loader
Dstv Habarileo  Mobile
Watumishi wa  Afya wawe waadilifu

Watumishi wa  Afya wawe waadilifu

KATIKA gazeti letu hili toleo la jana pamoja na toleo la leo, kuna taarifa zinazohusiana na watumishi wa umma katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu na ukosefu wa maadili wakati wakishughulikia suala la ugonjwa wa corona (Covid-19).

Juzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi alitangaza kuwasimamisha kazi watumishi tisa wa Kitengo cha Upimaji wa Covid-19 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Kwa mujibu wake, kitendo cha watumishi hao kutokufika kazini bila kutoa taarifa kwa uongozi juzi na jana ni utovu wa nidhamu. Alisema serikali haiwezi kuvumilia watumishi wasio na nidhamu na wanaodharau kutekeleza majukumu.

Kwa upande wa SMZ, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (Zaeca) imetangaza kuwashikilia watu 11 wakiwemo wafanyakazi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa kutengeneza vyeti bandia vya chanjo ya Covid-19 kwa watu mbalimbali wanaosafiri kwenda nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Zaeca, Ahmed Khamis Makarani, jumla ya vyeti bandia 548 vimetolewa kwa wasafiri wa nje ya nchi. Alisema watumishi waliokamatwa ni kutoka katika Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto Makao Makuu Mnazi Mmoja pamoja na watumishi wa Kitengo cha Chanjo ya Covid-19 mjini Unguja.

Wafanyakazi wengine waliokamatwa kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili ni kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Kitengo cha Ukaguzi wa Wageni wanaoingia nchini pamoja na sekta ya utalii.

 

Taarifa hizi mbili kwetu sisi ni za kusikitisha kutokana na ukweli kuwa, katika janga hili la ugonjwa wa Covid-19, watumishi wa umma hasa wa sekta ya afya wanapaswa kutanguliza mbele uzalendo na maslahi ya taifa ili kuhakikisha taifa linabaki salama wakati wa ugonjwa huo ambao wimbi la tatu limeikumba Tanzania.

Vitendo vyovyote vile vinavyohatarisha usalama wa taifa kwa hakika havipaswi kuvumiliwa na mamlaka husika hazina budi kuchukua hatua stahili kwa mujibu wa sheria.

Tunaamini watumishi wa umma wanayo maadili na wanapaswa kuyafuata na pia wanajua masuala ya uzalendo na uadilifu, hivyo kufanya vitendo vya kukiuka hayo, ni kujiingiza katika utovu wa nidhamu, lakini pia kuhatarisha usalama wa taifa hasa katika eneo lao nyeti la kudhibiti ugonjwa huo hatari wa Covid-19.

Kwa msingi huo, tunawaomba watumishi wa umma kuzingatia maadili ya kazi zao, kuheshimu miiko ya kazi zao, uadilifu, kutanguliza maslahi ya taifa na uzalendo ili kutoliingiza taifa katika majanga makubwa. 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/214adcec68a2ca52db88b8bd5bb35cac.jpeg

Miradi ya Maendeleo katika halmashauri za Serengeti, ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi