loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kuku wa 500,000/-, yai 10,000/- washangaza wengi Sabasaba

Kuku wa 500,000/-, yai 10,000/- washangaza wengi Sabasaba

WASHIRIKI wengi wa Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) wamevutiwa na ubunifu mbalimbali katika maonesho hayo pamoja na uwepo wa bidhaa za viwango vya kimataifa.

Katika maonesho hayo maarufu Sabasaba yaliyofikia tamati jana, bidhaa mbalimbali zilioneshwa za ndani na nje ya nchi, ikiwamo kuku wenye uzito wa kilo nne hadi tano wanaouzwa kwa Sh 500,000 mmoja.

Mbegu ya kuku hao imetolewa nchini Malaysia na kupitia kampuni ya Watanzania ya Platnum Kuku yenye shamba la kuku Bagamoyo, mkoani Pwani na ofisi Mwenge na Tegeta, Dar es Salaam. Yai moja la kuku hao huuzwa Sh 10,000. 

Baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo, Verani Mangesho na Salimu Abdallah walisema wamevutiwa na aina hiyo ya kuku na wanajipanga kwa mtaji na eneo ili wawanunue na kufanya ufugaji wa kibiashara. 

Akizungumza na HabariLEO katika banda la kampuni hiyo kwenye maonesho hayo huku watembeleaji wa maonesho hayo wakiwashangaa kuku hao wakubwa, Meneja Mauzo wa kampuni hiyo, Ray Namara alisema walichukua mbegu ya kuku mbalimbali wakiwamo Brahama kutoka Malaysia na kuwaleta nchini.

Alisema kilichowasukuma kuleta mbegu hiyo ni kutokana na faida za kuku hao ikiwamo nyama nyingi kutokana na kuwa na uzito mkubwa na utamu wake. 

Alisema kuku mtetea hutaga mara mbili kwa mwaka mayai 15 kwa mara moja, hivyo kutaga mayai 30 kwa mwaka, wakati kuku wa kawaida wa kienyeji hutaga zaidi ya mayai 50 kwa mwaka.

“Hawa kuku ni wapya, ndio tumewaleta sasa. Tuliwanunua jogoo na mtetea kwa ajili ya mbegu Sh milioni 1.5 wote na tangu watotolewe wana miezi minane sasa hivi, wana nyama nyingi na wanakuwa kwa haraka, mtetea ana kilo nne mpaka nne na nusu na jogoo anakuwa na kilo tano mpaka sita,” alisema.

Alisema walipata soko la kuwaleta kuku hao mwaka jana na sasa wanapambana kuwazalisha kwa wingi kwani wanasoko kubwa. 

Alisema kifaranga cha wiki mbili huuzwa kwa Sh 15,000 hivyo ili mtu apate mbegu atalipa Sh 30,000 na cha mwezi mmoja ni Sh 30,000, huku  mbegu ya mtetea na jongoo ikiwa ni Sh 60,000.

Kwa mujibu wa Namara, jogoo wa aina hiyo ya kuku, hapandi kuku mwingine hivyo kuwa na uhakika na aina ya vifaranga na si mkorofi kama jogoo wa Kuchi.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi