loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tuilinde Tanzania. Hatuna nyingine

Tuilinde Tanzania. Hatuna nyingine

“NIWAOMBE waandishi wa habari muitangulize Tanzania kwanza. Siku ikiharibikiwa Tanzania na nyinyi mtakuwa mmeharibikiwa pamoja na wale waliowapanga kuyaandika yale mnayoyaandika… 

“Unaweza ukawa unamchukia mtu fulani lakini kamwe usiichukie Tanzania. Multiplying effect yake ni kubwa… Kwa hiyo, hiyo ni meseji kwenu kwamba kalamu zenu mkizitumia vizuri mtawasaidia watanzania… Na ndugu zangu wa vyombo vya kutoa haki, katangulizeni Tanzania”. 

Maneno hayo yanayopaswa kuandikwa kwa wino wa dhahabu yalisemwa Rais wa Awamu ya Tano, Johhn Magufuli na kwa hakika yanashabihiana na yale aliyosema Rais Samia alipokuwa ziarani Morogoro.

Rais Samia alisema: “Niwaombe tuzidi kulinda amani na utulivu wa nchi yetu. Jinsi tunavyokaa kwa salama na amani ndivyo na mendeleo yatakuja. Niwaombe sana ndugu zangu, vijichokochoko vimeanza, naomba msivipokee. Wanaokuja na vichokochoko walishajua matumbo yao yanajaaje. 

“Naombeni msije ingia kwenye huo mkenge. Maana pakichafuka ni wewe utakayekaa ndani na watoto wako… Kwa hiyo niwaombe sana ndugu zangu tulinde amani yetu, nchi yetu itulie tuedelee na maendeleo yetu.”

Kauli hizi zote mbili zinasadifu maneno yaliyo kwenye wimbo wa Tanzania nakupenda kwa moyo wote hasa kwenye beti la pili inayosema: Tanzania, Tanzania nakupenda kwa moyo wote. Nchi yangu Tanzania, jina lako ni tamu sana. Nilalapo nakuota wewe, Niamkapo ni heri mama wee, Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote.

Inawezekaa kwa namna moja au nyingine umewahi kuimba wimbo huu au inawezekana pia unauimba na kuusikiliza kila siku. Je, huwa unafikiria maana ya msingi iliyomo kwenye wimbo huo na kuifanyia kazi? Ni wimbo unaolenga kuongeza uzalendo baina ya watanzania kwa nchi yetu.

Suala la mapenzi ya nchi kabla ya mapenzi ya mtu binafsi ni jambo muhimu sana kwa mstakabali wa taifa letu. Hata hivyo, kwa nyakati tofauti kupitia kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kumekuwa na mijadala ambayo kwa wakati mwingine inaweza kuhatarisha amani na umoja wa nchi yetu.

Mbya zaidi kuna wakati hata baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa wakitumika pasipo aidha kujua au kwa kujua. Kwa nyakati tofauti wanaonekana kutoa mitazamo yao ambayo kimsingi inaweza kuhatarisha mstakabali wa taifa letu kwa namna moja au nyingine. 

Swali ni je, wanaofanya haya yote wanalenga nini? Wanafaidi nini? Wametumwa na nani?

Mpenzi msomaji, ukiangalia katika kauli zote mbili za viongozi wa nchi yetu nilizozitoa hapo awali kwenye makala haya, wote wanabainisha pasi na kificho kwamba wanaotumika kuichafua nchi yetu na kuondoa hali ya amani wanakuwa wametumwa na wafadhili ambao sisi kama wananchi wa kawaida hatuwajui wala kuwaona! 

Je, ni kweli kwamba kuna wanasiasa wanapewa fedha ili waharibu amani ya nchi yetu? Inawezekana wanafanya hivyo ili wapate madaraka, je wakisha kupata watatekeleza maslahi ya nani?

Dhana ya usaliti baina ya wanasiasa haijaanza leo, katika miaka ya 1870 mtemi Mkasiwa alijiunga na Waarabu ili kumkabili Mtemi Milambo ambaye alikuwa ameshikilia njia kuu ya kibiashara ya Ujiji. 

Mtemi Mkasiwa alifanya hivyo ili kumdhoofisha kiongozi mwenzake wa Kiafrika ambaye alitumia muda wake mwingi kupigania heshima ya Mwafrika na kuwafanya wageni waliokuja kwenye tawala yake kulipa kodi kwa maslahi na maendeleo ya wana Urambo. 

Hata hivyo, histroia inaonesha kwamba washirika hao walishindwa vibaya dhidi ya Mtemi Milambo kwa kuwa alikuwa amejipanga vyema kijeshi. 

Kisa hiki kinanifanya nilinganishe na mazingira tuliyopo kwa sasa. Inawezekana kukawa kunafanyika baadhi ya mambo ambayo huyapendi kisiasa kwa kuwa hayaendani na itikadi zako, lakini je, ndio uharibu amani ya nchi yako? Ndio hadi uwachafue viongozi wako wa kitaifa? 

Vitabu vyote vya maandiko matakatifu vinahimiza kuheshimu mamlaka zilizo duniani kwa kuwa zimewekwa na Mungu. Ya nini kutunishiana msuli utadhani wote ni jamii ya samaki aina ya kambale?

Itatupungukia nini tukiamua kuungana kama watanzania kuijenga nchi yetu kwa maslahi yetu sote? Kwanza tumetoka kwenye kipindi kigumu sana cha kuondokewa na kiongozi mkubwa mbeba maono wa taifa letu. Kiogozi ambaye kwa muda mchache alijitahidi kufanya mambo makubwa sana.

 

Ni wazi kwamba hatukuwahi kupitia hali kama hiyo lakini sasa vkwa ile imetokea yatupasa kama Watanzania kuungana katika kuleta maendeleo ya nchi yetu. Maendeleo haya ni kwa faida yetu sote.

Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipata kusema: “Tutaijenga nchi hii kwa faida yetu wenyewe. Akipatikana mtu wa kutusaidia tutashukuru. Lakini kazi ya kujenga nchi hii kwa manufaa ya watanzania wote, ni kazi ya watanzania wenyewe. Si kazi ya mtu mwingine.”

Hatuwezi kufanikiwa katika hili iwapo mapenzi yetu kwa taifa letu ni haba! Hatuwezi kuendelea iwapo kila mtu anajiona yeye ndio yuko sahihi kwenye kile anachokiamini! 

Inawezekana kuna wakati tunatamani mambo kadha wa kadha yafanyike lakini je, ndo mkoseshe amani watanzania ili mfanikiwe kuyapata? Tutapungukiwa nini iwapo kwanza kama watanzania tutajikita kwenye kukuza uchumi wa nchi yetu kisha mengine yaendelee?

Afrika kwa kiasi kikubwa imeendelea kubaki chini ya ukoloni ndani ya uhuru kutokana na kuwa na uchumi wa chini sana. Uhuru siyo kamili iwapo uchumi wetu unamilikiwa na watu wachache huku pia ukihujumiwa na mabeberu.

Nchi kama China zimejiokoa kutoka ukoloni kutoka na kukuza uchumi wao kwa kasi. Cha kushangaza kweye nchi yetu kiongozi akisema watu tufanye kazi pasipo kujali chama cha mtu wala dini; baadhi wanaona kama wanapotezewa muda wa kuingia madarakani hivyo wanasababisha taharuki kupitia mitandao ya kijamii na hata kwenye vyombo vya habari vilivyopo.

Ni lini Watanzania tutatambua dhana ya kutanguliza mapenzi ya nchi yeu kabla ya kitu kingine chochote? Ni lini tutaweza kuzungumza lugha moja na kuijenga nchi yetu? Ni lini tutabadilisha mitazamo yetu isiyo rafiki kwa maendeleo ya nchi yetu? Jamani, hatuna nchi nyingine zaidi ya hii.

Nchi hii ni yetu sote na tunapaswa kuipenda na kuilinda na kama ambavyo amekuwa akihimiza Rais Samia, tukosoe kama tuna la kukosoa kwa lugha ya kiungwana na wakati huo huo tukipendekeza suluhisho.

Mwandishi ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni   +255-71224-6001,   HYPERLINK "mailto:flugeiyamu@gmail.com" flugeiyamu@gmail.com

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/8f1e6eaf6d67d0e2cdf6a39146c17d4b.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Felix Lugeiyamu 

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi