loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ugonjwa umeleta taharuki kilimo cha nyanya

Ugonjwa umeleta taharuki kilimo cha nyanya

Kilimo cha  mbogamboga na matunda kwenye kisiwa cha Rwamugasire, kilicho jirani na mji wa Musoma, kwa miaka mingi kimekuwa maarufu sana.

Umbali wa kufika kwenye kisiwa hicho siyo zaidi ya dakika tano, kwa kutumia boti yenye mashine kutokea kwenye mwalo wa Nyarusurya, Kata ya Rwamulimi.

Kisiwa hicho ni shina namba sita linalounda Mtaa wa Nyarusurya. Mjumbe wake, Vitalis Oganga anasema ameishi kisiwani humo tangu mwaka 1968 akiwa na umri wa miaka 22.

Anasema  kilimo ndiyo shughuli kuu kwenye kisiwa hicho kidogo chenye kaya 27, ikifuatiwa na uvuvi.

Anasema nyanya ndilo zao kuu linalolimwa katika kisiwa hicho na limekuwa likichukuliwa kama mkombozi kiuchumi wa wakazi wa kisiwa hicho na kwamba huwaleta kutoka maeneo mbalimbali, ndani na nje ya Mkoa wa Mara.

“Kwa miaka mingi watu wa kisiwa hiki na wengine ambao huja kukodi mashamba, huwa wanapenda kulima nyanya kwa sababu ndani ya muda wa miezi mitatu tu, kama hakujatokea matatizo kama vile magonjwa mtu huwa anajivunia fedha za kutosha,” anasema Oganga.

Kabega Mwendwa anasema alianza kilimo cha nyanya kisiwani humo mwaka 1997 akiishi kwenye nyumba ya kusaidiwa na mtu na hata shamba aliloanzia kilimo lilikuwa la kukodi baadaye akaamua kuwa mkazi na kuanzisha familia.

Anasema mpaka mwaka 2000 kipato cha familia yake kiliongezeka kutokana na kilimo cha nyanya, akaamua kuongeza shughuli ya kujiongezea kipato kwa kutengeneza mitumbwi ili waanze kufanya uvuvi pia.

“Mpaka mwaka 2013 kipato chetu kiliendelea kwenda vizuri mpaka tukanunua ardhi ili kufanyia kilimo badala ya kuendelea kukodi,” anasema Mwendwa.

Mkulima huyo mwenye mke na watoto saba anasema kuanzia mwaka jana (2020) mvua zilizonyesha hazikuiacha familia yake na wakulima wenzake salama.

Anasema mvua hiyo licha ya kusababisha uharibifu kwa mazao yaliyokuwa mashambani, nyumba kubomoka na mali nyingine kusombwa na maji, Mwendwa alipoteza ardhi ambayo alikuwa anaimiliki kisiwani humo kutokana na kuzama majini.

 

Anasema aliamua kukodi ekari moja anayoilipia Sh 120,000 kwa msimu ambao ni miezi minne alimopanda miche 3,000 ya nyanya iliyokuwa tayari imetoa matunda na kumpa matumaini makubwa.

Hata hivyo, kama ilivyo kwa wakulima wenzake, nyanya zimevamiwa na ugonjwa ambao unanyausha mche mzima na hivyo kusababisha nyanya ambazo zilitarajiwa kuvunwa katika wiki chache zijazo kunyauka na hatimaye kukauka.

Ugonjwa huo umesababisha hasara kwa wakulima wengi, kiasi cha wengi kutelekeza mashamba yao huku wakiapa kutorejea tena kulima kwenye kisiwa hicho.

“Ugonjwa unaoitwa mnyauko tunaufahamu, lakini huu unakuja kwa namna tofauti kwa sababu unakausha mpaka shina tena unasubiri mmea umeishazaa matunda mazuri yenye afya ndipo unaanza kushambulia mche mmoja baada ya mwingine mpaka shamba zima linakwisha,” anasema Mwendwa.

Anasema ingawa hawezi kuacha kilimo, hata yeye amepoteza matumaini ya kuendeleza kilimo kisiwani humo hivyo anamuomba Mungu amsaidie apate angalau Sh 1 milioni kwenye mavuno ya awamu hii ili akatafute shamba kwingineko.

Kigoma ni mkoa ambao unatajwa zaidi na wakulima hao, kwamba wanaweza kuhamishia shughuli zao huko kutokana na uwepo wa ardhi nzuri zaidi.

Mkulima mwingine, Kiumbe John anasema ametelekeza shamba lake la ekari moja, alilotumia Sh milioni 2.5 kulitayarisha lakini ugonjwa huo umemfanya aondoke mikono mitupu.

“Siwezi kuacha kilimo kwa sababu kinalipa na sina kazi nyingine, lakini sitathubutu kurudi kisiwani humo. Nitatafuta maeneo mengine,” anasema Kiumbe.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyarusurya, Iddy Changara anasema anafanya mawasiliano na ofisa kilimo wa kata hiyo ili waende katika kisiwa hicho kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.

Ofisa kilimo, Refaya Wakara anasema hajafika kwenye mashamba hayo kutokana na changamoto ya usafiri.

Hata hivyo, anasema kutokana na maelezo anayopata, kwa uzoefu wake anaamini ni ugonjwa ambao kitaalamu unafahamika kama Fusarium Wilt (mnyauko).

Ofisa kilimo huyo anasema, kama ni ugonjwa huo namna rahisi ya kuumaliza ni shamba lililopatwa ugonjwa kutolimwa nyanya kwa muda usiyopungua miaka mitano ingawa wakati mwingine njia ya kubadilisha mazao hushauriwa pia.

Anasema  zao linalopendekezwa  kulimwa kwenye ardhi iliyoshambuliwa na ugonjwa huo ni vitunguu maji.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/4642b8630c326e76eb1a477fc4b990d9.JPG

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Editha Majura

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi