loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wananchi Konde sikilizeni vyema sera za wagombea

Wananchi Konde sikilizeni vyema sera za wagombea

WAKATI wa kusikiliza sera na ahadi za wagombea na baadae kuamua kwa wananchi wa Jimbo la Konde, wilaya ya Micheweni, mkoa wa Kaskazini Pemba umewadia.

Wananchi wa jimbo hilo wanajiandaa na uchguzi mdogo wa marudio wa kiti cha ubunge.

Ndio, sasa ni wakati wa wananchi wa Konde wa kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni ili kuwasiliza wagombea na sera za vyama vyao waweze kuwa na chaguo sahihi kwa ajili ya maendeleo yao. 

Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Yasini Jabu Hamis alifanya uteuzi wa wagombea 12 ambao ndio wanaowania ubunge ili kujaza nafasi iliyowazi kwenye jimbo hilo. 

Vyama vilivyojitokeza kuwania nafasi hiyo, kwanza vinatakiwa kupongezwa kwa kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha wanasimamisha wagombea. 

Labda kuwakumbusha tu, wananchi hasa wapigakura wa Jimbo la Konde, vyama vilivyo na usajili wa kudumu nchi hii ni 14, lakini katika jimbo hilo  vyama 12 vimethubutu kusimamisha wagombea.

Wagombea waliosimishwa na vyama vyao na Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC) baada ya kukidhi vigezo vya uteuzi ni Mohamed Said Issa (ACT Wazalendo), Sheha Mpemba Faki (CCM), Salama Khamis Omar (CUF), Yahaya Mwinyi Ali (SAU) na Abdirahim Ali Slum (NCCR-Mageuzi).

Wengine walioteuliwa ni Ali Kassim Hamad (TLP), Mohamed Suleiman Said (Chadema), Rashid Hamad Said (Demokrasia Makini), Salma Abdallah Hamad (CCK), Suleiman Khamis Rashid (UPDP), Issa Shaame Hassan (NRA) na Fatma Rajab Omar (ADA-Tadea).

Katika kuangalia usawa wa kijinsia navipongeza vyama vitatu vya ADA –Tadea, CCK na CUF kwa kusimamisha wagombea wanawake tofauti na wenzao tisa waliosimamisha wanaume.

Jimbo la Konde kwa mujibu wa taarifa za Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, lina jumla ya wapiga kura 6,636 walioandikishwa katika daftari hilo.  

Hivyo, wakati nawahimiza wananchi hao 6,636 kujitokeza kwa wingi katika mkutano ya kampeni ambayo ilianza Juni 28 na kumalizika Julai 17, vyama navyo vizingatie maadili ya uchaguzi wakati wote wa kampeni.

Vyama vya siasa kwa mujibu wa miongozo inayotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa vinapaswa wakati huu wa kampeni kunadi sera zao zitakazowafanya wapigakura kuwachagua.

Kamwe hampaswi kama vyama na wagombea kunadi sera zinazopingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya Zanzibar na sheria nyingine za nchi. 

Wananchi wa Konde, shime mjitokeze kwa wingi mkasikilize sera za vyama na wagombea wao kwa umakini ili muweze kuchambua chuya na mchele siku ya kupiga kura Julai 18, mwaka huu.

Daima tunapokwenda katika mikutano hiyo tuzingatie sana suala la amani na utulivu katika kampeni, tukumbuke sisi sote ni ndugu hivyo siasa zisitufanye tugombane na kufanyiana vitendo visivyofaa ilhali uchaguzi utapita lakini maisha yataendelea. 

Ni wakati wa kusikiliza sera na si kugombana, lakini pia muendelee kuhamisishana siku ya kupiga kura kujitokeza kwa wingi na kupiga kura kwa amani na utulivu.

Ni haki ya kila mwananmchi ambaye anasifa za kupiga kura kutumia haki yake hiyo ya msingi kumchagua kiongozi anyemtaka.

Tusitegeane na kusema “Ah! mbona ameshashinda miye kura ya nini,” hapana tujitokeze kupiga kura.

Watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wana kadi zao za Mpiga Kura. 

Hata hivyo, NEC kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 61(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, pamoja na kifungu cha 62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala kama vile hati ya kusafiria, kitambulisha cha taifa au leseni ya udereva.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a63e03a28f85e1ef779b69bb9748286e.jpeg

TAARIFA za matukio ya mimba na ...

foto
Mwandishi: Mroki Mroki

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi