loader
Dstv Habarileo  Mobile
Watu 80 wafariki kwa  mafuriko Ujerumani

Watu 80 wafariki kwa mafuriko Ujerumani

TAKRIBANI watu 80 wamefariki dunia na zaidi ya 100 hawajulikani walipo nchini Ujerumani, kutokana na mafuriko makubwa kuwahi  kutokea nchini humo.

Mvua kubwa zilizorikodiwa kunyesha Magharibi mwa Ulaya zimesababisha mito kujaa maji na kufurika na kusababisha taharuki katika maeneo mbalimbali nchini Ujerumani.

Nchini Ubelgiji nako imeripotiwa takribani watu 12 wamekufa kutokana na hali mbaya ya hewa ambayo viongozi wa kisiasa wamelaumu kuwa chanzo chake ni mabadiliko ya hali ya hewa.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel aliahidi serikali kutoa msaada kwa waathirika wote wa mafuriko hayo.

Majimbo ya Rhineland-Palatinate na Kaskazini Rhine-Westphalia ndiyo yameathirika zaidi na mafuriko hayo.

Waziri Mkuu wa Jimbo la Nord Rhine-Westphalia, Armin Laschet alipotembelea maeneo yaliyoathirika, alisema hali hiyo ya hewa inatokana na ongezeko la joto duniani.

“Tutakabiliana na hali hii mara kwa mara, hii inamaanisha tunahitaji kuongeza kasi ya kuchukua hatua za kulinda mazingira yetu kwa sababu mabadiliko ya hali ya hewa si tatizo la nchi moja,” alisema Laschet.

Wanasayansi wameonya mara kwa mara kwamba ushiriki wa binadamu katika mabadiliko ya hali hewa utasababisha mvua kubwa kama hiyo iliyonyesha katika bara la Ulaya.

Uholanzi nayo imeathirika vibaya na mafuriko hayo ambayo pia yameathiri nchi za Luxembourg na Switzerland.

 

Nchini Ujerumani, wilaya ya Ahrweiler watu 1,300 hawajulikani walipo kwa mujibu wa mamlaka za nchi hiyo.

Msemaji wa serikali za mitaa alisema mitandao ya mawasiliano imeharibiwa hivyo ni ngumu kuwasiliana na watu.

Katika kijiji cha Schuld kinachokadiriwa kuwa na idadi ya watu 700 almanusura kizolewe chote na mafuruko.

Bwawa kubwa la Rurtalsperre lililopo jirani na mpaka wa Ubelgiji limejaa maji na kusababisha mafuriko makubwa katika maeneo jirani.

Takribani polisi 15,000 na vikosi vya dharura wamesambazwa maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutafuta na kuokoa watu, huku helkopta zikisaidia kubeba watu waliokuwa wamejihifadhi kwenye mapaa ya nyumba zao.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/bfcd397e6edc0f4767108bdec6909d0a.jpg

Waziri wa Uingereza, Boris Johnson ametengua uteuzi wa ...

foto
Mwandishi: BERLIN, Ujerumani

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi