loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ilani ya CCM na maeneo maalumu ya uwekezaji 

Ilani ya CCM na maeneo maalumu ya uwekezaji 

ILANI ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ukurasa wa 57 imeainisha masuala kadhaa kuhusu sekta ya viwanda nchini likiwamo la kuendeleza miundombinu ya ujenzi wa viwanda. 

“Hii ni pamoja na kuendelea kujenga kanda na kongani za viwanda zenye miundombinu wezeshi ya ujenzi wa viwanda, katika maeneo ya kimkakati kulingana na upatikanaji wa malighafi katika maeneo hayo, mfano ngozi, bidhaa za ngozi na uongezaji thamani madini,” inasema.

Ilani inaongeza: “Kufungamanisha ujenzi wa kanda maalumu za viwanda na biashara na miundombinu ya kimkakati iliyopo na itakayojengwa ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), Reli ya Kati, TAZARA, Bandari Kavu na upanuzi wa barabara.”

Rais Samia Suluhu alipolihutubia Bunge la Aprili 22, mwaka huu, pia alizungumzia umuhimu wa kufungamanisha sekta ya kilimo na ujenzi wa viwanda na azma ya serikali kuhusu ujenzi wa ukanda na kongani za viwanda.

Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitaifa wa CCM akasema: “Njia nyingine itakayotumika kuongeza kasi ya viwanda nchini ni kutenga na kuendeleza maeneo huru ya biashara, ambapo kipaumbele kitakuwa kwenye maeneo ya mipakani au maeneo yenye miundombinu thabiti ya usafiri, kama reli, bandari na barabara zinazotuunganisha na nchi jirani.” 

“Katika hilo, suala la kongani (mitaa ya viwanda) ni muhimu sana ili kuchochea ujenzi wa viwanda na pia kuiwezesha nchi kunufaika na fursa za kibiashara, ikiwemo kupitia itifaki mbalimbali kama vile EAC (Jumuiya ya Afrika Mashariki), SADC (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika) na Eneo Huru la Biashara la Afrika...”

Hivi karibuni wakati akitoa mada katika Kongamano la Kujadili Uhusiano Kati ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji na Uchumi wa Ndani lililoandaliwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) na Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute), Mkurugenzi wa Uhamasishaji, Uwezeshaji na Uwekezaji wa EPZA, James Maziku anasema: “Kwa mujibu wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Serikali imepanga kuendeleza maeneo maalumu ya kiuchumi manane ambayo ni Pwani, Kigoma, Tanga, Manyara, Mara na Ruvuma.”

Anasema: “Maeneo hayo yameainishwa kwa ajili ya kuwezesha biashara, kuhamasisha mauzo ya nje na kutengeneza ajira…”

Akifungua kongamano hilo lililofanyika Mlimani City, Dar es Salaam likiwakutanisha wadau mbalimbali, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, anasema: “Dhana ya uwekezaji katika maeneo maalumu nchini Tanzania ilianzishwa kama njia ya kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 inayolenga kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi shindani na endelevu kupitia viwanda.” 

“Katika kutekeleza dhamira hii,” Mkumbo anasema: “Mwaka 2002 Bunge lilipitisha sheria kuhusu maeneo maalumu na mahususi kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa kwa mauzo ya nje ya nchi (Export Processing Zones Act) na kuanzisha EPZA chini ya mpango uliojulikana kama Tanzania Mini-Tiger Plan 2020.”

Serikali ya Awamu ya Tatu ilijenga Export Processing Zone (EPZ) na ikapewa jina la Benjamin William Mkapa Special Economic Zone ambayo imeendelea kufanya vizuri kama eneo la mfano katika ukuaji uchumi wa ndani.

Katika mada yake, Maziku anasema: “Tangu kuanzishwa kwa EPZA imehamasisha uwekezaji katika maeneo maalum na kupata matokeo chanya yanayopimika katika kujenga upya sekta ya viwanda.

Anasema: “Thamani ya mitaji ya uwekezaji ni Dola bilioni 2.346; ajira mpya za moja kwa moja viwandani kwa ya Watanzania, zinakadiriwa kufikia 58,007 na thamani ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi inakadiriwa kufikia Dola bilioni 2.518.”

Kuhusu tija iliyopatikana katika Eneo Maalumu la Uwekezaji la Benjamin Willian Mkapa, anasema mtaji halisi uliowekezwa ni Sh bilioni  137.4, mauzo ya nje Sh bilioni 425.36, matumizi yaliyofanywa katika uchumi wa ndani ni Sh bilioni 219.18, kodi ya moja kwa moja iliyolipwa na kampuni mbalimbali ni Sh bilioni 22,67 na ajira zilizotengenezwa ni 3,156.

Anasema: “Ukilinganisha gharama ya mtaji wa Sh bilioni 36.4 na kodi ya moja kwa moja Sh bilioni 22.67 iliyolipwa na kampuni zilizowekeza Eneo Maalumu la Benjamin William Mkapa, utaona serikali imepata faida kubwa….”

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, John Mnali, anasema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, EPZA imetoa leseni kwa kampuni 176.

Anasema hadi Machi 2021, kampuni hizo zimewekeza mtaji wa Dola bilioni 2.5 na kutoa ajira za moja kwa moja kwa watu 58,198.

Katika hotuba yake, Profesa Mkumbo anabainisha mambo muhimu ambayo mwekezaji yeyote, huyazingatia kabla ya kuwekeza katika maeneo maalumu.

 Akasema: “Hayo ni pamoja na masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi, upatikanaji wa ardhi nzuri isiyo na migogoro ya umiliki wala athari kwa mazingira na uwepo wa miundombinu ya ndani kama barabara, maji, umeme na mawasiliano.”

Mengine ni uwepo wa nishati ya uhakika (umeme na gesi) inayopatikana kwa bei ya ushindani, upatikanaji wa rasilimali watu wenye ujuzi na stadi zinazoendana na shughuli wanazofanya viwandani na kwa gharama itakayoweza kuwapa ushindani, na kuwapo miundombinu ya uchukuzi ya kuingiza malighafi viwandani na kutoa bidhaa zinazozalishwa kuelekea katika masoko.

Naye Maziku akataja mahitaji mengine kuwa ni uwepo wa vivutio vya uwekezaji vya kifedha na visivyo vya kifedha. Anasema: “Wawekezaji huzingatia vigezo vyote hivyo sambamba na utulivu wa nchi kisiasa na usalama.”

Profesa Mkumbo anasema kwa kuzingatia mahitaji hayo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu, imeweka kipaumbele katika uendelezaji wa maeneo maalumu ya kiuchumi.

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaoanza kutumika katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, unasisitiza ustawishaji viwanda kama chombo cha mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.

Umeainisha pia maeneo ya kuzingatia na mahitaji ya kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda na yenye ustawi katika maisha ya watu. 

Mkumbo anasema: “Mpango unalenga kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi shindani na endelevu ifikapo mwaka 2025.” 

Anaongeza: “Katika kutekeleza mpango huo, Wizara imedhamiria kuendelea kuweka msisitizo katika kuvutia na kuwezesha uanzishwaji na upanuzi wa viwanda vinavyotoa ajira kwa watu wengi.” 

Anasema hivi ni viwanda vinavyotumia malighafi zinazozalishwa nchini hasa zinazotokana na kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, na madini ili kwanza, kuhakikisha rasilimali hizo zinaongezewa thamani hapa nchini.

“Pili, kuongeza ushiriki wa wananchi katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuwaongezea kipato na hatimaye kuleta uwiano mzuri wa kiuchumi na kijamii baina ya maeneo ya mijini na vijijini.” 

“Tumedhamiria pia msisitizo kuendeleza viwanda vya kimkakati ili kuunganisha sekta mbalimbali na kuongeza uzalishaji na ukuaji mpana wa uchumi, hivyo natoa rai kwa wadau wote, hususani taasisi za serikali, wanaohusika katika kuwezesha uwekezaji wa viwanda katika maeneo maalumu ya uwekezaji, kuhakikisha uwekezaji katika maeneo hayo unafanyika kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa,” anasema Mkumbo.

Anaongeza kuwa, sasa ni wajibu wa kila anayehusika kuhakikisha taratibu hizo haziwi kikwazo kwa uwekezaji na alenge kuhakikisha mwekezaji anahudumiwa haraka.

Profesa Mkumbo anasema: “… Tunataka shughuli za EPZA zifahamike kwa umma na wadau mbalimbali wakiwamo wawekezaji wa ndani na nje ya nchi… Nni vyema kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi nyingine zinazofanya mageuzi ya kiuchumi kwa kujenga uchumi wa viwanda kupitia maeneo maalumu ya uwekezaji, na uzoefu huo uletwe nchini kwa kuzingatia mazingira ya Tanzaniaili mkulima wa kawaida, msindikaji, mjasiriliamali na mfanyabiashara wa Kitanzania; wote wanufaike.

Alisema Rais Samia Suluhu anasisitiza umuhimu wa kuweka msukumo wa mazingira ya uwekezaji na biashara yakiwamo maeneo maalumu ya uwekezaji na mitaa ya viwanda maarufu ‘industrial parks’ ili kuchochea uwekezaji katika maeneo maalumu.

“Awamu hii tutaweka mkazo mkubwa sana Kurasini… Serikali imeamua kuanzia mwaka huu tutangaze eneo hilo la Kurasini (Dar es Salaam) kwa mkazo mkubwa ndani na nje ya nchi, hivyo nitoe mwito kwa wawekezaji wa ndani na nje wachangamkie eneo hili la uwekezaji la Kurasini,” alisema na kuongeza: “Tutaendelea pia Bagamoyo…”

Alisema serikali imepanga kuboresha usimamizi wa maeneo ya uwekezaji ili kuwa na machache yanayosimamiwa kitaifa na EPZA na mengine kuwa chini ya mamlaka za serikali za mitaa.

“Tunataka serikali za mitaa ziwe vituo vya maendeleo ya kiuchumi ili halmashauri zetu ziwe na shughuli za maendeleo ya viwanda na biashara kwa maeneo maalumu ya kiuchumi na machache yabaki kitaifa,” alisema.

Anasema lengo la kuanzisha serikali za mitaa lilikuwa  pia kuunganisha uwekezaji katika maeneo maalumu na uchumi wa ndani ili yachochee ukuaji wa uchumi na kuendeleza urasimishaji wa sekta isiyo rasmi.

Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, Tanzania inazidi kujiunga na jumuiya mbalimbali za kiuchumi za kikanda kama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na nyingine za kimataifa.

“Tunakwenda kuwa washindani kikanda na kimataifa, lazima tujiandae kushindana maana kwa sasa ndani ya EAC hilo ni soko la ndani na tunaelekea ambako sasa hata Afrika itakuwa soko la ndani… Rais Samia ameishatangaza azma ya kuifungua nchi kiuchumi na kibiashara, hivyo lazima tujipange kiushindani na kibiashara; lazima tuwe na vitu vingi vya kuuza nje ambavyo ni bora,” anasema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e9a623e003ee494b9853dda5beb8927f.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi