loader
Dstv Habarileo  Mobile
Siku 100 Urais wa Samia Wizara ya Ardhi imefanya makubwa

Siku 100 Urais wa Samia Wizara ya Ardhi imefanya makubwa

JUZI Gazeti hili lilikuwa na makala isemayo: ‘Wizara Ardhi ‘ilivyochuma matunda’ 24 Urais wa Samia’. Tuliona mafanikio lukuki katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi yaliyopatikana chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu katika kipindi cha siku 100 alizokuwa madarakani tangu Machi 2021. Katika makala haya, JOSEPH SABINUS anaendelea kuchambua mafanikio mengine kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya habari. FUATILIA.

Kwa nyakati tofauti, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mary Makondo, wanasema katika siku 100 za uongozi wa Rais Samia, Serikali imeendelea kuwezesha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya kujenga viwanda na uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.

Kwa mujibu wa viongozi hao wa wizara, ili kutekeleza jukumu hilo, Wizara imeendelea kuzisimamia mamlaka za upangaji kutenga maeneo na fedha ili kulipa fidia kwa ajili ya uwekezaji wakati wa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi mijini na vijijini.

Lukuvi anamshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa kuiwezesha wizara yake kuendelea kutimiza malengo kwa kadiri ya maelekezo na uongozi wake Rais akisema: “Katika kipindi hiki, Serikali chini ya Rais Samia, imeendelea kufanya ukaguzi na uhakiki wa mashamba makubwa ili kubaini utekelezaji wa masharti yaliyomo kwenye mikataba ya umilikishwaji ardhi ya uwekezaji.”

“Miliki za mashamba ambayo wamiliki wamekiuka masharti ya umiliki hubatilishwa na ardhi ya mashamba husika na kupangwa upya ili kupata ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali…”

Kutokana na msingi huo wa uongozi wa Rais Samia, Lukuvi anasema katika kipindi cha Machi 2021 Rais Samia alipoingia madarakani hadi Juni 2021, hekta 7,346 zimetengwa kwa ajili ya uwekezaji.

Kuhusu utoaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji kupitia Kamati ya Taifa ya Kugawa Ardhi, Lukuvi anasema Sheria ya Uwekezaji Na. 7 ya Mwaka 1997 na Sheria ya Ardhi Na.4 ya Mwaka 1999 zinatoa fursa kwa mwekezaji wa kigeni kupewa ardhi baada ya kukidhi vigezo kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) au Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA).

Anasema: “Jukumu la ugawaji ardhi kwa ajili ya uwekezaji linafanywa na Wizara kupitia Kamati ya Taifa ya Ugawaji.”

Kwa mujibu wa waziri huyo, katika siku 100 za Urais wa Samia Suluhu, kamati imeidhinisha maombi yote ya ardhi 72 yenye ukubwa wa hekta 4,007.

“Kati ya maombi hayo 72, maombi 45 yenye ukubwa wa hekta 3,610 ni ya wawekezaji kutoka nye ya nchi waliomilikishwa kupitia TIC na EPZA. Maombi 27 yenye ukubwa wa hekta 397 ni ya kampuni za Kitanzania,” anasema.

Akijikita katika uhawilishaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji, Lukuvi anafahamisha kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Sura ya 113, ardhi ya uwekezaji kutoka ardhi ya kijiji au hifadhi huhitaji kuhaulishwa kuwa ardhi ya kawaida kwa manufaa ya umma.

Hatua za uhaulishaji huanzia katika ngazi ya kijiji, wilaya, Wizara na hatimaye kuwasilisha mapendekezo kwa Rais ili kupata idhini.

“Katika kipindi cha Machi 2021 hadi Juni, 2021, ardhi yenye ukubwa wa hekta 36,335.72 imehaulishwa katika Halmashauri za Wilaya za Kilwa, Ruangwa na Morogoro. Ardhi iliyohaulishwa itamilikishwa kwa wawekezaji kupitia TIC na EPZA,” anasema Lukuvi.

Aidha, anasema katika kipindi hicho, michoro ya mipangomiji 860 yenye jumla ya viwanja 46,196 kwa maeneo mapya ilipokewa na kuidhinishwa.

Kuhusu urasimishaji makazi, anasema chini ya Uongozi wa Rais Samia, wizara yake inaendelea kutekeleza Programu ya Kurasimisha Makazi na Kuzuia Makazi Yasiyopangwa Mijini (2013 - 2023).

Anasema: “Lengo  la programu ni kuhakikisha usalama wa miliki na kuwezesha upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya huduma za kijamii na miundombinu muhimu kwa njia shirikishi kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na miongozo ya sekta ya ardhi.”

Kwa mujibu wa Lukuvi, katika kipindi cha Urais wa Samia, wizara kwa kushirikiana na mamlaka za upangaji iliandaa michoro ya urasimishaji 157 yenye viwanja 41,549 katika halmashauri mbalimbali nchini na taratibu za kuwapatia wananchi hatimiliki zao zipo katika hatua mbalimbali.

Anasema kwa mujibu wa Sheria ya Mipangomiji, Sura ya 355, upangaji na uendelezaji wa miji ni suala mtambuka linaloshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wamiliki wa ardhi, taasisi zisizo za kiserikali, sekta binafsi, asasi za kijamii na taasisi zinazotoa huduma za miundombinu kama vile barabara, umeme, maji na mawasiliano. 

“Tangu Rais Samia aingie madarakani Machi 2021, mwaka huu, maombi 90 ya mabadiliko ya matumizi ya ardhi yameidhinishwa kutoka mamlaka mbalimbali za upangaji nchini kwa kuzingatia Sheria ya Mipangomiji Na.8 ya Mwaka 2007,” anasema.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inayoongozwa na Lukuvi na Naibu Waziri, Dk Angelina Mabula, inamshukuru Rais Samia ikisema katika kipindii cha urais wake, ameisaidia kwa kuiwezesha kuendelea kuboresha utoaji wa huduma na utunzaji wa taarifa za ardhi.

Imebainika kuwa, Wizara kwa nyakati tofauti imeunda mifumo mbalimbali ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ili kurahisisha utendaji kazi katika sekta ya ardhi.

Kwa mujibu wa uchunguzi, mifumo hiyo ni pamoja na Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Ardhi pamoja na Usajili wa hati (MOLIS),  Mfumo wa Usimamizi wa Kodi ya Pango la Ardhi (LRMS), Mfumo wa Uidhinishaji wa kazi za Upimaji na Ramani (SRS), Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Majalada (FMS) na Mfumo wa Taarifa za mashamba (LIMS).

Ili kukabiliana na changamoto za kimfumo, wizara ilisanifu na kujenga Mfumo Unganishi wa Taarifa za Ardhi (ILMIS) unaounganisha taarifa za umiliki na taarifa za kijiografia zinazohusisha ramani za msingi, michoro ya mipangomiji na ramani za upimaji.

Miongoni mwa faida zinazotajwa mintarafu mfumo huu, ni pamoja na kusaidia kutoa huduma kwa uwazi, kuondoa umilikishaji wa kiwanja kimoja kwa zaidi ya mtu mmoja na kutoa huduma kwa haraka na kwa usahihi.

Lukuvi anafahamisha akisema: ”Tangu Machi 2021 hadi Juni, 2021, Wizara imekamilisha maboresho ya mfumo katika miamala msingi na ipo katika hatua za majaribio kwa kutumia taarifa za Jiji la Dodoma kabla ya kuanza kutoa hati ya kielektroniki.”

Anasema kazi ya kuchambua, kupiga picha (scanning) na kuhifadhi michoro na ramani za ardhi za mipangomiji na ramani za upimaji imefanyika katika Jiji la Dodoma.

“Tayari michoro 890 ya mipangomiji na michoro 4,300 ya upimaji na ramani yenye viwanja 215,400 imebadilishwa kutoka mfumo wa analogia kwenda mfumo wa digiti ili itumike katika mfumo unganishi wa taarifa za ardhi ulioboreshwa,” anasema Lukuvi.

Lukuvi anazidi kumshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa kuiwezesha wizara anayoiongoza kuzidi kuboresha huduma kwa wateja.

Anasema: “Ndani ya siku 100 za Urais wa Mheshimiwa Rais Samia, ametuwezesha na kutusaidia kiasi kwamba kama wizara, tumeanzisha ‘Call Centre’ yaani kituo cha mawasiliano kwa wateja katika Ofisi ya Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.”

“Hatua hii imelenga kuwezesha mawasiliano ya moja kwa moja na wateja popote walipo kwa njia ya simu na kutatua changamoto zinazowakabili bila kulazimika kufika katika ofisi za ardhi.”

Lukuvi anasema: “Utaratibu huo unatarajiwa kuwapunguzia wananchi kero, gharama za usafiri na muda wa kupata huduma. Wizara pia imeboresha ukadiriaji wa kodi ya pango la ardhi mtandaoni na sasa mwananchi anaweza kulipa kodi ya pango la ardhi anayodaiwa kupitia simu ya mkononi. Wizara imekamilisha Mkataba wa Huduma kwa Mteja ambao ni mwongozo wa utoaji wa huduma. Mkataba huo unapatikana kupitia tovuti ya Wizara (www.lands.go.tz).”

Itaendelea 

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/de9ec850d511578e934839548fe7c03b.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi