loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mnataka kunufaika? Badilikeni kifikra

Mnataka kunufaika? Badilikeni kifikra

AKIZUNGUMZA na wananchi wa Lindi kuhusu mradi mkubwa wa usindikaji wa gesi asilia (LNG), Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, anawataka kubadili fikira ili kutumia fursa zilizopo katika mkoa huo kubadili maisha yao kutoka kuwa duni na kuwa bora zaidi.

Ndemanga alitoa angalizo hilo wakati akifungua warsha iliyoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali mkoa wa Lindi la (LANGO) iliyolenga maandalizi ya ujio wa mradi mkubwa wa usindikaji gesi asilia (LNG) mkoani humo.

Mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa baadae mwaka huu, lakini kwa mujibu wa mkuu wa wilaya uzoefu unaonesha kwamba pamoja na mabilioni ya fedha kuingia katika mkoa huo kupitia kilimo cha korosho na ufuta, mabadiliko katika maisha ya wananchi yameendelea kutoonekana.


Mkuu huyo wa wilaya anasema ili kupisha mradi huo wa LNG, watu wa Kata ya Mbanja walilipwa fidia ya Sh bilioni 5.2 lakini ukiangalia fedha walizopokea wananchi kutokana na fidia hizo hazijaonyesha kuleta mabadiliko ya maisha ya wakazi wa maeneo hayo.

Anasema Lindi inaingiza wastani wa Sh bilioni 170 kila mwaka kutokana na mazao mbalimbali na huduma lakini maisha ya wananchi wake bado hayaoneshi uwapo wa kiasi hicho kikubwa cha pesa kwani kila msimu wa mauzo ukimalizika watu wapo vile vile!

Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2009, zilikuwa zinaonesha kwamba wastani wa pato la Mtazanzania kwa mwaka wakati huo lilikuwa shilingi 767,948 lakini  mwaka 2015 liliongezeka hadi kufikia shilingi 1,901,044 sawana ongezeko la asilimia 148. Hii ni wastani wa ongezeko la asilimia 21 kwa mwaka.


Pia pato la Mkoa wa Lindi limeendelea kuongezeka kutoka shilingi 695,361,000 mwaka 2009 hadi kufikia shilingi 1,690,403,000 mwaka 2015. Hili ni ongezeko la silimia 143 sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 20 kwa mwaka.

Pamoja na kuwepo kwa ongezeko hilo la kipato mkoani Lindi, bado changamoto ya umaskini miongoni mwa wananchi iko vilevile. Ni kutokana na hali hiyo Mkuu wa Wilaya anaona iko haja ya wananchi kubadilika kifikira kwa kutumia fedha wanazopata kubadilisha maisha.

Hatua wanazoshauriwa kuchukua ni pamoja na kuweka akiba na kuzidi kuwekeza kwenye masuala ya maendeleo ikiwemo kufungua mashamba bora zaidi, kusomesha watoto, kujijengea nyumba bora na mengine ya aina hiyo badala ya baadhi ya wanaume kutumia ongezeko la mapato kwa kujiongezea wake.

Kutokana na mazoea ya kuingiza fedha na kutoangalia kinachostahili kufanywa ili kuzidi kuimarika kiuchumi, Mkuu huyo wa wilaya anaona matumaini makubwa kwa LANGO kupeleka elimu mapema zaidi kuhusu sekta ya gesi na fursa zake na kuwataka wasiishie kuwaonesha tu wananchi fursa katika mradi huo wa LNG bali pia wawafundishe kubadilika kifikra.

“Twendeni tukabadili fikra za wazawa…  Zibadilike kwelikweli kwa kuona kwamba fursa zinapokuja tuzikamate. Lakini tusiishie hapo tu pia tuhakikishe fursa hizi zinabadili maisha ya wazawa,” anasema Ndemanga.

Anasema kwa sasa wakati wananchi wanasubiri mradi huo mkubwa uanze ipo haja kwa wananchi kuanza kutumia fedha kuanza ujenzi wa majengo ya kupanga, kuendesha mashamba ya mboga na vyakula na ufugaji wa kuku ili kutosheleza mahitaji ya mradi huo mkubwa unaotarajiwa ambao ukitumiwa vyema utabadili kwa kiasi kikubwa maisha ya wananchi wa Lindi.

Mkuu huyo wa wilaya anasema bila kubadili fikira za wananchi hakutakuwa na maendeleo kwani historia katika utumiaji wa fursa mkoani Lindi haitoi sura njema kwa wananchi.

“Niliwauliza watu wa Dangote kwa nini wanaagiza chakula kutoka nje wakaniambia kwamba walitoa zabuni kwa mtu wa Lindi kwa kila wiki kuleta kuku elfu mbili lakini alipeleka mara moja, mara ya pili pungufu na mara ya tatu hakutokea kabisa,” anasema Ndemanga.

Anasema masuala kama hayo ndio LANGO wanastahili kuyafanyia  kazi kwa maana ya kuwaandaa wananchi kifikra namna watakavyonufaika na fursa na pia kubadilika na kuwa wachakarikaji.

Shirika  la Lango linaendesha mafunzo yenye lengo la kuwafanya wananchi kujitambua huku likielimisha waraghibishi watakosambaza elimu kwa wananchi kuhusu Sera ya Ushirikishwaji wa Wazawa. 

Mafunzo hayo yanalenga kuiandaa jamii kunufaika na fursa zitakazoambatana na uwepo wa mradi wa kuchakata gesi asilia, unaotarajiwa kujengwa kwenye kata ya Mbanja, ndani ya Manispaa ya Lindi.

Mafunzo hayo kupitia mradi wa “Uwajibikaji kupitia Raia Wahamilifu katika Usimamizi wa Sekta ya Gesi Asilia na Mafuta mkoani Lindi”, yanafadhiliwa na shirika la Oxfam-Tanzania.

Ni mafunzo ambayo yamelenga kutoa msisimko wa kuonesha wajibu wa wanajamii na watoa uamuzi kuhusu mustakabali wa jamii. Mradi huo unaotarajiwa kutoa ajira mbalimbali za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja (huduma) kama za chakula.

Mtendajik Mkuu wa Lango, Michael Mwanga anasema ni wajibu wa taasisi yake kusaidia wananchi kujitambua na kujitathmini ili kutumia fedha wanazopata kwa busara na kwa maendeleo yao na kwamba kile anachokisema Mkuu wa Wilaya ndicho hasa wanachokifanya.

"Tutaenda kufanya tathmini kama Lango kuona zile fidia ambazo tayari zimeshalipwa na serikali wananchi ambao wamezipata wamenufaika nzao kivipi. Tuone  wamezielekeza katika maeneo gani na kama wameshindwa ndipo sasa tutaawataka wafunguke kwa kujiandaa na mradi huu mkubwa," anasema Mwanga.


Anaongeza: "Tunawataka waraghibishi tulioanza nao kuhakikisha wanatumia vyema fursa hii kuchukua elimu kuweza kusambaza ujuzi huu kwa jamii zetu zinazotuzunguka kwenye maeneo yetu. Tunawataka wachukue jukumu la kuelimisha wanaowazunguka kwenye maeneo yao walikotoka.

Ninaamini kwa kutumia rasilimali ndogo tulizonazo tusingeweza kufikia jamii kubwa, lakini kupitia kwao tunaweza kufikia jamii kubwa zaidi. Ni vyema tukubaliane kwa pamoja kubeba jukumu la kuelimisha wengine kuhusu yale tuliyowafunza," anasema Mwanga.

Sandali Mpelembwe, mtendaji wa kata ya Mbanje anasema ni wakati mwafaka sasa Manispaa ya Lindi kuandaa wataalamu watakaokua wanatoa elimu sahihi ya kitaalamu kwa wananchi kuhusiana na mradi huo na fursa zinazoambatana nao ili waweze kuzitumia.


Mafunzo hayo ambayo yalilenga kujenga uelewa kwa makundi hayo kuhusu sera ya ushiriki wa wazawa na namna wazawa wanavyoweza kushiriki kwenye nyanja tofauti katika sekta ya uziduaji gesi asilia.

Yalilenga pia kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa wadau kutoka ndani ya Manispaa ya Lindi kuhusu namna jamii zetu zinaweza kunufaika na uwepo wa miradi mbalimbali ya kimkakati katika tasnia hii ya gesi asilia, hususani mradi wa LNG.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/80aaa179825f58911d670d985eb049bf.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi