loader
Dstv Habarileo  Mobile
Pongezi Veta kwa kuliona hili

Pongezi Veta kwa kuliona hili

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), imesema imejipanga kushirikiana na wizara zinazohusu elimu na viwanda ili kuhakikisha ufundishaji unakuwa wa vitendo zaidi kwa kutumia vifaa vilivyotengenezwa nchini.

Imesema hatua hiyo inalenga kuzalisha vijana wengi wenye ujuzi ili waingie katika soko la ajira na uchumi wa viwanda. Tunapongeza hatua hiyo ya Veta, kwani tunatambua itakuwa ni mwarobaini wa kuwawezesha vijana wengi kuwa na ujuzi wa aina mbalimbali hivyo kuweza kujiajiri au kuajiriwa kwa urahisi.

Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kuwa elimu inayotolewa na taasisi mbalimbali nchini kuanzia ngazi za chini hadi juu imejikita zaidi katika nadharia kuliko vitendo na kuwapa wakati mgumu wahitimu baada ya masomo yao.

Mfumo huo wa elimu umekuwa ukisababishwa vijana wengi wanapomaliza masomo kubaki mitaani wakizurura kutafuta ajira za kuajiriwa na wengine kukaa vijiweni na kulalamika kukosa ajira kutokana na kutokuwa na ujuzi wa aina yoyote.

Hivyo, hatua hiyo ya Veta si tu itawapa ujuzi wa aina mbalimbali vijana wengi, lakini pia itaongeza ubunifu na kuchochea ugunduzi wa kisayansi wa masuala mbalimbali ya maendeleo ya teknolojia, mambo ambayo ni muhimu sana katika duniani ya sasa na maendeleo ya kiuchumi.

Kwa kuwa Veta ipo katika mikoa na wilaya nyingi nchini, ni wakati mwafaka kutumia huduma za Veta kuwafikia wanafunzi mpaka waliopo vijijini ili kuwapa ujuzi wa aina mbalimbali kwa manufaa yao na taifa.

Tunatambua kuwa, kuna vyuo 43 vinavyofanya kazi na vingine 33 vinajengwa na 30 vitakamilika mwaka huu na hadi mwakani kutakuwa na vyuo 71 vinavyofanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini.

Rai yetu kwa Veta, ijipange kuaandaa mitaala iliyofanyiwa utafiti wa kutosha kuhusu mahitaji ya sasa katika soko la ajira, biashara na uchumi ili mafunzo hayo yaweze kuwa na tija wahitimu watakapomaliza masomo yao na kuingia mitaani.

Tunashauri mitaala hiyo isijikite tu katika ufundi uliozoeleka kama wa magari, umeme, ushonaji, useremala, ususi, umakenika na mwingine wa aina hiyo, bali pia iwajenge vijana kuwa wabunifu wa kutengeneza zana za kisasa zinakazosaidia masuala mbalimbali katika sekta muhimu ya kilimo, mitambio ya kuongeza thamani ya mazao na teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Tunaipongeza na kuitia moyo Veta katika mipango yake hiyo, ili kuwaandaa vyema vijana wetu wamalizao masomo yao watumie ujuzi walioupata kujiendeleza kiuchumi na taifa kwa ujumla.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/cacc7e68d465eae075e232c4739a2ce4.jpg

Miradi ya Maendeleo katika halmashauri za Serengeti, ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi