolea bora kwa wakati na kwa bei nafuu. Hatua hiyo pia itaokokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza mbolea nje.

Majukumu ya TRFA

Katika kutekeleza majukumu yake, TFRA hutoa huduma mbalimbali za udhibiti ikiwemo kusajili mbolea na visaidizi vyake, wafanyabiashara na wawekezaji, maeneo ya shughuli za mbolea, wakaguzi na wachambuzi wa mbolea. Kazi zingine ni kutoa vibali vya kuingiza mbolea kutoka nje, leseni za watengenezaji na wafanyabiashara wa mbolea na visaidizi vyake.

Dk Ngailo anasema uzalishaji wa ndani wa mbolea bado uko chini sana, hivyo jitihada zaidi zinahitajika kuongeza uzalishaji wa ndani ili kutosheleza mahitaji ya wakulima. Ushiriki wa TFRA katika maonesho ya 45 ya kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba, barabara ya Kilwa, Dar es Salaam unatarajia kuleta hamasa ya uwekezaji katika viwanda vya mbolea nchini.

Kaulimbiu ya Maonesho ya Sabasaba kwa mwaka wa 2021 ni “Uchumi wa viwanda kwa ajira endelevu” ambayo inahamasisha umuhimu wa viwanda katika kutoa ajira na kukuza uchumi.

Matumizi ya mbolea bado madogo nchini

Dk Ngailo anaeleza kuwa mkutano wa wakuu wa nchi uliofanyika Abuja mwaka 2016 uliazimia masuala mbalimbali katika kilimo ikiwemo kuongeza matumizi ya mbolea katika eneo la ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kufikia angalau kilo 50 za viinilishe vya mmea (Plant Nutrients) kwa hekta.

Hata hivyo, matumizi ya viinilishe vya mbolea kwa Tanzania ni kilo 19 kwa hekta ambayo ni sawa na asilimia 38 ya kiasi kilichopendekezwa katika Azimio la Abuja.

Matumizi hayo madogo anasema yanatokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na bei kubwa za mbolea kwa wakulima, masharti ya ulipaji yasiyozingatia mizunguko ya msimu wa kilimo, uelewa mdogo juu ya matumizi ya mbolea na wakulima kutokuwa na uhakika wa masoko ya mazao na hivyo kutoona tija ya kuwekeza fedha zao kwenye mbolea.

Kutokana na hali hiyo, Dk Ngailo anasema Serikali iliona umuhimu wa kubuni mikakati mbalimbali ambayo ingesaidia kuhakikisha kuwa bei ya mbolea inashuka na wakulima wanawekewa masharti rafiki ya kuilipia.

Mikakati hiyo ni pamoja na kufuta tozo mbalimbali zilizokuwa zikitozwa kwenye mbolea, kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya mbolea na visaidizi vyake (FFS -Fertilizer and Fertilizer Supplements), kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa katika kuelimisha wakulima manufaa ya kutumia mbolea na kuanzisha Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS –Bulk Procurement System) ili mbolea ipatikane kwa punguzo litokanalo na ununuzi na usafirishaji wa mbolea nyingi kwa wakati mmoja.

Viwanda vya mbolea vilivyopo

Hadi kufikia mwezi Mei 2021, kulikuwa na viwanda 20. Viwanda vitatu; vilivyoko Tanga viwili na kimoja Dodoma hutengeneza visaidizi vya mbolea kwa ajili ya kuondoa tindikali au uchachu ili kuweka mazingira mazuri kwa viini lishe vya mbolea kuchukuliwa na mmea.

Viwanda 17 hutengeneza mbolea za aina mbalimbali za kupandia na vinapatikana mkoani Manyara (1), Arusha (10), Kilimanjaro (3), Tanga (2), Dodoma (1), Pwani (2) na Dar es Salaam (1).

Kwa miaka 10 iliyopita, Dk Ngailo anasema viwanda hivi vimekuwa vikitengeneza tani 20,000 – 35,000 ambapo tani 15,000 – 25,000 (asilimia 70 – 80 ya FFS zote zinazotengenezwa nchini) zimekuwa zikitengenezwa na Kiwanda cha Minjingu kilichoko mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa Dk Ngailo, katika miaka kumi iliyopita, utengenezaji wa mbolea ndani ya nchi umekuwa ukichangia matumizi ya wakulima kwa asilimia 4 – 10 na kiasi kilichobaki kiingizwa nchini kutoka nje ya nchi. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, wakulima wa Tanzania wamekuwa wakitumia jumla ya tani 250,000 – 500,000 kwa mwaka.

Mchango huu mdogo wa viwanda vya ndani katika soko la mbolea nchini umetokana na gharama kubwa za uwekezaji na gharama kubwa za uendeshaji kwa maana ya malighafi, nishati na kodi katika malighafi ziingizwazo kutoka nje ya nchi. Pamoja na jitihada za serikali kushughulikia changamoto hizo, TFRA bado inaendelea kuhamasisha wadau kutoka ndani ya nje ya nchi kuwekeza katika utengenezaji wa mbolea na visaidizi vyake hapa nchini.

Hadi kufikia mwezi Mei 2021 jumla ya wadau saba kutoka nchi mbalimbali walionesha nia ya kuwekeza katika utengenezaji wa mbolea na visaidizi vyake na TFRA inashirikiana nao katika kufanikisha azma zao. TFRA hufanya kazi kwa karibu sana na kituo cha uwekezaji (TIC) na pia hutoa huduma zote za udhibiti na ushauri ili kuwezesha wawekezaji kufanikisha malengo yao.

Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuongeza uzalishaji wa mbolea nchini ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wafanyabiashara wa mbolea na watu wengine wenye uwezo wa kujenga viwanda vya mbolea. Serikali pia huhamasisha viwanda vilivyopo kuongeza uzalishaji wa mbolea na kushirikiana na wazalishaji wa mbolea wa ndani kuainisha changamoto zinazowakabili na kuziwasilisha mamlaka za juu kwa utatuzi.

Serikali pia imekuwa ikihamasisha matumizi ya mbolea zinazotengenezwa nchini kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mashamba ya mifano kwa ajili ya kuonyesha ufanisi wa mbolea wanazozalisha ili wakulima na wadau wa kilimo waweze kuziona.

Fursa za uwekezaji viwanda vya mbolea

Dk Ngailo anasema Tanzania ni nchi inayofaa kwa uwekezaji katika viwanda vya mbolea na visaidizi vyake kutokana na fursa zilizopo ikiwa ni pamoja na utashi mkubwa wa kisiasa na soko kubwa la ndani na nje ya nchi. Anasema pia nchi ina mtandao wa mzuri wa barabara na pia kuna malighafi aina zote (Nitrogen, Phosphates na Potassium) kwa ajili ya utengenezaji wa mbolea za aina mbalimbali.

Anasema malighafi hizo zinatosheleza utengenezaji wa mbolea kwa miaka zaidi ya 100 ijayo. Fursa zingine zilizopo ni upatikanaji wa rasilimali watu wa kada zote wakiwemo wa kutoa utalaamu katika viwanda hivyo. Fursa zingine ni uwepo wa vituo vya utafiti kuhusu mbolea inayofaa kulingana na afya ya udongo wa eneo na zao husika.

Kuongezeka kwa viwanda vinavyochakata mazao ya kilimo nayo ni fursa muhimu kwa viwanda vya mbolea kwani matumizi ya mbolea yataongezeka. Ukiacha uwekezaji katika viwanda, pia kuna fursa za uwekezaji katika huduma nyingine wezeshi kama vile maghala ya kuhifadhi mbolea, utengenezaji wa vifungashio vya mbolea, huduma ya usafirishaji na nyinginezo.

Elimu zaidi kwa kilimo chenye tija

Ili kuongeza tija ni muhimu wadau wa kilimo kuendelea kuwaelimisha wakulima kuzingatia kanuni za kilimo bora ili kuongeza tija katika uzalishaji kwa utoshelevu wa chakula, kuongeza kipato na kukuza uchumi wa nchi.

Mambo ya kufuata kuanzisha kiwanda Kaimu Meneja wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, TFRA, Bwana Nkonya, anasema taratibu ambazo mwekezaji wa kiwanda cha mbolea anatakiwa kuzifuata ni pamoja na kutambulika kisheria kwa kuisajili kampuni na kuwasilisha maombi ya kuwekeza katika kiwanda cha mbolea TFRA.

Taratibu zingine ni kufanya tathmini ya athari kwa mazingira, TFRA kufanya ukaguzi wa uzalishaji wa mbolea ili kuhakiki ubora wake, usajili wa eneo na hapo mwekezaji atapewa leseni ya TFRA na kutakiwa kusajili mbolea husika. Hadi kufikia mwezi Mei 2021 jumla ya wadau saba kutoka nchi mbalimbali walionesha nia ya kuwekeza katika viwanda vya kutengenezaji mbolea na visaidizi vyake (FFS).

TFRA inaendelea kushirikiana nao katika kufanikisha azma zao. Uwekezaji katika viwanda vya mbolea ni muhimu kwani mbolea ni pembejeo muhimu katika kilimo, ikikosekana uzalishaji wa mazao hushuka na kusababisha nchi kuwa na upungufu wa chakula.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/0b216a0ad0e2059377974a9ecb10a676.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi