loader
Dstv Habarileo  Mobile
Matumizi ya dijiti katika kilimo  yanavyoashiria mapinduzi ya kijani

Matumizi ya dijiti katika kilimo yanavyoashiria mapinduzi ya kijani

SHIRIKA la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), linaamini kuwa ubunifu katika matumizi ya dijiti, hususani teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika kilimo utasaidia pakubwa katika kushirikisha vijana kwenye shughuli za kilimo hatimaye kupunguza ukosefu wa ajira miongoni mwao.

FAO imesema ni muhimu teknolojia ya dijiti katika kilimo kukumbatiwa ili kuleta mapinduzi ya kijani na kuzuia idadi kubwa ya vijana duniani kote ambao wanachagua kuishi mijini wakisaka kazi za ofisini bila kufahamu kwamba kilimo kina uwezo mkubwa wa kuwapa kipato maradufu.

Takwimu za shirika hilo zinaonesha kwamba katika nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara asilimia 60 ya watu wake, sawa na takribani watu bilioni 1.2 ni wa umri wa chini ya miaka 25.

Ni katika muktadha huo, kampuni inayojuhusisha na Tehama pamoja na fedha ya Bizy Tech Limited, imeanzisha mifumo ya kidijiti kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo ili kuwapatia huduma za kifedha, ikiwa ni pamoja na kutumia Tehama kuwasaidia kupanga, kutekeleza na kutathmini biashara zao.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Mkurungezi wa Bizy Tech, Mahmoud Shoo, anasema baada ya tafiti mbalimbali na ugunduzi wao mintarafu changamoto mbalimbali zilizo katika biashara na kilimo, Bizy Tech kama kampuni ya Tehama waliamua kutengeneza mifumo mbalimbali ya kidijiti ili kutatua changamoto hizo.

“Kama wadau wa kilimo tulifanya tafiti mbalimbali ili kujua changamoto zilizopo katika sekta hii na kuchukua maamuzi ya kutumia taaluma yetu ya Tehama ili kutatua changamoto hizo ambazo ni pamoja na upatikanaji hafifu wa pembejeo zenye ubora, unafuu wake na kutopatikana kwa wakati. Tehama inaweza kusaidia sana kutatua hizi changamoto.

“Kulima bila kutimia mbinu bora husababisha uzalishaji wa mazao yasiyo na ubora mzuri na kwa wingi. Wakulima kukosa masoko ya uhakika kwa ajili ya kuuzia mazao yao huwafanya wawe na changamoto kupata fedha na hivyo kushindwa kukidhi mahitaji yao ya kilimo na mengine ya kijamii,” anasema

Anasema wameanzisha kampeni inayojulikana kama “Let's make change” (sasa tufanye mabadiliko) yenye lengo la kuleta mapinduzi katika sekta ya biashara na kilimo kupitia mifumo mbalimbali ya kidijiti inayobuniwa na kutengenezwa na vijana wa kitanzania kwa lengo la kuleta suluhu ya changamoto katika sekta hiyo.

Anasema kwa kuanza na sekta ya kilimo na changamoto walizogundua waliamua kuanzisha mfumo wa kidijiti unaoitwa Kilimo Data Hub (KDH). 

Katika mfumo huo, taarifa za mkulima kwa maana ya jina lake kamili, jina la kikundi alichopo, namba yake ya simu, kijiji, kata, wilaya na mkoa anakoishi pamoja na aina ya mazao anayolima zinasajiliwa kwenye mfumo huo.

Hatua hiyo anasema humfanya mkulima mdogo na wa kati kujulikana na kuweza kupata huduma mbalimbali za kilimo zinazotolewa na BizyTech kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Shoo anasema hiyo inamwezesha mkulima kulima  kilimo chenye tija na mazao yenye ubora ambayo yatafanya aweze kuuza mazao kwa bei nzuri kwenye masoko ya ndani na ya nje ya nchi na hivyo kuweza kukuza kipato chake  na pato la Taifa.

“Mpaka sasa tumeshaweza kusajili wakulima zaidi ya 56,000 kwenye mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa, Songwe, Kigoma na Kagera,” anasema

Akizungumzia kampeni ya “Let's make change”, meneja maendeleo ya biashara wa kampuni hiyo, Michelle Fernandez, wamedhamiria kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo kupitia mbinu mbalimbali kupotia Tehama ikiwemo ya Kilimo Bando.

Anasema Kilimo Bando ni mkusanyiko wa huduma (kifurushi) anayopewa mkulima kwa udhamini wa kikundi cha wakulima ili kuweza kuwasaidia katika shughuli zao za kilimo.

Fernandez anasema kupitia Kilimo Bando, mkulima anaweza kupata huduma mbalimbali kama kujiwekea akiba kidogo kidogo kwenye mfumo rasmi wa kibenki, kupata mikopo, kuunganishwa na masoko ya mazao yao kwa bei nzuri ndani na au nje ya nchi, kupata elimu ya ugani ambayo itamwezesha kuendesha kilimo chenye tija na pia mkulima anaweza kupata bima ya mazao yake. 

“Bizy Tech kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kilimo tumeweza kusogeza huduma hizi kwa mkulima. Mapinduzi makubwa yamefanyika mpaka sasa, tumekuwa ni wakala wa benki kwenye vituo vya huduma nyingi zaidi vijijini, na kwa sasa tuna zaidi ya vituo vya huduma 450,” anasema.

Akifafanua zaidi, Ferdinandez anasema kupitia huduma yao nyingine ya Kilimo Akiba (KIA) mkulima atapata huduma za upatikanaji wa pembejeo za kilimo zenye ubora, kwa wakati na kwa bei nafuu.

Pia huduma yaoa ya usambazaji wa pembejeo imekusudia kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye mnyororo wa usambazaji ambapo katika utafiti waliofanya waligundua changamoto ya kutokuwepo kwa takwimu sahihi za mahitaji.

Changamoto zingine wanazojaribu kutatua anasema ni wakulima kutokua na pesa za kutosheleza kununua pembejeo, pembejeo kuchelewa kuwafikia wakulima, pembejeo kufika kwa wakulima zikiwa hazina ubora unaotakiwa na bei za pembejeo kuwa juu.

“Kwa kutatua changamoto zao tumewapa wakulima waleti namba, tumeshirikiana na wasambazaji wa pembejeo ili kupata bei nafuu, tumewapatia wakulima namba maalumu kwa ajili ya kuweka mahitaji (USSD CODE) *150*44#. Kwa kufanya hivyo tumeweza kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto hizo,” anasisitiza Fernandez.

Anasema kupitia kifurushi cha Kilimo Bando pia mkulima anapata huduma ya Kilimo Mkopo yenye lengo la kuwashika mkono wakulima kuelekea kwenye kilimo cha tija kwa kupata mikopo yenye masharti nafuu.

Pia amesema kupitia Kilimo Bando kuna kifurushi cha ‘Uza nasi’ ambacho kinalenga kuwaunganisha wakulima na masoko ya ndani na nje ya nchi kupitia mabalozi wetu na kuuza mazao yao kwenye masoko sahihi ili kuwawezesha kupata faida zaidi.

“Kuna kifurushi pia cha Bima ya Mazao inayokusudia kusaidia wakulima kwenye majanga au matatizo yoyote yanayoweza kuharibu mfumo wote wa uzalishaji kama vile hatari za moto, magonjwa ya mazao na mabadiliko ya tabianchi. Kilimo Bima inashirikiana na wadau wengine kwenye tasnia ya huduma za bima nchini na bima za mazao ya wakulima,” anasema.

Anataja masharti ya kujiunga na kilimo bando ni pamoja na kuwa mkulima, kujiunga kwenye kikundi (Amcos/Vicoba) kisichopungua watu 20 na kila mkulima kuwa na kitambulisho (cha kura au cha Taifa).

Anasema kusajiliwa kidijiti ni bure ambapo mkulima akishasajiliwa anapatiwa kitambulisho cha kilimo akiba kinachofahamika kama ‘Kia – e wallet’.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/54e64a0c6e000d544ca387ee7baf83db.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro  

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi