loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wakinga wanasifiwa sana kwa uchapakazi

Wakinga wanasifiwa sana kwa uchapakazi

LEO katika mwendelezo wa makala za utamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali ya Tanzania, tunaangazia jamii ya Wakinga.

Wakinga ni kabila la watu wanaoishi katika Mkoa wa Njombe wilayani Makete. Ni mojawapo ya makabila makubwa ya wenyeji mkoani Njombe, makabila mengine yakiwa ni Wabena na Wapangwa.

Kabila la Wabena liko Wilaya ya Njombe na eneo la Malangali likiwa linapakana na Wilaya ya Ulanga na Wilaya ya Kilombero (Mkoa wa Morogoro), na Wapangwa wako Wilaya ya Ludewa.

Yapo pia makabila madogo kama vile Wamahanji, Wakisi, Wamanda, Wamagoma n.k. ambao kwa ujumla wao wanachukua asilimia 6 tu ya watu wa Mkoa wa Njombe.

Lugha inayozungumzwa na Wakinga inaitwa Kikinga. Asili ya lugha hii, kwa mujibu wa machapisho, ina mkanganyo kidogo: baadhi ya taarifa zinaeleza kuwa asili ya lugha hii ni misitu ya Kongo, huku taarifa nyingine zinaeleza kuwa asili ya jamii ya Wakinga ni Afrika Kusini na kwamba waliingia eneo la Ukinga kwa kutokea Mkoa wa Ruvuma.

Koo za Wakinga

Jamii ya Wakinga ina koo mbalimbali maarufu, kwanza ukoo wa Sanga, ambao ndiyo ukoo mkubwa na ndiyo ulikuwa unatawala jamii yote ya Wakinga.

Koo nyingine ni pamoja na ukoo wa Kyando; Mahenge; Chaula; Tweve; Luvanda; Pila; Lwila; Ndelwa; Mbilinyi; Msigwa na Mbwilo. Hizi ni baadhi tu ya koo za jamii ya Wakinga.

Yapo machapisho yanayobainisha kuwa wilayani Makete kuna Wakinga wa aina tofauti na tabia zao zinatofautiana kulingana na maeneo wanayotoka.

Mosi ni Wawanji. Hawa wanatokea pembeni kabisa mwa Wilaya ya Makete jirani na Chimala, ni maarufu kwa kilimo cha mahindi na viazi, pia ni wafanyabiashara. Lakini wanasemwa kuwa wana tatizo la uchawi ujulikanao kama unyambuda”, na pia wanawake wao huwapiga sana waume wao.

Pili ni Wamahanji wanaotokea eneo la Bulongwa, Makete na Kipagalo. Ni wafanyabiashara na wasomi wazuri sana, wanapenda sana kilimo cha ngano, wanapenda sana kujisifia na pia wanapenda michezo. Ukioa binti kutoka jamii hii basi ujue kuwa wewe ndiye umeolewa kwani inasemwa kuwa wanapenda sana kuwafanyia dawa waume wao.

Tatu ni Wamagoma; wanatoka Tarafa ya Magoma, ni majirani na Wamahanji na wanafanana sana kitabia isipokuwa hawa wamezidi kwa uchawi na wizi. Inasemwa kuwa huko Magoma si ajabu kusikia kwamba mchungaji fulani ni mwizi ama mchawi.

Nne ni Wakinga halisi; hawa wametofautiana kutokana na kata zao. Waliopo katika Kata ya Isapulano ni wakulima wa viazi, mahindi na ngano, na ni wacheshi sana, lakini kwao shule si muhimu sana. Ni wao na biashara tu, na kwamba wafanyabiashara wengi wakubwa wa Kikinga wanatoka kata hii na wanapenda sana kuoana katika umri mdogo.

Kata ya Iwawa ndiyo kata inayounda mamlaka ya mji mdogo, na watu wa hapo ni wapole, wasomi kiasi na wanapenda biashara. Biashara yao kubwa ni mbao na miti, ila wana tatizo la ulevi wa kupindukia, hii ndiyo sababu ya kuwa na idadi kubwa ya watu wanaoishi na maambukizi za virusi vya ukimwi (VVU) na umasikini wilayani Makete.

Shughuli za kiuchumi

Wakinga, kama walivyo Wabena, ni wachapakazi sana. Inasemwa kuwa mkoloni wakati akiitawala Tanganyika aligundua makabila matatu ndio wachapakazi za mikono na wenye kujituma na waaminifu kazini kuliko makabila yote. Makabila hayo ni: Wabena toka Njombe; Wakinga toka Makete na Waha toka Kigoma.

Wilaya ya Makete inategemea zaidi barabara mbili kuu, moja ya kutoka Njombe na nyingine kutoka Mbeya, lakini inasemwa barabara pacha zinazoingia mkoani Mbeya kipindi cha mvua huharibika na huwa hazipitiki.

Ubovu wa barabara hizo umechangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha usafirishaji wa pembejeo na hivyo hazifiki kwa wakati. Lakini pia umechangia kukwamisha usafirishaji wa mazao kama matunda, viazi, pareto, mazao ya mbao, ngano, mahindi na mengine kwenda sokoni.

Kutokana na ubovu wa barabara hizi, mazao mengi toka Wilaya ya Makete, yakiwamo ya mbao. yamekuwa yakikwama kusafirishwa na hivyo kukwamisha ukuaji wa uchumi wilayani humo na hivyo kuwakosesha wananchi kipato, ajira na mahitaji yao ya kila siku.

Mahindi, ngano, shayiri na matunda ambayo yanalimwa kwa wingi maeneo ya Bulongwa na Matamba yanaozea mitini. Watu wachache wenye uwezo wanabeba kichwani umbali mrefu kwenda kuuza. Wenyeji pia wana zao la miti ya ulanzi.

Pia ubovu wa barabara wilayani humo umepandisha bei ya bidhaa za madukani ambazo zinaingizwa wilayani humo kupitia Mbeya na Njombe. Bei ya bidhaa nyingi ni ya ‘kuruka’ hasa katika maeneo ambayo barabara zimeharibika.

Japo Wakinga ni wafanyabiashara maarufu katika mikoa mbalimbali nchini hasa Mbeya, Iringa, Dar es Salaam, Ruvuma, Rukwa na maeneo mengine lakini wamekuwa wakishindwa kuwekeza wilayani kwao kutokana na barabara nyingi kuwa mbovu na kutopitika wakati wote.

Mazingira ya msiba katika jamii ya Wakinga

Katika jamii ya Wakinga, msiba unapotokea, wafiwa wa familia iliyofikwa na msiba hujawa na huzuni ya kuondokewa na mpendwa wao. Huzuni hiyo huambatana na vilio na kelele ambazo aghalabu huwavuta majirani na wapita njia kuja kuungana na wafiwa ili kuomboleza msiba ulioifika familia husika.

Yeyote anayekuja eneo la msiba huangua kilio. Vilio hivyo ndivyo huwavuta watu wengine na kutambulisha kuwapo kwa msiba katika familia husika.

Zipo njia nyingine mbalimbali zinazotumiwa kuwajulisha watu wa vijiji vya jirani kuhusu msiba. Njia mojawapo ni kupiga kelele maalumu zinazoashiria msiba ambapo mpigaji husimama juu ya kilima.

Mtu huyo anapopiga kelele hizo hutaja jina la marehemu na jina la ukoo uliopatwa na msiba. Njia ya pili ambayo ni maarufu ni kutumia mbiu inayopigwa kwa kutumia pembe ya mnyama aitwaye paa.

Pembe hiyo kwa lugha ya Kikinga huitwa “lukelema”. Mpiga-mbiu husimama juu ya kilima kinachoelekea vijiji jirani ili mvumo wa mbiu uweze kufika katika vijiji hivyo.

Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya sasa yanayohusisha mwingiliano wa imani, si misiba yote ambayo lukelema hutumiwa.

Endapo marehemu ni muumini wa dini ya Kikristo, waombolezaji huitwa kwa kupiga kengele kanisani alikokuwa akiabudu. Kengele hii hupigwa kwa vituo vya miimbo mitatu-mitatu na kupumzika kwa dakika kadhaa na kuendelea.

Namna hii ya upigaji kengele huashiria kuwapo kwa msiba. Baada ya utoaji wa taarifa kwa njia hizo tofauti, wanajamii huanza kukusanyika eneo la msiba. Huanza kuomboleza kwa kulingana na imani ya marehemu.

Imani kuhusu kifo

Wakinga wanaamini kuwa mtu akifa mwisho wa safari yake ni mahali maalumu panapoitwa “kumahame” au mahameni. Huko mahameni anaenda kuishi pamoja na wazee wake au ndugu zake waliokufa zamani.

Mahameni ni mahali ambapo kila ndugu wa ukoo anapofariki, lazima roho yake ipelekwe hapo kwa matendo maalumu ya kimila yanayoambatana na tambiko.

Watendaji wa tambiko hutenda vitendo ambavyo huambatana na maneno maalumu ambayo yana sifa ya ughani. Kisha hufurahi kwa kuimba nyimbo na kucheza ngoma za asili za Kikinga.

Katika utaratibu huu ni jambo gumu kutenganisha matendo ya dhati na matendo ya kisanaa (fasihi).

Jamii ya Wakinga wanaamini kuwa hata kama mtu atakufa na kuzikwa mahali pengine, utaratibu hufanywa ili kuihamisha roho ya marehemu na huizika tena kwenye kaburi dogo linaloandaliwa mahali ambapo watu wote wa ukoo wake huzikwa.

Katika muktadha huu, hatima ya maisha ya Wakinga si pale ulipozikwa mwili, bali ni mahali inapopelekwa roho yako baada ya uhamisho, wanaita “kutekela”.

Wakinga wanaamini kuwa uhamisho wa roho ya marehemu kwenda mahameni unapokamilika, ndipo walio hai pamoja na wafu huwa salama.

Inabainishwa kuwa kuna mizimu ambayo huwadhuru watu, mpaka ifungwe ndipo hali huwa salama. Na kuwa endapo taratibu zisipofuatwa katika mazishi kuna baadhi ya mizimu huweza kugeuka na kuwadhuru wanadamu walio hai.

Wakinga wanapofanya mchakato wa uhamisho wa roho za wafu huambatana na nyimbo za kughani kwa kutamka baadhi ya maneno. Wakishamaliza kumhifadhi mahameni, husherehekea kwa kunywa pombe na kuimba nyimbo maalumu za kughani.

Maneno ya ughani ambayo yanaghanwa na wafiwa wakati wa misiba yanadhihirisha kuwa ndugu waliokufa wako katika kusanyiko moja na wanakutana.

Mathalani, katika chapisho moja la kitafiti kuhusu misiba ya Wakinga inaelezwa kuhusu msiba wa mtoto mmoja katika kijiji cha Maliwa mwaka 2017, maneno ya ughani yaliyoghanwa na wafiwa yalihusisha kutuma salamu kwa waliotangulia, akiwamo baba yake marehemu.

Walisema “Vasamtsyakevoni’ (Uwasalimie wote), Ukamsamtsyakenu dadajo” (Ukamsalimie na baba yako).

Kuendeleza Umoja na Ushirikiano

Umoja na ushirikiano katika jamii ya Wakinga upo kati ya walio hai kwa walio hai, na kati ya wafu na walio hai. Ushirikano na walio hai hujidhihirisha nyakati za misiba na matukio mengine ya kijamii.

Mtu asiposhiriki huweza kupewa adhabu fulani na kutoimbiwa, wakazika tu na kutawanyika bila kurudi tena nyumba yenye msiba kwa ajili ya kuwafariji wafiwa kwa nyimbo za maombolezi.

Nyimbo za kuliwaza wakati wa msiba hulenga “kumsaidia mtu aliyefikwa na msiba ajisikie vizuri” au “ili mfiwa asiumie zaidi kutokana na huzuni anayopitia”.

Kwa sababu hiyo, nyimbo zinazolenga kuliwaza huambatana na tumaini kwamba ipo siku ambayo wafiwa wataonana na ndugu yao aliyeondoka.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au bhiluka@gmail.com

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/ed8bc1aebbc7dd93eefb351ff4fd7a38.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi