loader
Dstv Habarileo  Mobile
Maadili haya yapaswa kuzingatiwa uchaguzi mdogo jimbo la Konde      

Maadili haya yapaswa kuzingatiwa uchaguzi mdogo jimbo la Konde  

KITI cha Mbunge wa Jimbo la Konde lililopo Halmsahauri ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba kipo wazi kufuatia kufariki kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo mwishoni mwa mwezi mei mwaka huu. 

Kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 37(1)(b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeandaa uchaguzi mdogo ili kujaza nafasi ya mbunge iliyo wazi katika jimbo hilo.

Akizungumza Jijini Dodoma hivi karibuni, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dk Wilson Mahera amesema Tume imeandaa uchaguzi huo ambao utafanyika tarehe 18 Julai, 2021 baada ya kupokea taarifa rasmi kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai akimtaarifu Mwenyekiti wa Tume, Semistocles Kaijage juu ya kuwepo wazi kwa nafasi hiyo kama inavyoelekezwa na Kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

Tarehe 27 Juni, 2021, Tume kwa kupitia kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Konde, Yasini Jabu Hamis ilifanya uteuzi wa wagombea 12 wanaotokana na vyama 12 vya siasa vyenye usajili wa kudumu. 

Hamis anasema kati ya wagombea hao wanawake ni watatu na wanaume ni tisa. Anawataja wagombea hao kuwa ni pamoja na Sheha Mpemba Faki wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Salama Khamis Omar wa Civic United Front (CUF), Mohamed Said Issa wa Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), Yahaya Mwinyi Ali wa Sauti ya Umma (SAU) na Abdirahim Ali Slum wa National Convention for Constitution and Reconstruction-Mageuzi (NCCR-Mageuzi).

Wengine ni Ali Kassim Hamad wa Tanzania Labour Party (TLP), Mohamed Suleiman Said wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Rashid Hamad Said wa Demokrasia Makini, Salma Abdalla Hamad wa Chama cha Kijamii (CCK), Suleiman Khamis Rashid wa United People’s Democratic Party (UPDP), Issa Shaame Hassan wa National Reconstruction Alliance (NRA) na Fatma Rajab Omar wa Tanzania Democratic Alliance (ADA-TADEA).

Kwa mujibu wa Kifungu cha 46 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kipindi cha kampeni hutangazwa na Tume. Kifungu hicho kinaeleza kwamba kampeni zitaanza siku moja baada ya siku ya uteuzi na kumalizika siku moja kabla ya siku ya Uchaguzi.

Msimamizi huyo wa uchaguzi wa Jimbo la Konde amesema kampeni za uchaguzi kwenye jimbo hilo zimeanza tarehe 28 Juni, 2021 na zinatarajiwa kuhitimishwa tarehe 17 Julai, 2021 na kwamba uchaguzi unatarajiwa kufanyika tarehe 18 Julai, 2021.

Kwa kuzingatia kanuni ya 40 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2020 na kanuni ya 35 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2020 zikisomwa pamoja na kipengele cha 2.1(c) cha Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2020 muda wa kuanza kampeni utakuwa saa 2:00 asubuhi na kumalizika saa 12:00 jioni.

Maadili ya uchaguzi ni zao la makubaliano yaliyoafikiwa baina ya vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wagombea wote ili wakidhi vigezo vya kuteuliwa wanapaswa kusaini fomu namba 10 kukiri kwamba watazingatia na kuheshimu maadili ya uchaguzi katika kipindi chote cha uchaguzi.

Mambo ambayo vyama, wagombea, wafuasi wa vyama na wadau mbalimbali wa uchaguzi hawapaswi kuyafanya kwa mujibu wa maadili hayo ya uchaguzi ni pamoja na matumizi ya lugha za kashfa na matusi kwa wagombea na viongozi wa vyama vya siasa wakati wa kampeni na kuzidisha muda wa kampeni.

Mengine wasiopaswa kufanya ni ukiukwaji wa ratiba ya kampeni, maandamano ya wafuasi wa vyama vya siasa yasiyokuwa na kibali kabla na baada ya kampeni, wafuasi wa vyama kuharibu mabango ya wagombea wa vyama vingine na baadhi ya watendaji wa serikali kuingilia shughuli za vyama vya siasa.

Mambo mengine yanayokiuka maadili ni pamoja na vurugu dhidi ya vyama na wagombea katika baadhi ya maeneo, kubandika picha za wagombea juu ya picha za wagombea wa vyama vingine, wafuasi wa vyama na wagombea kuingilia mikutano ya wagombea wa vyama vingine na kutoa kauli zisizoweza kuthibitishwa.

Maadili haya ya uchaguzi yanaweka misingi ya kuheshimiana, kuzingatia ratiba za kampeni, kuelimisha wanachama wa vyama katika misingi ya kuelewa sera za vyama husika, kutojenga chuki, kushirikiana na kutobeba silaha za aina yoyote katika mikutano ya kampeni.

Kama usemavyo msemo wa Kiswahili, “Penye wengi, pana mengi,” uwepo wa washiriki 12 kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Konde kunasadifu msemo huo na busara kwa wadau wa uchaguzi huu itakuwa ni kuhakikisha kwamba amani na utulivu unakuwepo katika kipindi chote cha uchaguzi.

Pia inatazamiwa kwamba maadili haya ya uchaguzi ambayo yamesainiwa na wagombea wote na ambayo ni zao la vyama vya siasa yatazingatiwa na wadau wote muda wote.

Maadili haya ya uchaguzi yameweka kamati za maadili ambazo zitasimamia na kushughulikia malalamiko yanayotokana na ukiukwaji wa maadili wakati wa kampeni za uchaguzi kuanzia hatua ya kuanza kwa kampeni hadi kukamilika kwa kampeni za uchaguzi. 

Vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi vina wajibu wa kuhakikisha vinatekeleza makubaliano ya kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi ili kuhakikisha kuwa kampeni zinafanyika kwa amani na utulivu.

Kwa uchaguzi huu wa ubunge, kamati ya maadili ngazi ya jimbo chini ya mwenyekiti wake ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo itakuwa na wajibu wa kusikiliza na kufanya uamuzi juu ya malalamiko yatakayowasilishwa na wadau wa uchaguzi kipindi hiki cha kampeni. 

Wajumbe wa kamati hii ni mwanachama mmoja kutoka kwenye kila chama cha siasa chenye mgombea wa ubunge na mwakilishi wa serikali aliyeteuliwa na katibu tawala wa wilaya husika.

Kila mgombea, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, serikali au chama kilichosaini maadili ya uchaguzi na kuweka mgombea wana haki ya kuwasilisha kwa maandishi malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi, saa 72 tangu ukiukwaji huo ulipofanyika kwa kamati ya ngazi husika.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/0120619301feeb2b03673966ee656523.JPG

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Abdulwakil Saiboko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi