loader
Dstv Habarileo  Mobile
'Tumenufaika na mgodi wa   Buzwagi unaofungwa, lakini...'

'Tumenufaika na mgodi wa  Buzwagi unaofungwa, lakini...'

“KUENDESHA mashine aina ya Liner Handler migodini kunampatia mwendeshaji kiasi kisichopungua Sh 300,000 kwa siku. 

Hii ni mashine inayotumika kukarabati mtambo maalumu wa kusaga mawe makubwa ya dhahabu, ujulikanao kama Sag mill, wanasema baadhi ya vijana waliokua waajiriwa katika mgodi wa Buzwagi, Wilayani Kahama mkoani Shinyanga, uliopo hatua za mwisho kufungwa.

 

Wanathibitisha kwamba ni kazi inayofanyika kwa saa chache tu, tena kwa msimu wa siku tano hadi saba kwa mwezi, lakini wapo wanaolipwa hadi Sh 500,000, kwa siku, kulingana na eneo analohudumu mtu.

 

“Huu ndio urithi tunaoachiwa na Buzwagi. Sasa tuna uwezo wa kuendesha mitambo mbalimbali migodini bila usimamizi wa mtaalamu yeyote kutoka nje ya nchi,” anasema Dotto Msaka, mmoja wa waliokuwa waajiriwa wa Buzwagi kupitia Kampuni ya kitanzania ya Magare, inayojihusisha na uhandisi wa umeme na mitambo viwandani na migodini.

 

Masaka anasema kwamba si tu kuvuna ujuzi, bali pia wamepata mitaji ya kuwekeza katika shughuli za ujasiliamali, ikiwemo kununua pikipiki za kubeba abiria, maarufu kama ‘bodaboda’ kutokana na kipato kizuri walichokua wakilipwa kutokana na kazi hiyo.

 

Anakiri kwamba ni kazi nzito inayohitaji ujuzi wa kutosha, maarifa, muda na nguvu kwani ukarabati wa ‘Sag mill’ huhusisha kuondolewa kwa vifaa vilivyochakaa na kuwekewa vipya, wakati kifaa kimoja kina uzito usiopungua tani moja.

 

Anapongeza juhudi za serikali kuweka mazingira bora yaliyokaribisha wawekezaji katika migodi, na wao (wawekezaji) wakaweza kushirikisha kampuni za ndani, hatimaye vijana wakapata fursa za kukuza ujuzi na kupata ajira.

 

Anasema kushirikisha kampuni za ndani kuna faida lukuki, ikiwemo wazawa kujifunza teknolojia mbalimbali za kisasa, na hivyo kuondoa utegemezi wa wataalamu kutoka nje.

 

Yeye ni miomgoni mwa vijana waliopatiwa ujuzi na wataalamu kutoka nje ya nchi, hasa Afrika ya Kusini na Australia, waliokuwa wakialikwa na kampuni ya Magare kuja nchini kwa ajili ya kazi hiyo.

 

Hata hivyo, licha ya kujivunia kupata ujuzi ambao wanauita mtaji wao wa kudumu, vijana hao hawana vyeti vya kuwawezesha kupata ajira maeneo mengine.

 

Anasema hiyo ni kutokana na ukweli  kwamba kampuni yao haihusiki na utoaji vyeti kwani haitoi mafunzo ya moja kwa moja, bali kupitia watalaamu kutoka nje ya nchi.

 

“Tunaishauri serikali kuanzisha chuo maalumu cha mafunzo ya kuendesha mitambo migodini ili wanaofuzu wapatiwe vyeti na kutambulika rasmi katika tasnia hii, na hivyo kukamata fursa za ajira ndani na nje ya nchi,” anasema.

 

Thobias Inncocent, yeye anathibitisha kwamba vijana wamenufaika ipasavyo kwa kupata ujuzi, na anathibitisha kwamba hata endapo serikali itaamua kuwekeza yenyewe migodini hakutakuwa na changamoto ya uhaba wa wataalamu wa kuendesha mitambo nchini.

 

“Tuliitumia ipasavyo fursa ya kuwepo mgodini kwa kujifunza kila walichifanya wataalamu kutoka nje, na tumefuzu vizuri, changamoto ni vyeti tu,” anasema.

 

Mkurugenzi wa Magare, Mabula Magangila anaunga mkono hoja ya uwepo wa chuo cha mafunzo ya kundesha mitambo migodini, kwa upatikanaji wa wataalamu wengi wazawa.

 

Anasema  fahari yake ni kuona Watanzania wenzake wanapata maarifa ya kutosha kuendesha shughuli mbalimbali za kitaalamu kwa manufaa yao binafsi na nchi yao.

 

Anakiri kwamba kuagiza wataalamu kutoka nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo kwa Watanzania kuna gharama kubwa lakini ilimbidi kufanya hivyo ili kuandaa wataalamu wa ndani, hivyo anaiomba seriali kuunga mkono juhudi kwa kuanzisha chuo.

 

Hata hivyo, wakati wakisubiri uwepo wa chuo nchini, Kampuni yake itaendelea kuagiza wataalamu kutoka nchi zinazozalisha mitambo ya migodini  kuwapatia vyeti vijana ambao tayari wamejipatia ujuzi.

 

Ni wataalamu wa kampuni zile zile zilizohusika kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa Magare zitakazohusika kwa utoaji vyeti.

 

Alipoulizwa kuhusiana na vijana kupoteza ajira baada ya kufungwa kwa Buzwagi, Mkurugenzi huyo anasema kampuni yake inahudumu katika takribani migodi yote iliyopo Kanda ya Ziwa na kwamba katika miradi ya kimkakati kama ya Ujenzi wa MV Mwanza na reli ya kisasa (SGR), ujuzi wa vijana wake bado unahitajika.

 

Kampuni imekua pia ikiajiri vijana wanaohitimu katika vyuo vya ufundi stadi  (VETA) na kuwashirikisha katika miradi hiyo ya kimkakati.

 

Magangila anasema lengo si kujipatia kipato pekee bali pia kuendelea kukuza ujuzi kwani takribani kila hatua kwenye miradi inahusisha teknolojia mpya.

 

Katika mradi wa ujenzi wa MV Mwanza na SGR, anasema vijana wa Magare wanahusika pamoja na kazi zingine, uchomeleaji, utandazaji wa miundombinu ya maji na umeme pamoja na upakaji rangi.  

 

“Vijana wangu hawajapoteza ajira kabisa (kutokana na Buzwagi kufungwa) kwani bado wanahitajika katika migodi ya North Mara na Bulyankhulu ambayo mchimbaji wake ni huyohuo aliyekua akichimba Buzwagi,” anasema.

 

Mkuu wa Wilaya Kahama, Festo Kiswaga anathibitisha kwamba taratibu za kuufunga mgodi wa Buzwagi ziko mwishoni ambapo baadhi ya wafanyakazi wameshalipwa stahiki zao na kutawanyika.

 

Anasema tarehe rasmi ya kufunga ilikuwa 30 ya mwezi uliopita na kwamba mwekezaji alizingatia hilo, lakini akaomba siku zaidi, hadi mwisho wa mwezi huu ili kukamilisha baadhi ya shughuli, ikiwemo kusaga mawe ya dhahabu yaliyosalia.

 

“Ombi limeshatumwa kwa taasisi husika za juu ambazo kimsingi ndizo zenye mamlaka ya kutangaza rasmi kufungwa kwa mgodi,” anasema.

 

 

Anasema uwepo wa mgodi huo wa Buzwagi umeleta faida nyingi zitakazoendelea kupatikana kwa mtu mmoja mmoja, jamii nzima ya Kahama na serikali kwa ujumla.

 

Mojawapo ya faida hizo endelevu anasema ni majengo takribabi 300 yalijengwa na mwekezaji na yanatarajia kuwa sehemu ya taasisi yoyote ya elimu, hasa chuo kikuu, baada ya shughuli za kufukia mashimo ya machimbo na kurudisha mazingira katika mwonekano wake wa zamani.

 

Anasema ipo pia mipango ya mamlaka ya maji mkoa kuhamia eneo hilo kutoka na uwepo wa miundombinu ya maji safi na salama iliyowekwa na mwekezaji, ikiwemo tangi lenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita milioni 1.5.

 

Anasema baadhi ya maofisa wa Buzwagi, akiwemo meneja wa mgodi wataendelea kuwepo nchini kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, kusimamia shughuli za kuweka mazingira sawa na kumalizia taratibu  za kutoa faida kwa jamii (CSR) inayozunguka mgodi huo.

 

Mojawapo ya shughuli kubwa zitakazofanywa anasema ni upanuzi wa uwanja wa ndege utakaoweza kupokea ndege kubwa.

 

“Kwa ujumla wana Kahama na jamii zingine za jirani wataendelea kunufaika kama kumbukumbu ya uwepo wa mgodi huu. Vijana waliopata ujuzi wa kuendesha mitambo migodini watendelea kunufaika na ajira katika migodi mingine pia.”

 

Anaeleza zaidi kwamba, kupitia mfumo wa CSR, tayari jamii imenufaika na mgodi huo katika maeneo kadhaa, ikiwemo kilimo,  afya na elimu ambapo takribani madarasa 300 yamejengwa na fedha kutoka kwenye mgodi huo unaofungwa na yanatumika.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/65036c0575dc96345baa2543b5bbf1e6.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Abela Msikula

1 Comments

  • avatar
    Adrian
    13/07/2021

    MBONA HAWAJAELEZA KWA NINI MRADI HUO UMEFUNGWA ?

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi