loader
Dstv Habarileo  Mobile
Hoja ni katiba mpya au taasisi imara?

Hoja ni katiba mpya au taasisi imara?

MJADALA uliopo hivi sasa nchini kuhusiana na katiba mpya unaonekana kushika hatamu miongoni mwa makundi ya jamii na vyama vya siasa. 

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan aliwaomba wananchi hasa wanaodai katiba mpya, 'wampe muda ajenge uchumi kwanza'. Bila shaka kauli hii haikueleweka na wanaohanikiza suala la katiba mpya na hivyo kuendelea kuzua mjadala mpana.

Nae Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisisitizia kuwa "Katiba tuliyo nayo ni imara kwani imetuvusha katika kipindi kigumu tukiwa salama," hoja hizi na zile za wanaotaka mabadiliko ya Katiba zinanifikisha kwenye kujiuliza, 'Hoja ni Katiba Mpya ama Taasisi Imara?'

Nitatolea mifano ya nchi mbalimbali kama Kenya, Afrika ya Kusini, Ethiopia na Uingereza ili kuona tatizo lipo wapi hasa. Je, hoja iwe Katiba au taasisi imara?

Maendeleo endelevu

Ili tuweze kupata upana wa hoja ni vema kwanza tupambanue taasisi imara ni ipi? Je, inatokana na Katiba? Je, Katiba iliyopo haileti uwezekano wa kujenga taasisi imara kama ilivyoainishwa kwenye lengo namba 16 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs)?

Kwa kuanzia lengo namba 16 la SGDs linahusu Amani, Haki na Taasisi Imara' na kwa tafsiri yangu linaelezwa kama ifuatavyo: Kukuza jamii yenye amani na jumuishi kwa maendeleo endelevu, kutoa nafasi ya haki kwa wote, kujenga taasisi madhubuti, zinazowajibika katika ngazi zote.'

Kutokana na maelezo ya malengo hayo hapo juu tunaweza kupata tafsiri ya taasisi imara (strong institution) kwamba taasisi imara inatazamwa katika sura kuu mbili;

Mosi, taasisi imara ni zile zinazowawezesha wananchi kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa amani na pili ni zile zinazoweza kutoa haki kwa wote kwa kuzingatia usawa kama ilivyofafanuliwa na Jopo Kuu la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 2015.

Taasisi imara zinaweza kuwa za kiserikali ama za zisizo za kiserikali. Kwa msingi huo basi tunaweza kubaini kuwa taasisi imara inatazamwa katika maeneo tisa ambayo ni pamoja na ujumuishi, uwajibikaji na uwazi.

Maeneo mengine ni utawala wa sheria, kupambana na rushwa, kutoa haki, usimamizi wa amani, kutoa huduma za msingi na umiliki.

Haya yamebainishwa pia kwenye taarifa ya Umoja wa Mataifa kupitia Idara yake ya Masuala ya Jamii na Uchumi (DESA) pale walipoeleza kwenye ripoti yao ya mwaka 2019.

Taarifa hiyo na kwa tafsiri yangu isiyo rasmi inaonesha kuwa, Serikali ina jukumu muhimu katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Kwamba pasipokuwa na taasisi madhubuti, zinazowajibika na jumuishi, hakutokuwa na muendelezo katika utoaji wa huduma muhimu kama vile afya, elimu, maji safi na salama au usafiri.

Kodi, miundombinu, rushwa

Mbali na haya yaliyoelezwa na DESA, Abdalla Hamdok katika andiko la Steve Mugerwa la mwaka 2003 lililobeba jina 'Kuhuisha Taasisi za Afrika yeye anabainisha pia masuala ya ujenzi wa miundombinu kwenye maeneo ya vijijini na kulinda maskini na makundi yaliyo katika hatari.

Pia anahimiza kuhusishwa kwa wananchi katika kufanya maamuzi katika masuala yanayowaathiri kupitia wabunge madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa) kuwa ni sehemu ya taasisi imara inayowajibika kwa watu wake. 

Salusi yeye katika chapisho hilo hilo anaeleza namna kutamalaki kwa rushwa kunavyoifanya Nigeria ipoteze sura ya taasisi imara. 

Sambamba na hayo, ripoti iliyotolewa na Shirika la kimataifa la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (Organisation for Economic Co-operation and Development-OECD) mwaka 2013 ilibainisha pia ujenzi wa miundombinu, usimamizi na ukusanyaji mzuri wa kodi kuwa ni sehemu ya ujenzi wa taasisi imara.

Kwa mujibu wa OECD, kwa miaka mitano kuanzia 2007 mpaka 2011 uelewa kuhusu kulipa kodi ulifikia asilimia 34 tu. Je, hali ikoje hivi sasa?

 

Katika kukazia dhana hii ya kujenga taasisi imara tulimsikia Rais Samia Suluhu Hassan akisisitiza kuwa hataki kodi za dhulma, hivyo maelezo ya DESA (2019), Hamdok, Salisu na OECD (2013) yanafaa yatupe maswali ya kujihoji sisi wenyewe, kwamba je serikali haitoi huduma hizi muhimu ambazo zimetajwa kwenye taasisi imara? 

Kama inatoa huduma hizo, je tumefanikiwa kwa kiasi gani? Ni kwa kiasi gani serikali imepambana na rushwa? Vipi kuhusu kodi? Je, serikali ina mpango gani au haina mpango wa kusaidia kaya masikini? 

Kunusu Kaya Maskini

Kama ndivyo, vipi kuhusu Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf)? Kama imefanya basi tuamini kuwa kuna ujenzi wa taasisi imara unaendelea kufanyika la na kama haijafanya basi tuna haja ya kuhoji.

 

Lakini labda tujiulize kwa nini tuhoji? Jibu ni kwamba kwa sababu ni sehemu ya wajibu wetu katika dhana hii ya taasisi imara kama ambavyo walibainisha DESA waliposema: Watu kupata taarifa, uwazi, ushirikishwaji na uwajibikaji ni sehemu ya lengo namba 16 la SDGs. 

Hapa napo tunapaswa tujiulize, ni kwa kiasi gani sisi kama wananchi tunahoji yale ambayo yameahidiwa na wabunge, madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa ama na serikali?

 

Je, tunahoji lolote ili taarifa za mapato na matumizi ya kata au halmashauri zetu? Je, tunawahoji wabunge wetu tuliowachagua watupe taarifa za fedha za mifuko ya jimbo?

 

Je, tuunajua wajibu wetu wa kuwahoji wawakilishi wetu juu ya maendeleo yetu kila baada ya muda gani au tunasubiri kipindi cha kampeni?

 

Ni kwa kiasi gani sisi wananchi tunashiriki katika maamuzi ya masuala ya kisera yanayohusu mustakabali wetu?

 

Kama tulihoji na wawakilishi wetu hawakutupa mrejesho hapo kuna tatizo kwenye dhana nzima ya taasisi imara kwa sababu ile dhana ya usikivu wa serikali (Responsive Government) itakuwa haipo ila kama hatuhoji na huku tunadai Katiba mpya basi sisi wananchi ndiyo tatizo!

 

Utawala shirikishina

Kwa mtazamo wangu suala kwa sisi waafrika si kuwa na Katiba mpya au imara bali kuwa na taasisi imara kwa sababu hata ripoti ya Berg ya mwaka 1981 iliyosimamiwa na Bretton Woods Institutions ilibainisha kuwa tatizo kubwa Afrika ni utawala ambao si shirikishi. Kwamba nchi nyingi za Afrika zina changamoto ya kukosa usirikishwaji wa wananchi katika maamuzi ya kisera. Lakini je kwetu Tanzania lipo?

 

Hoja hii ya taasisi imara dhidi ya Katiba Mpya inabebwa na mifano hai ya nchi kama Kenya ambayo wakati walipopitisha mabadiliko ya katiba yao miaka kadhaa iliyopita sote Afrika Mashariki tulisema na kuisifu kuwa ile ni mfano wa Katiba bora katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Lakini tujiulize, bila ya busara za Rais Uhuru Kenyatta baada ya Januari, 30, 2018 Kenya isingekuwa imetapakaa damu?

 

Kwa nini? Kwa sababu Raia Odinga alijiapisha ama niseme aliapishwa pasipo halali kuwa Rais wa Kenya. Kimsingi ingawa alijiita Rais wa Watu lakini Katiba ya Kenya kama zilivyo katiba za nchi nyingi duniani zinasema 'kutakuwa na Rais mmoja tu'. 

Hivyo, kwa kitendo kile cha 'kujiapisha' na kama Rais Uhuru ambaye wakati ule alikuwa Addis Ababa kwenye Mkutano wa Umoja wa Afrika asingemuamuru waziri wake wa Usalama wa Raia aondoe askari pale Uhuru Park, huenda leo hii tungekuwa tunazungumzia  machafuko makubwa zaidi ya yale ya 2007-2008.

 

Lakini tujiulize pia, licha ya Kenya kuwa na Katiba inayoelezwa kuwa ni nzuri sana, rushwa imatapakaa kwa kiasi gani? Ni vipi uwiano kati ya aliye nacho na asiye nacho? Je, Kenya ina taasisi imara ikiwa mara kwa mara inakutana na changamoto ya kupungukiwa na chakula kiasi cha kuagiza chakula toka Tanzania?

 

Wanafalsafa wa kizungu wanasema: 'Knowing the rules is one thing, being able to apply them is another different thing' kwa tafsiri yangu isiyo rasmi ni kuwa kujua kanuni ni jambo moja na kujua namna ya kuzitumia hizo kanuni ni jambo lingine tofauti. 

Hivyo kuna wakati busara inaongoza kuliko hata sheria au kanuni kwa sababu kama Kenya wangetumia sheria inavyotaka leo huenda tusingeshuhudia amani Kenya, ni busara tu ya Rais Uhuru Kenyatta.

 

Nchi nyingine ni Afrika ya Kusini ambayo Katiba yake ya mwaka 1996 inaelezwa kuwa bora zaidi kwa ukanda wa SADC. Lakini je ni kwa kiasi gani uwiano katika ya aliye nacho na asiye nacho umekuwa mkubwa nchini Afrika ya Kusini? Ni kwa kiasi gani kuna amani nchini Afrika ya Kusini? Ni kwa nini kumekuwa na wimbi la chuki dhidi ya weusi mara kwa mara? Je, Afrika ya Kusini wana taasisi imara licha ya kuwa na katiba bora?

 

Mbona haya hatuyaoni kwa nchi ya Uingereza ambayo haina Katiba ya kuandikwa tangu msuguano wa Magna Carta karne ya 17 mpaka leo na bado wananchi wanapata huduma zote za msingi, kuna uwajibikaji, utawala wa sheria, wananchi wanashirikishwa kama tulivyoona kwenye Brexit na rushwa inaogopwa. 

 

HOJA YA MSINGI NI IPI?

Kwa maoni yangu ni kwamba, tusipojenga hoja thabiti kwenye haya maeneo ya taasisi imara yaliyoainishwa na Umoja wa Mataifa na kujielekeza kwenye katiba mpya basi hata kama ikitokea tukapata katiba mpya huko baadae, kama hatujajingea misingi bora kwenye haya ya kuwa na taasisi imara tutakuwa tumejidanganya na  tutakuwa kama Kenya, Nigeria au Afrika Kusini.

Licha ya kuwa na katiba zinazoelewa kuwa nzuri lakini bado zinakabiliwa na changamoto za rushwa, kutokuwepo kwa mgawanyo sawa wa rasilimali, usimamizi hafifu wa rasilimali na kukosekana kwa uwajibikaji.

 

NINI KIFANYIKE?

Mosi, tujenge tabia ya uwajibikaji, hili linafaa kupigiwa kelele na watu wote. Uwajibikaji uanzie kwa mtu binafsi ama mtu mmoja mmoja. Tujenge utamaduni wa kuwajibika kitaasisi (institutional culture). Uwajibikaji usiwe kwa sekta za umma tu au Serikali bali hata sekta binafsi.

 

Rais Samia anaonesha wazi kuwa anataka kujenga uwajibikaji wa kitaasisi pale alipowaomba wabunge waikosoe serikali na kuielekeza pasi na kupepesa macho. Lakini pia alieleza hayo alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari Jumatatu tarehe 28 Juni, 2021 pale Ikulu, Dar es Salaam.

Alisema wazi kuwa hakatai serikali yake kukosolewa bali anaekosoa atoe na njia mbadala ya kile alichokikosoa, lakini pia mtu anapokosoa jambo azingatie adabu na heshima ya kiafrika. Haya ndiyo aliyosisitiza. 

 

Hapa tunaona Rais anataka kutujengea tabia ya kushiriki katika maamuzi na kuhoji mambo sambamba na kushauri suluihisho akitazama dhana ya ushirikishwaji wa wananchi katika ujenzi wa taasisi imara.

Jambo la pili ni kuimarisha sekta binafsi. Sekta binafsi ni muhimu katika uchumi na maendeleo ya nchi yotote ile. Sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi wa kisasa. Lakini si kila mradi unaweza kuendeshwa na sekta binafsi, kwa mfano, miradi kama bandari, reli, ujenzi wa barabara, madaraja, viwanja vya ndege bado vinaweza kubaki kwa serikali kwa kuzingatia athari zake kwa maslahi ya taifa.

Ni vyema kutambua kuwa kuna athari pia sekta binafsi ikiwa na ushawishi mkubwa katika maamuzi ya serikali. Kwa mfano nchini Afrika ya Kusini nchi iliwekwa mikononi na familia ya Gupta  katika kile kilichoitwa State-Capture na hatimaye Rais wa wakati ule, Jacob Zuma kukutwa na hatia ya rushwa na kufungwa miezi 15 hivi karibuni. Wakati ninaandika makala haya suala la Zuma liikuwa linasababisha vurugu kwenye nchi hiyo yenye katiba ‘bomba’!

Hivyo basi, kuna umuhimu wa kuzingatia athari hasi za sekta binafsi pia endapo zinakuwa na ushawishi uliopitiliza katka maamuzi ya Serikali kama ilivyobainisha ripoti ya OECD ya mwaka 2015 yenye kichwa cha habari: 'Kujenga taasisi zenye kuleta matokeo, zinazowajibika na zinazoshirikisha wananchi wote.'

Sambamba na hilo uimarishwaji wa vyombo vya habari ni muhimu pia katika kujenga taasisi imara lakini pia uzingatiaji wa sheria katika utoaji habari ni muhimu kwa upana wake kwa sababu hata Hayati Mwalimu Nyerere alipata kusema: “Uhuru bila mipaka ni fujo.”

Kwa mantiki hiyo ile kauli ya Rais Samia aliyosema tumpe muda ajenge uchumi kwanza na kwa kuzingatia hoja ya ujenzi wa taasisi imara ambayo inataka serikali ijenge miundombinu wezeshi ya kiuchumi kama barabara, reli ya SGR, bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, ununuzi wa meli, ujenzi wa bandari, hospitali, vifaa vya tiba, ujenzi wa  shule na utoaji wa elimu msingi bure,  huduma za afya na maji binafsi naiona ni hoja kubwa.

Nasema hivyo kwa sababu hata kama serikali itakubali katiba mpya lakini rushwa ikatamalaki kama Nigeria au migogoro ikajitokeza kama Ethiopia au Afrika Kusini hatutakuwa tumekidhi hoja ya kuwa taasisi imara.

Naomba nirejee kunukuu maneno ya OECD (2015) ambao nao walinukuu ripoti ya UN kuonesha umuhimu wa kujenga taasisi imara kwamba ujenzi wa taasisi imara huifanya serikali kuwa sikivu, yenye sera zenye usawa, uwazi na zinazowajengea imani wananchi wake. 

Lakini pia kunakuwa na mapambano dhidi ya rushwa, matumizi mazuri ya rasilimali, uwepo wa vyombo mbalimbali vya habari vinavyoweza kuwapa wananchi taarifa mbalimbali zenye kuweza kuwafanya waiwajibishe serikali yao na kuifanya iwatumikie ipasavyo. Hiyo ndiyo misingi ya taasisi imara.

Tunachoweza kujiuliza ni kuwa je serikali haijayafanyia kazi hayo? Kwa mfano Tanzania ni ya kwanza katika nchi za Afrika kwa mapambano dhidi ya rushwa kwa mujibu wa ripoti ya Transparency International ya mwaka 2019.

Je, hili la mapambano dhidi ya rushwa linahitaji katiba mpya au taasisi imara?

Tanzania imeingia katika uchumi wa kipato cha kati cha chini na kwa mujibu wa hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni kwamba kuna kila dalili Tanzania ikaenda kwenye kipato cha kati cha juu.

Je, hoja hapa ni katiba mpya au kuendeleza ujenzi wa taasisi imara ili kuweza kufikia azma hiyo ya kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu?

Kimsingi, kwa maoni yangu haya ndiyo mambo ya muhimu sana kupigiwa chapuo na wapigania katiba mpya kwa sababu kuna ombwe kubwa la wananchi kujua wajibu wao kwa Serikali yao kama alivyobainisha Fosu (2018) katika chapisho lake, 'Governance and Development in Africa'.

Hivyo muhimu kwanza wananchi wajue ushiriki wao katika ujenzi wa taasisi imara ndipo baadae tunaweza kuhamia kwenye hoja ya Katiba mpya. Haya ni maoni yangu.

Kwa mantiki hiyo tukiwa tunahoji kuhusu katiba mpya ni vema pia kujiuliza ni kwa kiasi gani katiba mpya itatujengea taasisi imara?

Ikiwa mifano ya Kenya na Afrika Kusini ambazo zina katiba zinazoelezwa kuwa nzuri bado katiba hizo hizo zimeshindwa kuondoa tofauti ya kipato kati ya walio nacho na wasio nacho na kuondoa ubaguzi wa kikabila. Huko siyo suala la katiba bali kumekosekana ujenzi wa taasisi imara.

Je, ni vipi katiba mpya itatuhakikishia uwepo wa amani ya kutosha hata wakati wa changamoto kama iliyotufika mwaka huu ya kuondokewa na Rais akiwa madarakani?

Hivyo basi kwa maoni yangu naona tunahitaji  kujenga taasisi imara kama ambavyo Rais anajielekeza huko kwa kutujengea dhana ya kujiwajibisha kitaasisi (institutional culture) kwamba Bunge lifanye kazi yake ipasavyo kwa mujibu wa sheria, mahakama ifanye kazi yake ipasavyo kwa mujibu wa sheria na serikali kuu ifanye kazi yake huku mihimili hiyo ikiheshimiana.

Ninaamini hiki ndicho anachotaka kukijenga Rais Samia na ndiyo maana aliomba tumpe muda ajenge uchumi kupitia ujenzi wa taasisi imara. Mimi ninaona dhamira yake njema na ninamuunga mkono.

Mwandishi wa makala haya ni mbobezi katika masuala ya diplomasia. Mawasiliano yake ni +255 719 258 484

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/91e280fc32fd35d64f6b305972dcae5b.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Abbas Mwalimu 

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi