loader
Dstv Habarileo  Mobile
Hifadhi ya Serengeti,   inufaishe pia Mara’

Hifadhi ya Serengeti,  inufaishe pia Mara’

WIKI hii yamefanyika makabidhiano ya ofisi kati ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Robert Gabriel, ambaye kwa sasa ni mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mkuu mpya wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi.

Yaliyojiri katika tukio hilo lililofanyika mjini Musoma, ndiyo kiini cha makala haya yenye mengi ya kujifunza.

Gabriel, kabla kukabidhi ofisi, alitoa taarifa fupi iliyotokana na uzoefu wake, katika kipindi kifupi alichokuwa mkuu wa Mkoa wa Mara na kumshauri Hapi kuanzia alipoishia.

Taarifa yake ilihusisha kuboresha utalii mkoa wa Mara, kumtegemea Mungu, uthubutu, kukubali kuaminika, juhudi, maarifa, hekima, busara na kujituma kwa kushirikisha viongozi wengine ili kuleta maendeleo.

Anasema alibaini kuwa, hifadhi maarufu Tanzania na duniani kote ya Serengeti haijatangazwa kwa kiwango cha kutosha, hali ambayo imesababisha kudhaniwa ipo katika Mkoa wa Arusha wakati ni mali halali ya Mkoa wa Mara.

Ni kutokana na hali hiyo, Mkoa wa Mara umekuwa haunufaiki sana na hifadhi yake hiyo kutokana na watalii kutotokea Mara. Bila kufafanua, inafanana na Kenya ilivyokuwa inatangazia dunia kwamba Mlima Kilimajaro uko Kenya wakati si kweli.

Pia Gabriel anasema katika kipindi kifupi amefanyia kazi jengo la iliyokuwa Hoteli ya Musoma ambayo iliteketea kwa ajali ya moto.

Kwamba anaona umuhimu wa kuhifadhi historia ya Taifa kwani kumbukumbu zinaonesha kwamba Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa Musoma mjini, alikuwa akifikia katika hoteli hiyo ya kitalii.

Anabainisha kwamba hatua alizokwishachukua kuhusu hoteli hiyo ni kuelekeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kukadiria gharama za kuijenga upya ili ianze kufanya kazi, kwani itakuwa ya kichocheo mapato na ajira.

Kwa upande wa Sekta ya Madini anasema mara ina utajiri wa madini ya dhahabu, chuma na ardhi ambayo inakubali aina nyingi za mazao ya kibiashara na ya chakula kama vile korosho, mkonge, pamba na kahawa.

Anasema Waziri wa Madini alishaandikiwa barua kuhusu nia ya mkoa huo kufanya maonesho ya kitaifa ya madini ili kuongeza wigo wa uwekezaji katika eneo hilo.

“Katibu tawala alishatafuta eneo la kufanyia maonesho hayo na ilipendekezwa yafanyikie Tarime kwa kuwa ndiko yaliko madini mengi. Kuna mwongozo wa fursa za uwekezaji katika mkoa huu, utauona naamini utafaa,” anasema Gabriel akimwelekeza Hapi.

Anasema alipoingia Mara akitokea Geita alipokewa na viongozi wa Dini ya Kikristu na Kiislamu ambao pamoja na maombi walimuusia kumtegemea Mungu zaidi katika kila jambo.

“Kazi yangu ilikuwa nyepesi kwa sababu Mungu alinitangulia, Mungu akitangulia mwanadamu ananufaika,” anasema Gabriel.

Ndani ya muda mfupi aliyokuwa akiongoza mkoa wa Mara, anasema alifanya mikutano minane ya mabaraza ya madiwani na anasema mkutano wa Baraza la Madiwani wa Wilaya ya Tarime, ulikuwa wa ‘moto’ kuliko mingine yote.

Anaelezea alichobaini wilayani humo kuwa ni siasa kugeuzwa bidhaa ghali kuliko maelezo, kwamba mtu kugombea na kupata uenyekiti wa serikali ya mtaa bila Sh milioni 50 ni sawa na ndoto za alinacha, haiwezekani.

Hali hiyo anaihusisha na kudorora kwa maendeleo, kwani inasababisha viongozi kupatika kwa kutumia rushwa na hivyo wanapokuwa madarakani, wanafanya urasimu hata usiyokuwa na sababu ili kupata pesa za kurejesha walichotumia katika harakati za kuwania uongozi badala ya kuwatumikia wananchi.

Gabriel anasema alikutana na wananchi wa kada tofauti ili kujua changamoto zao, alikagua miradi na kutembelea mpaka kati ya Tanzania na Kenya.

Mambo aliyobaini katika jamii anasema yalimwezesha kujiwekea malengo na mikakati ambayo ikitekelezwa kwa ufanisi itasababisha matokeo chanya katika maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi mkoani humo

Lengo lake kuu katika kutekeleza majukumu yake linaelezwa naye kuwa ni kufikia matarajio ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa maendeleo ya mkoa wa Mara.

Anasema hali ya usalama aliikuta na kuiacha vizuri, hapakuwa na uvunjifu mkubwa wa usalama wenye kuweza kusababisha uvunjifu wa amani na kwamba alibaini kiini cha hilo ni Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo kwani ni ina watu mahiri na wabobezi wa mambo.

Changamoto ya kukosekana kwa nidhamu katika ukusanyaji na utumiaji wa fedha za umma, anasema aliibaini katika mamlaka zilizopewa dhamani hiyo na kwamba katika baadhi ya maeneo hakuna uadilifu wa kutunza rasilimali za umma.

“Kuna changamoto ya halmashauri kutoa asilimia 40 ya mapato yake kwa shughuli za maendeleo, hali inayosababisha mkwamo kwenye maeneo mengi. Niliamuru halmashauri zote kupeleka fungu hilo kama inavyotakiwa ili maendeleo yasikwamishwe,” anasema  Gabriel.

Anasema pia alibaini kuwepo kwa tabia ya kula fedha ambazo siyo za halmashauri na kushidwa kuzirudisha na kwamba hali hiyo imezaa madeni ambayo Hapi atakutana nayo.

Ili Serikali iweze kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inahitajika fedha lakini anasema kuna tatizo katika makusanyo ya mapato ya ndani, kiasi kwamba hata takwa la kisheria la kila halmashauri kupeleka asilimia 10 ya mapato yake kwa wanawake, vijana na walemavu kwa asilimia kubwa halitekelezwi.

Anaitolea mfano Halmashauri ya Tarime kwamba ina mradi ambao inashirikiana na mdau/mwekezaji kuutekeleza, kwamba yenyewe imetoa fedha na mdau amejenga mabanda ambapo mkataba baina ya pande hizo mbili ni kugawana mapato yanayotokana na malipo ya kodi za pango.

“Lakini inaonesha halmashauri inapata kiasi kidogo sana kwa mfano kodi ya pango ni Sh 150,000, halmashauri inapata Sh 20,000 mdau anapata Sh 130,000 na ni mkataba wa miaka 15,” anabainisha RC Gabriel.

Anasema alielekeza mradi huo ukaguliwe, thamani halisi ya fedha zilizotumika kuujenga ijulikane na mkataba upitiwe upya.

Pia anasema alishauri halmashauri zote kutoingia mikataba hususani ya uwekezaji bila kushirikisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, ili kulinda maslahi ya umma.

Ikumbukwe utaratibu unampa mtu anayeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa, wiki mbili za kupumzika tangu anapoapishwa, lakini kinachoonekana kwa Robert Gabriel ambaye kwenye gari lake hutembea na buti za kazi kuwa shughuli zote hizo alizifanywa ndani ya muda usiyozidi wiki mbili tangu alipoapishwa, muda aliyopaswa kupumzika.

Wakati wa Jukwaa la Biashara lililofanyika Geita mwaka 2018 yeye akiwa mkuu wa mkoa huo alisema ukishakuwa kiongozi wa umma, basi ujue muda wako wa kulala ni mdogo sana.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/5fb5d124660f926de4b86fcfd822d367.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Editha Majura

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi