loader
Dstv Habarileo  Mobile
Vijana na ajenda zao  tano 2020 hadi 2025

Vijana na ajenda zao tano 2020 hadi 2025

TANZANIA imekuwa nchi ya tano Afrika kuanzisha Jukwaa la Vijana la Kimataifa  ambalo linalenga kukutanisha vijana mbalimbali pamoja ili kujadili masuala yanayowahusu na kuyatafutia ufumbuzi.

Jukwaa hilo ambalo kwa sasa linalelewa na shirika la kimataifa lisilo la kiserikali la Actionaid limezinduliwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Ulemavu), Ummy Nderiananga. Nchi nyingine za Afrika zenye Jukwaa la aina hiyo ni Uganda, Kenya, Zambia na Senegal.

Katika uzinduzi huo, vijana wamewasilisha ajenda zao kuu tano ambazo wanataka wao wenyewe, serikali na wadau wengine wazifanyie kazi kwa ajili ya mustakabali wao na wa taifa kwa ujumla.

Akiwasilisha kwa Naibu Waziri ajenda za vijana wanazotaka zitekelezwe katika kipindi cha miaka mitano (2020-2025), Mwenyekiti wa Ajenda za Vijana, Rogers Fungo, anasema ajenda hizo zilipatikana baada ya vijana kufanya uchunguzi kwa njia ya kuwahoji vijana wenzao Tanzania nzima.

Anasema uchunguzi huo uliibua mambo mengi ambayo ni mahitaji ya vijana lakini katika kuyaweka sawa, wameibuka na mambo matano makuu.

“Huko nyuma tulipokuwa tunaandaa ilani za vijana tulikuwa tunasema ‘tunaitaka serikali… tunaitaka… tunaitaka, lakini sasa tumekuja na ajenda ambazo pamoja na kuitaka serikali ifanye, sisi vijana pia tutashiriki katika utekelezaji wake pamoja na wadau wengine wa maendeleo,” anasema Rogers.

 

KUPATA TAARIFA

Mwenyekiti huyo wa ajenda za vijana anasema hitaji la kwanza la vijana nchini ni kupata taarifa sahihi, kwa wakati na wezeshi kutoka serikalini na kwa wadau wote muhimu.

Anasema katika hilo vijana wanatakiwa pia wawe wanatafuta taarifa huku serikali pia ikiweka mazingira wezeshi ya vijana kupata taarifa muhimu kwao na kwa usahihi wake.

“Siku moja nilikuwa ninazungumza na mheshimiwa mmoja kutoka kwenye wizara inayohusika na sisi vijana. Akaniambia mbona haya mambo unayouliza yanatangazwa? Nikamuuliza yametangazwa wapi? Akajibu kwamba yako kwenye website (tovuti) ya wizara. Jamani, ni vijana wangapi wanatembelea hiyo website?” Anahoji Rogers.

Mwenyekiti hiyo, kwa niaba ya vijana wenzake nchini, anashauri taarifa muhimu kwa vijana zipelekwe ambako wanapatikana kama vile kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari.

 

AJIRA

Rogers anasema hitaji la pili kubwa la vijana wa Tanzania ni ajira. Anasema pamoja na serikali na sekta binafsi kujitahidi sana katika kutengeza fursa za ajira nchini, lakini bado hazilingani na idadi ya vijana walioko kwenye soko la ajira.

Anasema wanachotaka vijana ni serikali kuwasaidia kutengeneza mazingira wezeshi ya vijana kujiajiri.

 

ELIMU

Mwenyekiti hiyo anasema mfumo wa elimu wa Tanzania unapaswa kuangaliwa upya ili kusaidia suala zima la ajenda yao ya pili ya ajira.

Anasema vijana wanapendekeza mfumo wa elimu nchini uwe ni wa kuwawezesha kujitegemea kwa maana ya kumudu kujiajiri.

“Tunataka tufike mahala ambapo mhitimu wa chuo kikuu, akiondoka katika majengo ya chuo anakuja kutengeneza ajira yake na wengine. Yaani tutoke kwenye dhana ya kuzalisha raslimali watu, kwa maana ya watu wanaotoka chuoni na kusubiri wapate kazi. Hapana,” anasema.

Anasema mazingira ya sasa ya mtu kusubiri kuajiriwa hayapo tena nchini.

 

AFYA

Hitaji la tano la vijana nchini kwa mujibu wa mwenyekiti wao ni afya kwa maana ya kuwepo kwa mazingira rahisi na rafiki ya kupata huduma za afya kwa vijana.

Anasema pamoja na serikali kujitahidi kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali huku ikioongeza dawa za kutosha na vifaa tiba ncini lakini vijana wana changamoto zao tofauti na makundi mengine.

“Kwa mfano, vijana wa kiume kuna wakati tunatamani hata tuwe na maduka yetu ya dawa kwa ajili ya wanaume tu. Kwani unaweza kwenda kwenye duka la kawaida ukashindwa kununua baadhi ya vitu unavyotaka kwa sababu unakuta watu wengi wamejaa dukanui. Unajikuta unalazimika kurudi au kuuliza Panadol,” anasema.

 

LETENI MAWAZO MBADALA

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ummy anawataka vijana kukaa pamoja na kutengeneza mawazo mbadala yatakayoisaidia serikali kuiletea jamii maendeleo.

“Ninategemea jukwaa hili liwe tanuri la fikra za vijana wengi hapa nchini katika kutengeneza mawajawabu ya matatizo yanayowakabili wao na jamii kwa ujumla,” anasema na kuongeza kwamba vijana wanategemewa sana na serikali katika kuleta vuguvugu dhidi ya changamoto zinaolikabili taifa.

Analitaka jukwaa hilo kujielekeza katika kuangalia fursa zilizopo kisayansi ili kuwasaidia vijana kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ajira.

CHUKUENI HIZI TAARIFA

Anasema serikali inaendelea na mikakati yake ya kuwawezesha vijana kwa kuwapatia mikopo kupitia halmashauri za miji.

“Mwenyekiti wa ajenda za vijana alikuwa anazungumzia hapa suala la taarifa. Kwa hiyo taarifa moja wapo ninayowapa ni kwamba ile mikopo ya asilimia nne zinazotolewa na halamshari, tumepunguza idadi ya watu kuiomba kutoka 10 hadi sasa vijana watano wanaweza kupata na tunaendelea kufanya maboresho.

“Niwape pia taarifa nyingine kwamba upo Mfuko wa Vijana wa Taifa ambapo pia wapo vijana wananufaka nao… Wapo vijana ambao wameanza kununua hisa wanaziuza, wengine wanafanya kilimo cha mtandao na kuna vijana wamesoma vyuo vikuu kama SUA (Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo) tumewatembelea wamebuni zana za kufanya kilimo cha kisasa,” anasema.

Anasema baadhi ya vijana wa SUA wamebuni trekta dogo ambalo wanaliuza kwa bei ndogo ambayo watanzania wengi wanaweza kununua na kurahisisha kilimo.

Ummy anasema Ofisi ya Waziri Mkuu pia ina programu ya kukuza ujuzi kwa vijana. Anasema wanachukua vijana waliomaliza elimu ya chuo kikuu wanapata mafunzo na baadaye wanawapeleka katika taasisi na mashirika mbalimbali ili wapate ujuzi kupitia programu yao ya kimafunzo mahala pa kazi.

Anatoa wito kwa vijana waliohitimu vyuo vikuu watafute fursa hiyo ya kupata mafunzo hayo kwa kujiandikisha kwa Wakala wa Huduma za Ajira (TAESA).

Anasema serikali pia inawasaidia vijana kwenye kilimo ambapo serikali inapanga kujenga vitalu nyumba (green houses) katika kila halmashauri na kwamba baadhi ya halmashauri zimeanza kujenga vitalu hivyo.

Anasema katika mkakati wa kusaidia vijana serikali ilipelaka vijana 136 Israel ili wapate ujuzi wa namna wenzao wa nchi hiyo wanavyoweza kuendesha kilimo cha kisasa katika mkakati wa kuelekea kwenye kuondokana na kilimo kinachochukiwa na vijana.

 

CHAMBUENI MIFUMO MIBOVU

Mkurugenzi wa Actionaid inayolea jukwaa hilo la vijana, Bavon Christopher anasema shughuli zao kubwa ni kupambana na umaskini kwa makundi ya pembezoni kama wanawake, vijana na watoto ikiwa ni pamoja na kuangalia mifumo ambayo ina matatizo ili kuitafutia mabadiliko chanya.

“Kuna mifumo mingi na si lazima iwe ya serikali lakini inaweza kuwa mibovu. Kuna mifumo katika mila na desturi inayokwamisha maendeleo. Inaweza ikawa mifumo katika elimu, ugawaji wa mikopo na kadhalika. Je, mifumo hii ni rafiki kwa vijana au makundi mengine ya pembezoni?” Anawataka vijana kuhoji.
 

Anawahimiza vijana katika jukwaa hilo kuchambua mifumo mibovu na kupendekeza namna ya kuiboresha.

VIONGOZI BORA WAKO HUKU

Anapongeza serikali kwa kuteua vijana katika uongozi lakini anazitaka mamlaka za uteuzi pia kuangalia kwenye taasisi zisizo za kiserikali zinazolea vijana kama Actionaid.

Anamhakikishia Naibu Waziri na Ummy kwamba Jukwaa jilo lililozinduliwa litapika viongozi wa baadaye kwani kimsingi hiyo ni atamizi (incubator)

 

“Huku tunapika vijana ambao wanaelewa maana ya kuwajibika, watu ambao wanaelewa matatizo. Wamekua au watakua muda wote wakipembua matatizo na kuyatafutia ufumbuzi. Maana yake ni kwamba ukimpata kiongozi hapa unapata kiongozi ambaye anakuwa moja kwa moja ni suluhu ya matatizo katika jamii. Hana haja ya kukaa miezi sita ya kujifunza,” anasema.

Anafafanua kwamba kituo hicho kilichozinduliwa si cha itikadi fulani ya kisiasa au dini bali ni cha vijana wote nchini kujadili mambo ya kuwanyanyua kimaendeleo.  

“Hapa ni jukwaa la vijana wote, kuangalia ajenda za vijana na kuzichambua na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zao. Natoa wito sisi tulioko hapa tuwe chachu au wawakilishi wa kutafuta vijana wengine zaidi bila kujali elimu zao; waendesha boda boda, wavuvi, wakulima, wasanii na kadhalika,” anasema.

Anasema viongozi waasisi wa Afrika, akina Mwalimu Julius Nyerere, Kenneth Kaunda (Zambia) na wengineo, wakati huo wakiwa vijana, waliona umuhimu wa namna ya kulikomboa bara la afrika kwa kuunda umoja wao wa wanamajumui wa Afrika.

Ni katika muktadha huo, Bavon anasema jukwaa hilo linalowaleta pamoja vijana ni vyema wakalitumia kama umoja wa kuwakomba vijana nchini.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f4b915c6095f05807e45abee381ebb00.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi