loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tamisemi yaagiza utaratibu mishahara watumishi wapya

Tamisemi yaagiza utaratibu mishahara watumishi wapya

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeziagiza halmashauri zote kuwa hadi Julai 14 mwaka huu watumishi wote wapya kada ya ualimu na afya wawe wameingizwa kwenye mfumo wa malipo ya mshahara.

Juni 25 mwaka huu, Tamisemi ilitoa orodha ya waajiriwa wapya wakiwemo walimu 6,949 na watumishi wa kada ya afya 2,726.

Katibu Mkuu Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe alilieleza HabariLEO kuwa wakuruguenzi wa halmashauri wanapaswa kutekeleza agizo hilo na akabainisha kuwa watumishi hao wapya hawataruhusiwa kuhama hadi watimize miaka mitatu kwenye vituo walivyopangiwa sasa.

“Wakurugenzi hakikisheni ndani ya muda huo waajiriwa wote wapya mnawaingiza kwenye orodha ya malipo ya mishahara ili wapate mishahara yao. Kuchelewa kuwaingiza kwenye mfumo wa malipo ya mshahara kutasababisha kwanza kuweka madeni ya watumishi ambalo sio lengo la serikali na pia kunaweza kuwapa shida watumishi hao wapya kujikimu kimaisha,”alisema Profesa Shemdoe.

Kuhusu suala la uhamisho alisema “Nasisitiza pia kuwa waliopangiwa vituo hatutawahamisha, kwani miongozo inaelekeza mtumishi hataruhusiwa kuhama mpaka amalize miaka mitatu kwenye kituo husika, hivyo nasisitiza kuwa hakuna tutakayemhamisha kabla ya miaka mitatu.”

Pia alisema kuna miongozo inayoonesha kipindi ambacho mtumishi anatakiwa kukaa kabla ya kwenda kwenye masomo hususani mpaka pale atakapomaliza kipindi chake cha matazamio.

Kwa mujibu wa Profesa Shemdoe, kuongeza elimu ni motisha kwa mtumishi.

Alisema halmashauri zihakikishe zinawapokea watumishi hao wapya ndani ya siku 14 kuanzia Julai Mosi mwaka huu.

Hivi karibuni Profesa Shemdoe alieleza kuwa watumishi hao walianza kuwasili kwenye vituo vya kazi hivyo akaagiza wakurugenzi wa halmashauri watoe mawasiliano ya ofisi ili kurahisisha mchakato huo.

“Kwa mwajiriwa atakayepata changamoto asisite kupiga simu kituo cha huduma kwa wateja cha Ofisi ya Rais- Tamisemi”alieleza kwenye ukurasa wa wizara katika mtandao wa kijamii wa twitter.

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi